Thursday, September 8, 2016

Samia: Viongozi wa Vijiji na Kata watangaze mali zao na kujaza fomu za viapo.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia katika ufunguzi wa jengo la ofisi za sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya kusini lililopo mjini Mtwara.

Makamu wa Rais wa Tanzania-Samia Suluhu Hassan akiwa na waziri wa nchi utumishi na utawala bora-Angela Kairuki na mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego


Juma Mohamed, Mtwara

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameitaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhakikisha fomu za viapo vya uadilifu na kutangaza mali, zinajazwa na viongozi kuanzia ngazi za chini ikiwa ni pamoja na vijiji na kata.
Akizungumza mkoani hapa katika ufunguzi wa jengo la ofisi ya sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya kusini, amesema wapo viongozi wa ngazi za chini ambao wanajilimbikizia mali huku akimtaja diwani mmoja wa mkoa wa Lindi ambaye amekamatwa akisafirisha korosho tani Nne visivyo halali.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego.

“Lakini nataka nikuambie kamishna, sisi mnaotuletea fomu tutangaze mali zetu hatuna chochote kuliko hawa wa chini..huku chini kuna watu wamejilimbikizia mali nyingi na itabidi zile fomu tunazojaza sisi mjipe mzigo mkubwa zaidi ziende chin zaidi watu wajaze watangaze mali zao na muwakague..” alisema.
Naye, waziri wa nchi ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Angela Kairuki, amewataka watanzania wote kujiamini na kuitumia ofisi hiyo iliyowekwa kwa ajili ya kukuza maadili ya viongozi wa umma.

Waziri wa nchi ofisi ya Rais, utumishi na utawala bora, Angela Kairuki, akihutubia katika halfa la ufunguzi wa jengo la ofisi za sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya kusini lililopo mjini Mtwara.

“Kupitia kwako mhe. Makamu wa Rais, mimi niendelee kuomba hadhara hii pamoja na watanzania wote wanaotusikiliza, tujiamini ofisi hii ni yenu imewekwa kwa ajili yenu katika kuhakikisha tunatunza maadili ya viongozi wa umma, katika kuhakikisha hakuna ubadhirifu wa mali za umma..” alisema Kairuki.
Akitoa taarifa ya jengo hilo, kamishna wa maadili ya viongozi wa umma Jaji Mstaafu Salome Kaganda ameeleza idadi ya viongozi waliorejesha matamko yao ya rasilimali na madeni kuwa ni 1,286 mpaka mwezi Juni mwaka huu.

Kamishna wa maadili ya viongozi wa umma nchini, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo la ofisi za sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya kusini.

Makamu wa Rais yupo mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo baada ya uzinduzi wa jengo hilo lililojengwa kwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 2.1, anatembelea kiwanda cha kuchakata gesi asilia cha Madimba kabla ya kumalizia ziara yake wilayani Tandahimba.

Baadhi ya viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa jengo la skretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kanda ya kusini, lililofunguliwa na makamu wa Rais wa Tanzania-Samia Suluhu Hassan.




No comments: