Tuesday, April 24, 2012

Monday, April 23, 2012


HII NDIYO SIMBA SC, MNYAMA MKALI ANAYEISHI KATIKATI YA JIJI


Kikosi cha Simba msimu huu

JIONI hii Simba SC imeifunga Moro United mabao 2-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, na sasa inahita pointi moja tu katika mechi zake tatu zilizobaki ili kutawazwa rasmi kuwa mabingwa.
Simba wanawavua ubingwa wapinzani wao wa jadi, Yanga SC ambao msimu huu ‘wamefulia’ kiasi cha kukosa hata nafasi ya pili, ambayo ingewawezesha kucheza michuano yua Afrika mwakani.
Ni ukweli usiopingika kwamba chachandu ya soka ya Tanzania ni klabu mbili kongwe, Simba na Yanga, ambazo kwa sababu hiyo, zina mashabiki lukuki nchini.
Maelfu ya Watanzania wanaweza kuziunga mkono timu za majimboni mwao, wilayani mwao, mikoani mwao, lakini mwisho wa siku wanabakia kuwa na timu ambazo zipo kwenye damu zao, Simba au Yanga.
Ni kwamba, Tanzania ina wapenzi wawili tu wa soka, mmoja ni wa klabu ya Simba na mwingine wa Yanga. Hata wale ambao wamejijengea umaarufu kama mashabiki wa timu fulani, mfano Yamungu aliyekuwa Reli Morogoro na Mang'ombe aliyekuwa Pamba FC ya Mwanza, nao pia inadaiwa kuna timu waipendayo miongoni mwa hizo.
Hakuna ubishi, Simba na Yanga ndiyo maana halisi ya soka Tanzania.

Je, waijua vyema Simba SC?
Jezi za rangi nyekundu na nyeupe ndio utambulisho wao dimbani, rangi ambayo inatumiwa na klabu nyingi kubwa za Ulaya, hususan England, kama Liverpool, Manchester United na Arsenal.
Unapoizungumzia Simba, unamaanisha klabu kubwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, ambayo ilianzishwa mwaka 1936, enzi hizo ikijulikana kwa jina la Queens, yaani Watoto wa Malkia.
Baadaye Simba ilibadilisha jina na kuwa Eagles, yaani ndege aina ya Tai, kabla ya kuanza kutumia jina jingine, Sunderland, ambalo lilidumu hadi mwaka 1971 lilipobadilishwa na kuwa Simba.
Wakati huo Sunderland ilikuwa ina matawi yake, ambayo yalikuwa ni timu za Morning Stars, Canada Dry, Liverpool na Ilala Stuff, ambako huko mchezaji aliyeonekana kukomaa alipelekwa kukipiga Sunderland.
Sababu ya kuachana na jina la Sunderland ni aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume (sasa marehemu), ambaye wakati anaweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la klabu hiyo, lililopo Mtaa wa Msimbazi, mwaka huo 1971, alikemea tabia ya kupenda kuiga mambo ya Waingereza, akiamini kufanya hivyo ni kuendelea kuutukuza ukoloni.
Rais Karume, aliwaambia Simba waachane na majina ya kizungu na watumie jina la asili ya Afrika na ndipo jina la Mnyama tishio zaidi porini, Mfalme wa Nyika, Simba, lilipowavutia hata ukawa mwanzo wa Simba SC.
Simba ikiwa inaitwa Sunderland, iliweza kutwaa ubingwa wa Tanzania mara mbili tu, ikiweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kutwaa taji hilo mwaka 1965 na kuutetea mwaka 1966 na baada ya hapo haikuutia tena mikononi hadi ilipobadilishwa jina na kuwa Simba, ndipo ilipourejesha mwaka 1973.
Simba ilishindwa kutetea taji lake mwaka 1974, baada ya kuporwa na watani wao wa jadi, Yanga mwaka uliofuata, kwa kipigo cha mabao 2-1 katika fainali ya kihistoria iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, mjini Mwanza.
Adamu Sabu (marehemu) aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya Saad Ali, aliifungia Simba bao la kuongoza, kabla ya Sunday Manara kuisawazishia Yanga na Gibson Sembuli (marehemu pia) kufunga la ushindi kwa Watoto wa Jangwani.
Ubingwa wa Tanzania mwaka 1975 kwa mara ya kwanza ulikwenda nje ya Dar es Salaam, ukichukuliwa na Mseto ya Morogoro, iliyokuwa ikinolewa na kocha maarufu, Mohamed Msomali.
Simba iliurejesha ubingwa wake mwaka 1976 na kuutetea kwa miaka minne mfululizo, 1977, 1978, 1979 na 1980. Baada ya hapo, Simba iliyumba na kupoteza makali, kabla ya kuibuka mwaka 1984 na kutwaa taji hilo. Ililipoteza tena na kulazimika kulisubiri hadi mwaka 1990, kabla ya kulipoteza na kulitwaa tena mfululizo mwaka 1994 na 1995. Simba ilitwaa tena taji hilo katika miaka ya 2001, 2003, 2004, 2007 katika Ligi Ndogo, ikiifunga Yanga kwenye fainali na msimu uliopita.
Ukiachana na utawala wa Simba katika soka ya Tanzania, kwenye medani ya kimataifa klabu hiyo ndiyo inayoongoza kwa kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Simba ndiyo klabu pekee iliyoweza kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika, mwaka 1974 ikiitoa timu ngumu ya Ghana katika Robo Fainali, Hearts Of Oak kwa jumla ya mabao 2-0.
Yalikuwa ni mabao ya Sabu na Abdallah 'King' Kibadeni, Wakenya wakimuita Ndululu kutokana na ufupi wake, mjini Accra, yaliyoipa timu hiyo ushindi wa 2-0, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Dar es Salaam.
Hata hivyo, baada ya kushinda 1-0 mjini Dar es Salaam dhidi ya Mehala El Kubra, Simba ilikwenda kufungwa pia 1-0 na Waarabu hao mjini Cairo, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako Wekundu wa Msimbazi waling'olewa.
Nyota wengine wa Simba walikuwa ni kipa Athumani Mambosasa, mabeki Shaaban Baraza, Mohamed Kajole, Athur Mwambeta, Omari Chogo, viungo Khalid Abeid, Willy Mwaijibe, Haidari Abeid, Abbas Dilunga na washambuliaji Adam Sabu na Abdallah Kibadeni.
Nyota hao ndio waliowafunga watani wao wa jadi, Yanga mwaka 1973, baada ya Watoto hao wa Jangwani kutawala soka ya Tanzania kwa miaka mitano mfululizo, wakichukua ubingwa wa nchi tangu mwaka 1968 hadi 1972. Hao pia ndio waliotwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwa mara ya kwanza mwaka 1974 mjini Dar es Salaam.
Simba pia ni klabu pekee ya Tanzania, iliyoweza kucheza fainali ya michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Hiyo ilikuwa ni mwaka 1993, ilipofanikiwa kutinga fainali ya Kombe la CAF, (sasa limeunganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho) na kufungwa na Stella ya mjini Abidjan, Ivory Coast.
Bahati haikuwa yao Wekundu wa Msimbazi, kwani baada ya kulazimisha sare ya bila kufungana ugenini, wengi waliamini kwenye mechi ya marudiano, Stella hawatapona Dar es Salaam, lakini matokeo yake, wenyeji walilala 2-0 kwa mabao ya Boli Zozo.
Klabu hiyo pia ilifanikiwa kuwa ya pili Tanzania kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, baada ya Yanga kuwa ya kwanza mwaka 1998. Lakini Simba ilitinga hatua hiyo kiume zaidi, ikiwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri, kwa mikwaju ya penalti.
Hiyo ilifuatia ushindi wa 1-0 mjini Dar es Salaam, kabla ya kwenda kufungwa 1-0 na yenyewe pia Cairo, lakini mchezo ulipohamia kwenye mikwaju ya penalti, Juma Kaseja, mtaalamu wa kuokoa michomo hiyo, aliibeba Simba baada ya kucheza penalti mbili.
Nyota waliokuwa wakiunda kikosi cha Simba mwaka 2003 ni Juma Kaseja, Amri Said, Said Sued, Boniface Pawasa, Ramadhan Wasso, Victor Costa, Yusuf Macho, Athumani Machuppa, Jumanne 'Shengo' Tondola, Emmanuel Gabriel, Steven Mapunda, Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe, Patrick Betwel, Selemani Matola, Amani Mbarouk, Farouk Ramadhan, Yahaya Akilimali, Primus Kasongo, Abu Amrani, Kevin Mhagama, Majuto Komu, Lubigisa Edward Lubigisa, Christopher Alex, William John, Emmanuel Kingu, Edibilly Lunyamila na Clement Kahabuka.
Aidha, Simba pia ndiyo klabu iliyoweza kutwaa mara nyingi zaidi Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, lijulikanalo kama Kombe la Kagame katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002.
Katika michuano mingine midogo ya Afrika Mashariki, Kombe la Tusker, Simba tena ndiyo timu iliyotwaa mara nyingi zaidi taji hilo, mara nne kati ya michuano saba ya Kombe hilo, katika miaka ya 2001, 2002, 2003 na 2005. Ililikosa mwaka 2006, lilipochukuliwa na Kagera Sugar, mwaka 2007 lilipochukuliwa na Yanga, mwaka 2008 lilipochukuliwa na Mtibwa Sugar na mwaka 2009, lilipiochukuliwa na Yanga tena.
Asili ya Simba SC tangu enzi na enzi ni kucheza soka ya utulivu yenye kuburudisha mashabiki wake, wakitandaza pasi kwa wingi kabla ya kulifikia lango. Imekuwa bahati iliyoje makocha wote wameendelea kuuenzi utamaduni huo hadi kesho.
Japokuwa imepita mikononi mwa makocha wengi tangu kuanzishwa kwake, lakini makocha wa kihistoria na wa kukumbukwa kwenye klabu hiyo ni watano tu, kwanza Paul West Gwivaha (sasa marehemu), pili Nabby Camara, tatu Abdallah Kibadeni, nne Msomali Enteneh Esheteh na wa mwisho ni Mkenya, James Siang'a.
Kwa nini hao ndio makocha wa kihistoria Simba SC?
Wakati Simba inafika Nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974, ilikuwa inanolewa na Gwivaha na wakati inafika fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, ilikuwa chini ya Kibadeni na Esheteh na mwaka 2003 ilipoitoa Zamalek katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa, ilikuwa inanolewa na Siang'a.
Camara, aliyekuwa raia wa Guinea, atakumbukwa kwa kuvumbua vipaji vya nyota waliowika Simba baadaye, kama Abbas Kuka, Filbert Rubibira, Nico Njohole na George 'Best' Kulagwa, kupitia timu ya vijana aliyounda mwaka 1975, baada ya kutua Simba.
Kwa sasa Simba iko chini ya kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia, Patrick Phiri, ambaye ameiwezesha kurejesha makali yake, huku mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, wakiwa wana matumaini ya kula raha zaidi chini ya Mzambia huyo.
Simba SC ipo chini ya Mwenyekiti Ismail Aden Rage, Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji, ambao ni Joseph Kinesi, Suedi Mkwabi, Saidi Pamba, Daniel Manembe, Francis Waya na Ibrahim Masoud. Simba ina watendajiwa wa kuajiriwa, ambao ni Ofisa Utawala, Evodius Mtawala na Ofisa Habari, Clifford Ndimbo- wakati meneja wa timu ni Innocent Njovu na daktari ni Cosmass Kapinga.
Rasilimali kubwa za Simba ni majengo yake mawili pacha yaliyopo Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam. Jengo la kwanza la Simba lilijengwa kwa mchango wa Karume na wanachama wa klabu hiyo wakaongezea fedha na wakashiriki ujenzi, wakibeba, zege, mchanga, kokoto- yaani vifaa vya ujenzi kwa ujumla na hata kufyatua tofali. Jengo la Simba lilijengwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti Dumelezi na Katibu Mkuu Said Mpolaki.
Jengo la pili lilijengwa kwa mpango maalumu wa mkataba na mtu aliyeamua kuwekeza kwenye kiwanja cha wazi cha klabu hiyo. Mwekezaji aliruhusiwa kujenga na kutumia jengo kwa biashara zake hadi mwaka 2012 alikabidhi kwa klabu.
Mpango kamili wa ujenzi wa jengo hilo ulioanzishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Simba, Kassim Mohamed Dewji, ni kuwa na ghorofa nane katika mtindo huo wa makubaliano na watu wenye nia ya kuwekeza kwenye jengo hilo.
Mwekezaji wa sasa angeweza kuendelea na ujenzi wa jengo hilo, kama wanachama wa klabu hiyo wasingefungua kesi mahakamani kupinga zoezi hilo.
Simba SC pia ina mpango wa kujenga Uwanja wake wa kisasa hivi sasa na tayari Rage amekwishakaririwa mara kadhaa akizungumzia ujenzi huo- kwamba mipango inaendelea vizuri ingawa haujaanza.
Pamoja na mafanikio hayo, Simba imepitia vipindi tofauti, vikiwemo vigumu, wakati ilipokutwa na misiba ya viongozi na wachezaji wake. Migogoro pia, imekuwa sehemu ya matatizo ndani ya klabu ya Simba, ingawa kwa upande mwingine hiyo ni demokrasia.
Mbali na majengo yake, Simba inajivunia udhamini wa kampuni ya Bia Tanzania, kupitia bia ya Kilimanjaro.
Kilimanjaro imeleta ukombozi Simba, ambayo ilikuwa inahaha tangu kumpoteza mdhamini wake wa mwisho, Mohamed Enterprises Limited (MeTL), kampuni inayomilikiwa na mpenzi mkubwa wa klabu hiyo, Mohamed Gullam Dewji.
Wafadhili wengine wa Simba, tangu enzi za Sunderland ni mmiliki wa Salama Travel Agency, Saleh Ruwey ambaye aliwanunulia basi la kwanza, Colt Rosa (sasa halipo tena), Ramesh Patel, Fakhrudin Amijee, Ally Mwinyi Tambwe na Abdulrahman Muchacho, ambaye alikuwa akiilisha Simba.
Miaka ya 1990, ndipo walipoibuka wafadhili wengine kama Azim Dewji, ambaye baadaye aliitema timu hiyo kutokana na migogoro, japo amebaki mwanachama na anahudhuria mikutano wakati mwingine.
Mkataba wa awali wa Kilimanjaro uliokuwa na thamani ya Sh bilioni 3, kila mwaka Simba ilikuwa inapata Sh bilioni 1, kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa timu.
Mkataba huo, ulisainiwa Agosti 18, mwaka 2008, katika hoteli ya Movenpick, mjini Dar es Salaam.
Kilimanjaro Premium Lager, ambayo imetoa pia udhamini kama huo kwa Yanga, imekuwa ikiipa Simba Sh milioni 16, kila mwezi kwa ajili ya mishahara ya wachezaji, hiyo ikiwa ni mbali na kupatiwa mabasi mawili madogo. Mabasi hayo, moja aina ya Hiace na jingine Coaster, tayari yamekwisha kukabidhiwa kwa klabu hiyo na yameanza kutumika.
Aidha, Kili pia imeweka utaratibu wa kuipa Simba zawadi, iwapo itafanikiwa kushika moja ya nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikiwa bingwa itapata Sh milioni 25 na ikishika nafasi ya pili, itapewa Sh milioni 15.
Agosti mwaka jana, TBL kupitia bia yake ya Kilimanjalo ilisaini mkataba mpya na Simba katika hoteli ya Double Tree.
Mkataba huo ulioanza rasmi Agosti 1, mwaka jana utaisha Julai 31, mwaka 2016.
Katika mkataba huo, Simba watakuwa wanapewa fedha za mishahara kwa mwezi Sh. Milioni 25 kwa mwezi, watapewa basi jipya la abiria 54, fedha za kuendeshea Mkutano Mkuu wa mwaka, Shilingi Milioni 20 kwa kwa ajili ya tamasha la kila mwaka, Simba Day, vifaa vya mechi na mazoezi vyenye thamani ya Sh. Milioni 35 kila msimu, wakiwa mabingwa watapewa Sh Milioni 25, wakiwa washindi pili Sh. Milioni 15.
Simba, inayojulikana pia kwa majina ya utani kama Wekundu wa Msimbazi, Mnyama na Taifa Kubwa, imekuwa ikipewa vifaa vya thamani na vya kisasa vya michezo, lengo likiwa ni kuifanya iwe bora na mfano wa kuigwa katika ligi hiyo.
Lakini Simba ina kundi la wapenzi wa klabu hiyo, waliounda umoja wao chini ya Kassim Dewji, uitwao Friends Of Simba, ambalo linasaidia mno klabu hiyo. Kundi hilo lililoibuka mwaka 2001, likiwa na watu kama Crescentius Magori, Evans Aveva, Mulamu Nghambi, Mohamed Nassor, Musley Ruwey, Harrison Mutembey, Jerry Yambi na wengine, limekuwa likisaidia huduma za timu, usajili na kadhalika.
Bado kuna watu wengine mashuhuri nchini, wakiwemo wafanyabiashara na viongozi wa serikali, ambao kwa mapenzi yao wamekuwa wakiisaidia mno Simba.
Timu hii yenye mashabiki hadi nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, ina sura ya kitaifa na ina matawi hadi mikoani, bara na visiwani.
Ingawa tathmini inaonyesha Yanga ndiyo yenye mashabiki wengi zaidi ya Simba, lakini siku za karibuni ni kama mambo yanaanza kubadilika, kwani kwa vigezo vile vile vilivyotumika kubaini kuwa Yanga ndiyo yenye mashabiki wengi, Simba nayo inaonekana kuongeza idadi ya mashabiki wake.
Kigezo kikubwa kinachotumika ni idadi ya mapato yatokanayo na viingilio vya milangoni, Simba nayo siku hizi inavutia watu wengi na kutengeneza mapato makubwa, wakati mwingine kuliko Yanga.
Yote kwa yote, linapokuja swali nani zaidi baina ya watani wa jadi, ukiachilia mbali mechi baina ya wababe hao, Simba inaweza kujinasibu ndiyo mbabe, kutokana na rekodi nzuri katika medani ya kimataifa.
Naam, hao ndio Simba SC, Wekundu wa Msimbazi, wapeperusha vyema bendera ya nchi kwenye michuano ya kimataifa.

REKODI ZA SIMBA:
UBINGWA WA LIGI KUU:
1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004 na 2007 (Ligi Ndogo), 2010 na 2012.
LILILOKUWA KOMBE LA NYERERE:
1984, 1995 na 2000
LILILOKUWA KOMBE LA MUUNGANO:
1993, 1994, 1995, 2001, na 2002
KOMBE LA TUSKER:
2001, 2002, 2003 na 2005
KOMBE LA CAF:
Ilifika fainali mwaka 1993
KOMBE LA KAGAME:
1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002
LIGI YA MABINGWA AFRIKA:
Kucheza hatua ya makundi 2003
KLABU BINGWA AFRIKA:
Kucheza Nusu Fainali 1974

MABINGWA WA JUMLA LIGI KUU:
1965 : Sunderland (Dar es Salaam)
1966 : Sunderland (Dar es Salaam)
1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam)
1968 : Yanga
1969 : Yanga
1970 : Yanga
1971 : Yanga
1972 : Simba
1973 : Simba
1974 : Yanga
1975 : Mseto SC (Morogoro)
1976 : Simba
1977 : Simba
1978 : Simba
1979 : Simba
1980 : Simba
1981 : Yanga
1982 : Pan African
1983 : Yanga
1984 : Simba
1985 : Yanga
1986 : Tukuyu Stars (Mbeya)
1987 : Yanga
1988 : Coastal Union (Dar es Salaam)
1989 : Yanga
1990 : Simba
1991 : Yanga
1992 : Yanga
1993 : Yanga
1994 : Simba
1995 : Simba
1996 : Yanga
1997 : Yanga
1998 : Yanga
1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2001 : Simba
2002 : Yanga
2003 : Simba
2004 : Simba
2005 : Yanga
2006 : Yanga
2007 : Simba (Ligi Ndogo)
2008 : Yanga
2009: Yanga
2010: Simba SC
2011: Yanga SC
2012: Simba SC

SIMBA SC BINGWA 2012


Mashabiki wa Simba SC kwa raha zao leo
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC jioni hii wamejihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuifunga Moro United ya Morogoro maba 3-0 na mechi ya wapinzani wao katika mbio za ubingwa, Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar ikivunjika timu hizo zikiwa zimefungana 1-1, Uwanja wa Azam, Chamazi.
Mabao ya Simba SC yalifungwa na Patrick Mutesa Mafisango, Haruna Moshi Shaaban 'Boban' na Felix Mumba Sunzu Jr.
Simba sasa imetimiza pointi 59, ambazo kutokana na matokeo ya leo ya sare ya 1-1 kati ya azam na Mtibwa, haziwezi kufikiwa na timu yoyote. Lakini kujiweka salama, Simba itahitaji japo polnti moja katika mechi zake tatu zilizobaki.
Mchezo kati ya Azam na Mtibwa ulivunjika wakati beki Salum Swedi amekwishaifungia bao Mtibwa na Mrisho Khalfan Ngassa ameifungia Azam FC. Mtibwa waligomea mechi hiyo wakipinga Azam kupewa penalti. Sasa Kamati ya Ligi Kuu itakutana kesho na kutoa uamuzi, lakini kuna uwezekano mkubwa Mtibwa ikatozwa faini na wapinzani wao kupewa ushindi.






Msimamo Ligi Kuu ya Vodacom

tan
TAN
Nafasi Timu MP W D L GF GA +/- Pts
1  Simba SC 25 18 5 2 42 12 30 59
2  Azam 23 15 5 3 34 11 23 50
3  Young Africans 24 15 4 5 38 21 17 49
4  Mtibwa Sugar 23 10 5 8 31 25 6 35
5  Coastal Union 24 10 2 12 24 29 -5 32
6  Kagera Sugar 24 7 10 7 25 25 0 31
7  JKT Ruvu 24 7 10 7 25 30 -5 31
8  Ruvu Shooting 24 7 9 8 20 19 1 30
9  JKT Oljoro 23 7 8 8 16 20 -4 29
10  Toto African 24 5 11 8 23 27 -4 26
11  African Lyon 24 5 8 11 20 29 -9 23
12  Villa Squad 24 6 5 13 26 43 -17 23
13  Moro United 25 3 10 12 27 44 -17 19
14  Polisi Dodoma 25 3 8 14 18 34 -16 17

No comments: