Wednesday, August 10, 2016

Waendesha Bodaboda Tandahimba waliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wasiovaa Helmet na Viatu.


Waendesha Pikipiki waliopata mafunzo ya usalama barabarani katika Tarafa ya Mahuta wilayani Tandahimba, wakiwa katika hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo.



Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki wa Tarafa ya Mahuta, wilayani Tandahimba akiwaimbisha wanafunzi wake.

Juma Mohamed, Tandahimba.

Waendesha Pikipiki za kubeba abiria maarufu Bodaboda wilayani Tandahimba mkoani Mtwara, wameliomba jeshi la Polisi wilayani humo kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaoendesha vyombo hivyo bila kuvaa kofia ngumu (Helmet) ili kuokoa maisha ya Watanzania wanaokufa kwa uzembe.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mafunzo ya siku saba ya usalama barabarani kwa waendesha pikipiki hao katika Tarafa ya Mahuta wilayani humo, katibu wa mafunzo hayo Latifu Komba, alisema wengine wanafikia hatua ya kuendesha wakiwa wamevaa kandambili hali ambayo inashusha hadhi ya kazi hiyo.
“Na kwakua tulishakaa vikao mbalimbali na kukubaliana kwamba madereva Bodaboda wote wafuate sheria za usalama barabarani, tunaomba kwanzia leo dereva bodaboda yeyote ambaye hana kofia ngumu yani Helmet au aliovaa ndala wakati akiendesha pikipiki na akabeba abiria na hasievaa kofia wote kwa pamoja wachukuliwe hatua tena hatua kali za kisheria ili kulinda hadhi ya kazi yetu na kuokoa maisha ya Watanzania wanaokufa kwa uzembe unaoweza kuhepukika..” alisema Komba.

Picha ya pamoja, mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba katikati, kushoto ni mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmad na kulia ni mkurugenzi wa APEC Respicius Timanywa wakiwa katika picha ya pamoja.



Naye, kamnada wa polisi wilaya ya Tandahimba, Mrakibu wa Polisi, Fraterine Tesha, alisema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza ugomvi uliokuwapo baina ya waendesha pikipiki hao na jeshi la polisi na kwamba kwakua wamekiri wenyewe kutii sheria za usalama barabarani, watakiuka kwa makusudi watachukuliwa hatua.
Mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba, amewasisitiza waendesha pikipiki hao kwenda kuitumia vizuri elimu waliyoipata ili kuhepuka kupata ajali zisizo za lazima na kuhatarisha maisha yao.

Mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba, akiwahutubia waendesha pikipiki wa Tarafa ya Mahuta, wilayani Tandahimba waliohitimu mafunzo ya usalama Barabarani.



“Vilema ni wengi, sikuhizi jamani hakuna ‘spare’ ya kichwa..kwahiyo nduguzangu elimu hii muitumie vizuri kuhepuka kupata ajai, vaa ‘helmet’ mwingine anaona akivaa ‘helmet’ sura yake itakuwa imefichwa hataonekana, hapana sura yako itabaki ileile ila ukitembea na helmet ni kinga tosha..” alisema.
Mbunge wa Tandahimba, Katani Ahmad, aliwataka waliohitimu mafunzo hayo kwenda kuwahamasisha wengine ambao walikataa kwa makusudi kuudhuria mafunzo hayo ili awamu nyingine waweze kujifunza sheria hizo na kudai kuwa wanampa wakati mgumu kuwatetea pindi wanapokamatwa kwa makosa ya kizembe.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa shirika la Kupunguza Umasikini na Kutunza Mazingira (APEC) linalotoa mafunzo hayo, Respicius Timanywa alieleza matarajio ya shirika hilo baada ya mafunzo hayo.
“Tunatarajia wahitimu hawa wakimaliza mafunzo haya hatutamwona dereva wa pikipiki akiendesha bila ‘helmet’..tunatarajia baada ya kumaliza mafunzo haya hatutaona ‘site’ mirror zinang’olewa kwenye pikipiki na kuachwa nyumbani..” alisema.
Katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika vituo vinne tofauti wilayani humo, jumla ya vijana 76 wamehitimu na wanatarajia kupatiwa leseni za udereva.

Picha ya pamoja, mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Sebastian Waryuba, viongozi mbalimbali na waendesha pikipiki wa Mahuta.



No comments: