Saturday, August 13, 2016

Mtwara Girls waibuka washindi Young Scientists Kitaifa





Washindi wa maonyesho ya Wanasayansi na wanateknolojia wachanga (Young Scientists & Technology), Diana Sosoka (kushoto) na Nadhra Mresa kutoka shule ya sekondari ya Wasichana Mtwara wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego pamoja na wakuu wa wilaya za Mtwara.

Washindi wa maonyesho ya Young Scientists & Technology kutoka Mtwara Girls, Diana Sosoka (kulia) na Nadhra Mresa wakiondoka eneo la uwanja wa ndege Mtwara kuelekea shuleni kwao.





Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Dkt. Khatibu Kazungu, akiongea wakati wa hafla ya kuwapokea wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Mtwara walioshinda maonyesho ya Young Scientists & Technology Kitaifa, Diana Sosoka na Nadhra Mresa.


Wanafunzi wa Mtwara Girls wakifurahia ushindi wa wenzao



Na Juma Mohamed, Mtwara

Kwa mara nyingine, mkoa Mtwara umeendelea kufanya vizuri katika elimu baada ya shule ya sekondari ya wasichana Mtwara kufanikiwa kuwa washindi wa kwanza Kitaifa katika maonyesho ya wanasayansi na wanateknolojia wachanga (Young Scientists & Technology) yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, na kutunukiwa zawadi mbalimbali.
Wanafunzi Diana Sosoka na Nadhra Mresa wa kidato cha sita, waliopata ushindi huo ambao ulihusisha shule 150 wamesema kupitia mashine ambayo wameibuni ya kutotolesha vifaranga vya kuku na kupelekea ushindi huo, inaweza kuwakomboa wanawake kuondokana na umasikini.

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Wasichana Mtwara, wakiwa nje ya uwanja wa ndege wa Mtwara kuwasubiri wenzao washindi wa maonyesho ya Young Scientists & Technology.



“Hatujapata ‘sapoti’ kubwa sana ya kuweza kutengeneza ‘incubator’ ambayo ni mzuri, matarajio yetu tungeomba ushirikiano na ‘sapoti’ maana ni biashara hii tunaifanya na pia tunataka kutoa elimu kwa wanawake..sio wanawake tu, na wanaume pia, kwahiyo elimu itolewe kwa Watanzania wote ili kuondoa huu umasikini..” alisema Diana.
Mwalimu wa sayansi alioambatana nao katika maonyesho hayo Rashidi Ally alieleza siri ya ushindi huo, ambao ulipelekea kupewa zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha sh. Milioni 1.7, kusomeshwa bure katika chuo kikuu nje ya nchi baada ya kumaliza mtihani wa kidato cha sita na kupelekwa nchini Thailand.
Afisa elimu wa mkoa wa Mtwara Fatuma Kilimia, aliwahusia wanafunzi hao kutokubali kudanganywa na wanaume na kuharibu malengo yao, na kuwataka kujifunza kusema hapana.

Washindi wa maonyesho ya Young Scientists & Technology Kitaifa, Diana Sosoka (kulia) na Nadhra Mresa.



Mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego, aliahidi kuwaunganisha na shirika la Kuhudumia viwanda vidogogo SIDO pamoja na chuo cha VETA Mtwara kwa ajili ya kuendeleza ujuzi wao, pamoja na kuchapisha majina yao katika mashine nyingine za kutotolesha kuku zitakazotengezwa.
“Hiki walichofanya watoto wetu mimi niahidi tutawaunganisha wapo wenzetu wa SIDO wapo wenzetu wa VETA, ili sasa kuuhisha kile walichofanya na waone katika macho yao kuna wanawake wamewakomboa kwa kutumia akili zao..kwahiyo sisi tutafanya hayo ili hilo walilotengeneza liwe kwa wingi na ubora Zaidi ili waweze kusonga mbele..na kwakweli nitawaomba SIDO na VETA waweke nembo kwa kutumia majina zile mashine zipewe majina kwa kumbukumbu thabiti ya kuukomboa mkoa wa Mtwara.” Alisema Dendego
Ushindi huo kwa Mtwara unakuwa ni mafanikio mengine baada ya hivi karibuni kuingia katika mikoa kumi bora iliyofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kutokana na matokeo ya shule ya sekondari ya Tandahimba




No comments: