Thursday, May 24, 2012

BREAKING NEWS: NCHUNGA AJIUZULU YANGA BAADA YA KUVAMIWA USIKU WA MANANE NYUMBANI KWAKE



Nchunga akitangaza kujiuzulu leo jioni hii ofisini kwake
MWENYEKITI wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ametangaza kujiuzulu wadhifa wake jioni hii ofisini kwake, jengo la NSSF, barabara ya Bibi Biti, Dar es Salaam, siku moja baada ya kuvamiwa na kundi la watu nyumbani kwake, Mbezi, Jijini usiku wa wa manane.
Hata hivyo, Nchunga amekataa kulihusisha tukio la kuvamiwa kwake usiku wa jana na kujiuzulu kwake, akisema kwamba amefikia uamuzi huo kuinusuru Yanga, kwa sababu wapo watu wako tayari Yanga ife, lakini wamng'oe yeye madarakani, kitu ambacho yeye hapendi kitokee.
Nchunga alisema kwamba majira ya saa nane usiku wa jana, alivamiwa na kundi la watu takribani 15, lakini hawakufanikiwa kufanya chochote kutokana na ulinzi mkali uliopo katika nnyumba hiyo.
"Kwanza mbwa walianza kubweka, walinzi wakashituka wakaomba msaada kwa walinzi wenzao, nasi tukapuga simu polisi, wakaja haraka sana na kukuta watu hao wamekwishakimbia,"alisema


TAARIFA YA KUJIUZULU KWA NCHUNGA:



LLOYD NCHUNGA BIHARAGU
C/O LLOYD ADVOCATES,
Morogoro/Bibi TIti Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers
P.BOX 75111, Dar-Es- Salaam,Tanzania.



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI YA UENYEKITI WA KLAB YA YANGA.
Ndugu wana Habari, najua kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika nayo.
Tangu tumeingia madarakani tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja kwa watani wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei 2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika klab yetu.
Hali kadhalika tumeshirikiana mpaka tumeweza kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia mkataba na kampuni ya NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa wa mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati miliki za maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za mwisho za kumalizia michoro.
Hali kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na kukusanya data za wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi 300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu. Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
Kwa ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano kwa kiongozi ajaye.
Aidha, tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa, na kongamano la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.
Haya yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo mtaona yalikuwa mazuri.
Lakini pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja. Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali, tulitumia kila jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.
Ninachokiona mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia. SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema.
Sioni mantiki katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!
Kwa wanaoijua Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado wachezaji walicheza kwa morali.
Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia.
Baada ya mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao , Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo cha Redio moja maarufu hapa nchini wakidai kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea kuongoza!
Hii imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu.
Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu.
Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi.
Natumaini kamati ya utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa mafanikio zaidi.
Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.
Wasalaam,


LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.

Nakala kwa:-
Mama Fatma Karume,Mdhamini
Francis Kifukwe, Mdhamini
Bwana Yusuf Manji – Kwa taarifa


 

MALAWI WATUA TAYARI KUIKABILI STARS TAIFA


Stars mazoezini

TIMU ya taifa ya Malawi, The Flames inatarajiwa kuwasili nchini leo saa 10 jioni kwa ndege ya Air Malawi kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Taifa Stars itakayofanyika Jumamosi (Mei 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi hiyo ni kwa ajili ya kuipima nguvu Taifa Stars kabla ya mechi yake mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast itakayofanyika Juni 2 mwaka huu jijini Abidjan. Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari iko kambini chini ya Kocha Kim Poulsen.
Malawi itafikia hoteli ya Sapphire iliyoko Mtaa wa Lindi na Sikukuu ambapo Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 VIP B na C wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
Malawi ambayo itafikia hoteli ya Sapphire iliyoko Mtaa wa Lindi na Sikukuu baada ya mechi hiyo itakwenda Zanzibar ambapo Mei 28 mwaka huu itacheza na Zanzibar Heroes.
Makocha wa timu zote mbili Taifa Stars na The Flames kesho (Mei 25 mwaka huu) saa 5 asubuhi watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF.

MAKALLA AWAKABIDHI BENDERA TWIGA STARS, WAPAA ADDIS


Twiga Stars

TIMU ya taifa ya soka ya miguu kwa wanawake Tanzania, Twiga Stars inayotarajia kuondoka leo saa 11.05 jioni kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwenda Ethiopia imekabidhiwa Bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makalla.
Twiga Stars yenye msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi itacheza na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya mchujo kwa ajili ya Fainali za Nane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu Equatorial Guinea.
Mechi hiyo itafanyika Mei 27 mwaka huu kwenye Uwanja wa Addis Ababa wakati ile ya marudiano itachezwa Juni 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imepeta tiketi ya kwenda Equatorial Guinea.
Wachezaji walioondoka na kikosi hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri, Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis.
Kwa upande wa Benchi la Ufundi ni Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha Msaidizi), Furaha Francis (Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa) na Christina Luambano (Daktari wa Timu).
Twiga Stars ambayo msafara wake unaongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu saa 6 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines.
Wakati huo huo: Ligi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa sasa itaanza Mei 27 mwaka huu badala ya Mei 26 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali. Uamuzi wa kusogeza mbele kwa siku kuanza kwa ligi hiyo uliofanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 23 mwaka huu).
Timu 23 zitachuana katika kinyang’anyiro hicho kitakachofanyika katika vituo vya Kigoma (Uwanja wa Lake Tanganyika), Musoma (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume) na Mtwara (Uwanja wa Umoja) ambapo kinatarajia kumalizika Juni 13 mwaka huu.
Kituo cha Kigoma kina timu za Aston Villa ya Singida, Bandari (Kagera), CDA (Dodoma), JKT Kanembwa (Kigoma), Majimaji (Tabora), Mwadui (Shinyanga) na Pamba (Mwanza).
Ashanti United ya Ilala, Flamingo (Arusha), Forest (Kilimanjaro), Korogwe United (Tanga), Nangwa VTC (Manyara), Polisi (Mara), Red Coast (Kinondoni) na Tessema ya Temeke ziko kituo cha Musoma.
Kituo cha Mtwara kina timu za Kurugenzi ya Iringa, Lindi SC (Lindi), Mighty Elephant (Ruvuma), Mkamba Rangers (Morogoro), Mpanda Stars (Rukwa), Ndanda (Mtwara), Super Star (Pwani) na Tenende (Mbeya).

HISTORIA YA EURO A-Z MJUE NA MWASISI WAKE


Mabingwa watetezi Hispania

MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2012 inayoandaliwa kwa pamoja na Poland na Ukraine itakuwa ni fainali za 14 za michuano hiyo kufanyika.
Lilikuwa ni wazo la Henri Delaunay, Katibu wa Shirikisho la Soka Ufaransa, ambaye aliibuka na wazo hilo kwa mara ya kwanza kwenye bara hilo, mwaka 1927.
Kwa mara ya kwanza alipata sapoti kidogo sana na michuano hiyo haikuanza hadi mwaka 1960. Hadi mwaka 1980 ni timu nne tu zilikuwa zinacheza hatua ya fainali, lakini sasa ni timu 16 na imekuwa moja ya michuano mikubwa katika kalenda ya soka.
Michuano yote 13 iliyotangulia imeacha kumbukumbu kibao – BIN ZUBEIRY inakuletea wasifu wa michuano hiyo hadi kufikia fainali za mwaka huu.
Mfungaji wa bao la ubingwa fainali zilizopita za Euro,Torres amerejeshwa kikosini dakika za mwishoni, je atang'ara tena?

1960
MICHUANO ya kwanza ilifanyika Ufaransa na bingwa alikuwa Soviet Union. Mabingwa hao waliongozwa na kipa wao gwiji, Lev Yashin langoni kwenye michuano hiyo. Kipa aliyeipa England taji la Kombe la Dunia, Gordan Banks alifunikwa na kipa huyo.

1964
Hispania kwa sasa wanatawala katika ulimwengu wa soka, lakini mafanikio yao ya kwanza yalikuja katika Euro ya 1964, wakati walipotwaa taji hilo kwenye ardhi ya nyumbani katika timu iliyoongozwa na Luis Suarez. Kiungo huyo aling’ara kwenye michuano hiyo, ambayo Hispania ilifunika mbaya.

1968
Michuano ya tatu ya Ulaya ilifanyika Italia na kama ilivyokuwa Hispania 1964, pia michuano hii ubingwa ulichukuliwa na wenyeji. England ilifika Nusu Fainali na ilifungwa na Yugoslavia katika mechi ya kusisimua, iliyokuwa na upinzani mkali. Alan Mullery wa England alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi hiyo.

1972
Waliokuwa mabingwa watetezi wa Ulaya, Italia walishindwa kufuzu kuingia kwenye fainali hizo, wakiangushwa na Ubelgiji waliokuwa wenyeji, katika Robo Fainali. Pamoja na hayo, Ujerumani waliweza, waliwafunga wenyeji hao na kufuzu kutinga fainali za michuano hiyo, ambako waliifunga iliyokuwa USSR mabao 3-0 na kutwaa Kombe.

1976
Michuano ‘iliyong’ara’ ya Euro 1976 taji lilichukuliwa na Czechoslovakia walioifunga Ujerumani Magharibi kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti mjini Belgrade. Lakini pia ilikuwa michuano ambayo Wales ilikaribia kufuzu.

1980
Mfumo wa michuano ulibadilika mwaka 1980, kwa timu nane kuingia kwenye fainali, lakini mwonekano wa matokeo haukubadilika, kwa Ujerumani kutwaa ubingwa. Pamoja na hayo, kulikuwa kuna ‘maajabu’ kadhaa ikiwemo Ubelgiji iliyokuwa na vipaji babu kubwa kufika fainali, mmojawao akiwa ni Jean-Marie Pfaff.

1984
Ufaransa walikaribia kutwaa taji la Kombe la Dunia mwaka 1982, kabla ya kupokonywa tonge mdomoni na Ujerumani Magharibi katika Nusu Fainali ya kukumbukwa, lakini hakukuwa na maajabu katika ardhi ya nyumbani, wakati Wafaransa walipoongozwa na gwiji wake Michel Platini kutwaa taji hilo.

1988
Ilikuwa ni michuano ambayo mshambuliaji wa Uholanzi, Marco van Basten alikuwa hana wa kumfananisha naye, kutokana na kufunga mabao ambayo yaliiwezesha nchi yake kutwaa Kombe. Pamoja na hayo, ilikuwa habari tofauti kwa USSR, iliyoongozwa na kocha wake gwiji, Valery Lobanovsky walipokaribia kutwaa taji.

1992
Denmark haikufuzu kwenye fainali hizo nchini Sweden, lakini walipata nafasi kutokana na Yugoslavia kuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, hivyo kushindwa kushiriki. Na vijana hao wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, wakiifunga Ujerumani kwenye fainali. Kim Vilfort, ambaye alifunga kwenye fainali alielezea namna ambavyo Denmark walikuwa na maandalizi mazuri kabla ya fainali hizo.

1996
Euro 96 – michuano ambayo ilipewa jina soka imerejea nyumbani. England ilifika Nusu Fainali, lakini ikafungwa na Ujerumani kwa mikwaju ya penalti. Ujerumani ilifanikiwa kutwaa taji hilo kwa kuifunga Czechs Uwanja wa Wembley. Mshambuliaji wa England, Alan Shearer alifanya vitu adimu sana kwenye fainali hizo.

2000
England ilifanikiwa kuifunga Ujerumani, lakini hawakufanikiwa kufuzu kutoka kwenye kundi lao na vijana wa Kevin Keegan walirejeshwa nyumbani kimaajabu. Ufaransa walitwaa Kombe la Dunia nyumbani kwao mwaka 1998 na wakadhihirisha ubabe wao kwa kutwaa taji la Ulaya pia kwenye fainali zilizoandaliwa kwa pamoja na Ubelgiji na Uholanzi. Kiungo Emmanuel Petit aliyeng’ara kwenye michuano hizo alielezea siri ya mafanikio ya nchi yao.

2004
Euro 2004: Ugiriki walipoibuka mabingwa. Ilikuwa unakwenda kuwa mwaka wa Ureno, katika fainali ambazo walikuwa wenyeji, lakini wakafungwa na Ugiriki 1-0 kwenye fainali. Cristiano Ronaldo aliumizwa sana na matokeo hayo, kwani ulikuwa mwaka wa kufurahia mafanikio na timu yake ya taifa, lakini ikashindikana.

2008
Katika michuano iliyoandaliwa kwa pamoja na Uswisi na Austria, ambayo ilifana, Hispania waliibuka mabingwa baada ya miaka 44 ya kusubiri taji la kimataifa. Hispania waliifunga 1-0 Ujerumani katika fainali, bao pekee la Fernando Torres dakika ya 33 na sasa wanaingia kwenye fainali za mwaka huu kutetea taji, wakiwa pia mabingwa wa dunia. Je, wataweza? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.

MENEJA KILIMANJAREO ABAINI SIMBA NA YANGA ZA TANO DUNIANI, MUZIKI WETU UNAUZA ZAIDI NJE


Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Geroge Kavishe akizungumza na Waandishi wa Habari leo wakati akitambulisha kampeni ya 100% tz Flava leo katika hoteli ya New Africa.
UCHUNGUZI uliofanywa na Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe umemuonyeaha mambo mawili makubwa kuhusu Tanzania- kwanza ni muziki wa nchini kuwa bidhaa inayonunuliwa zaidi nje na pili Simba na Yanga kuwa kwenye tano ya wapinzani wa jadi jadi dunaini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya 100% TZ Flava, iliyofanyika kwenye hoteli ya New Africa mchana huu mjini Dar es Salaam, Kavishe alisema kwamba mbali na Simba na Yanga kuwa kwenye tano bora ya wapinzani wa jadi duniani, pia zinashika nafasi ya pili Afrika.
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Executive Solutions, waratibu wa kampeni ya 100% tz Flava akizungumza na Waandishi wa Habari katika hoteli ya New Afrika leo
Akiizungumzia kampeni hiyo, Kavishe alisema kwamba itatembea kwa miezi sita na itapambwa na mambo mengi mazuri ya kujivunia kuhusu Tanzania.
Alisema kampeni hiyo itakuwa na sehemu tatu, ambayo ni kwanza kuzindua alama ya kampeni hiyo, 100% tz Flava- tusherehekee kilicho chetu.
“Kwenye hii kampeni, imetengenezwa ili kumpa mteja raha, lakini lazima iache ujumbe, ambao ni furahia kilicho chetu. Kampeni inahusu muziki wetu, tumetumia picha za wanamuziki wetu,”alisema Kavishe na kuongeza;
“Kwanza nataka niwaambie kama mlikuwa hamjui, bidhaa ambayo inauzika nje zaidi kwa sasa hapa Tanzania, ni muziki wetu, watu wa nje ya nchi wananunua sana muziki wetu na ndio bidhaa inayoongoza kuuzika nje ya nchi,”alisema.
Alisema pia wametumia picha za Simba na Yanga, klabu ambazo zinadhaminiwa na bia hiyo. “Hakuna nchi duniani, klabu zake za ndani zina ukubwa na uzito ambao Simba na Yanga zinao. Mvuto wa Simba na Yanga duniani ni wa tano kwa ukubwa. Na kwa Afrika wa pili,”alisema Kavishe.
Aidha, Kavishe pia alisema katika kampeni hizo, pia wametumia lugha za mtaani, ambazo pia ni fahari ya Tanzania kwa mfano piga tarumbeta, neno linalowakilisha kunywa bia kwa kutumia chupa moja kwa moja na kula bata, yaani kula raha.
Mapema, Kavishe alisema kampeni hii ni mwendelezo wa kampeni ya Kili Jivunie Utanzania, ambayo amesema kwa kiasi kikubwa imefanikiwa.
“Bia ya Kilimanjaro Lager ipo tangu mwaka 1954. Ilipotea wakati wa harakati za uhuru na ikarudi mwaka 1966 kama Kilimanjaro Premium Lager na hadi leo tunasukumana nayo, tunabadilisha nembo na kadhalika, lakini bado tupo nayo,”alisema.
Kavishe alisema bia kama maisha ya mwanadamu, inazaliwa, inakuwa, inakomaa na inakufa- lakini kudumu kwa bidhaa sokoni kunatokana na kampeni inayofanywa kuibakiza sokoni.
Alisema uchunguzi walioufanya mwaka 2009 ili kutambua kwa nini bia ya Kilimanjaro ipo sokoni na wateja wanaionaje, uliwaonyesha kwamba bia hiyo inakubalika mno mbele ya Watanzania.
Waandishi wakisikiliza kwa makini
“Sisi tulikuwa tunajua ni Safari Lager, tukataka kujua bia ipi inakubalika zaidi kama ya Kitanzania, majibu yaliyokuja hatukukubaliana nayo. Hatukuamini, walisema ni Kilimanjaro Premium Lager,” alisema.
Kavishe alisema Safari Lager iko sokoni tangu mwaka 1977 na ilikuwa inachukuliwa kama ni bia ambayo asili yake ni Tanzania kutokana na alama ya kanyumba ka msonge, lakini wateja wao wakasema ni Kilimanjaro kwa sababu ya alama ya mlima Kilimanjaro, mnyama Twiga na kufanya vitu ambavyo vinawagusa Watanzania moja kwa moja

No comments: