Bin Kleb |
MJUMBE wa
Kamati ya Utendaji ya klabu ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb, amerejea Dar es
Salaam na kusema kwamba Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage
anastahili tuzo ya kutunga uongo kwa kitendo chake cha kuwadanganya wanachama wa
Simba eti kuna mtoto wa kigogo aliingilia usajili wa Mbuyu Twite.
“Rage
anastahili tuzo ya muongo, ile vita ilikuwa kati yangu mimi na yeye, nadhani
yeye alikuja Kigali kupiga picha na yule mchezaji, baada ya kushindwa kufanya
hivyo alipokuwa Dar es Salaam, maana yake alikuja haraka haraka akazungumza na
kiongozi mmoja wa FERWAFA (Shirikisho la Soka Rwanda), akapiga picha na Twite
akaondoka.
Karudi Dar
es Salaam kwenye Mkutano Mkuu anasema amemsajili Twite, baada ya mimi kuonyesha
vielelezo vya kumsajili huyo mchezaji kama mikataba na picha akiwa anasaini na
kukabidhiwa jezi, akaanza kusema kuna mtoto wa kigogo, huyo mzee vipi? Mbona
anakuwa muongo namna hii.
Yeye aseme
kweli tu, hana uzoefu na mambo haya, yeye ni mtu wa kuropoka tu, hawezi
kazi,”alisema Bin Kleb.
Rage,
alilalamika hadi kutoa machozi mjini Dodoma, wakati akizungumzia sakata la Mbuyu
Twite akidai kuna mtoto wa kigogo aliingilia kati na ndio maana mchezaji huyo
akabadilisha uamuzi wake na kwenda Yanga.
Rage alidai
kumsaini kwanza Twite, huku akinywa kahawa mjini Kigali na akadai wakati
anamsaini na kumpa dola za Kimarekani 30,000 Yanga wakapiga simu na mchezaji
huyo akawajibu amekwishamalizana na watu wa Simba.
Lakini
baadaye Twite akaibuka akisaini Yanga na kurudisha fedha za Wekundu hao
wa Msimbazi.
MTAKATIFU TOM AELEZA MIKAKATI YAKE KABLA YA LIGI KUU
Mtakatifu Tom kazini Yanga |
KOCHA wa
klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Mbelgiji Tom Saintfiet amesema kwamba anataka
mechi mbili kabla ya kutoka nje ya nchi kwenda kuweka kambi fupi ya kujiandaa na
msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza
na BIN ZUBEIRY jana, Mtakatifu alisema kwamba mechi ni dhidi ya timu hapa ya
nyumbani na nyingine dhidi ya timu ya nje na baada ya hapo atakuwa tayari kwa
safari ya nje nchi.
Kuhusu hilo,
Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa alisema jana kwamba maandalizi ya mechi
hizo yanaendelea vizuri na wanaweza kucheza na African Lyon ya Dar es Salaam na
AFC Leopard ya Kenya.
Habari za
ndani zinasema kwamba Yanga itakwenda Rwanda kuweka kambi fupi ya kujiandaa na
msimu na huko itacheza na mechi za kirafiki na vigogo wa huko kama APR, Rayon,
Rayon na Polisi.
Akiwa
anaingia mwezi wa pili tangu aanze kazi Yanga, tayari Tom amekwishaweka Kombe
moja kwenye kabati la mataji la Yanga, ambalo ni la Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Yanga
ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani
na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa
ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali
kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa
mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga
bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga
ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika
fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa
marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua
tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao
2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na
Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua
tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3,
kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa
Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika
Peter akicheza penalti mbili za Waganda.
Aidha, kwa
kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya
kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975
kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya
Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania,
mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam
Timbe.
MATOLA ASEMA MTIBWA SUGAR WATAANGUKIA PUA KAMA AZAM
Suleiman Matola |
KOCHA wa
timu ya vijana ya Simba SC, Suleiman Abdallah Matola amesema kwamba hawahofii
kabisa Mtibwa Sugar kuelekea fainali ya michuano ya Bank ABC Sup8R na anaamini
atabeba Kombe mbele yao keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Akizungumza
na BIN ZUBEIRY jana baada ya mechi Uwanja wa Taifa, Matola ambaye
ni Nahodha wa zamani wa Simba SC, alisema kwamba Mtibwa ni timu nzuri aliiona
vizuri wakati ikiifunga 5-1 Jamhuri ya Pemba, lakini bado kwa Simba B
wataangukia pua.
“Itakuwa
mechi ngumu hilo naamini kabisa, lakini nataka nikuambie, kama nilivyosema kabla
ya kucheza na Azam, nasema tena kabla ya kucheza na Mtibwa Sugar, tutawafunga
bila kuongezewa nguvu ya wachezaji wa timu A,”alisema
Matola.
Simba jana
ilitinga Fainali ya michuano ya BankABC Sup8R baada ya kuifunga Azam FC, mabao
2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Jumamosi itamenyana na Mtibwa
Sugar, ambayo katika mechi ya kwanza imeifunga Jamhuri ya Pemba mabao 5-1,
uwanja huo huo.
Katika
mchezo huo, hadi mapumziko, Simba B walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa
kimiani na Rashid Ismail aliyeunganisha krosi ya Edward Christopher dakika ya
pili tu ya mchezo huo.
Kipindi cha
pili ‘Watoto wa Matola’ walirudi na moto na kulisakama kama nyuki lango la Azam,
wakigongeana pasi za uhakika ndefu na fupi na kuwafunika kabisa mabingwa wa
Kombe la Mapinduzi.
Christopher
Edward aliifungia Simba bao la pili kwa penalti dakika ya 56, baada ya yeye
mwenyewe kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Luckson
Kakolaki.
Azam
walipata bao la kufutia machozi dakika ya 71, mfungaji Zahor Pazi aliyeingia
kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Gaudence Mwaikimba, baada ya kutokea
purukushani kwenye lango la Simba B.
Christopher
Edward amezidi kujiimarisha katika mbio za kusaka kiatu cha dhahabu kwa kutimiza
mabao matano, akifuatiwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’ mwenye mabao
manne.
Simba
iliingia Nusu Fainali, baada ya kuongoza Kundi A, kwa pointi zake saba, baada ya
kutoa sare moja na kushinda mechi mbili, wakati Mtibwa inayofundishwa na Nahodha
pia na Nahodha wake wa zamani, Mecky Mexime, iliongoza Kundi B kwa pointi zake
tisa baada ya kushinda mechi zote tatu.
Kanuni za
mashindano haya ni kushirikisha timu zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi
Kuu za Bara na visiwani na mbili zilioongoza katika kupanda Ligi Kuu zote mbili,
lakini kwa Bara, Yanga waliokuwa washindi wa tatu msimu uliopita, walijitokea na
nafasi yao ikachukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye
Ligi Kuu.
Bingwa wa
michuano hiyo mipya itakayokuwa ikifanyika kila mwaka, ataondoka na Sh. Milioni
40, mshindi wa pili Sh. Milioni 20, wa tatu Sh. Milioni 15 sawa na wa nne,
wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5 kila moja.
AZAM WAKUBALI MATOKEO, WAIPA GWALA SIMBA B YA MATOLA
Kipre Tchetche wa Azam kulia |
AZAM FC
imekubali matokeo ya kutolewa katika Kombe la BankABC Sup8R na imewapongeza
Simba SC sababu timu yao ya vijana ni nzuri.
Msemaji wa
Azam FC, Jaffar Iddi Maganga alisema jana kwamba, bahati ilikuwa yao Simba SC,
kwani nafasi mbili walizopata walizitumia vizuri kwa kufunga mabao yao
yaliyowapeleka fainali.
Jaffar
alisema kwamba jana bahati haikuwa upande wa Azam, kwani walipoteza nafasi za
wazik za kufunga mabao zaidi ya tano.
“Mtu kama
Kipre Tcheche peke yake, alipoteza nafasi nne za wazi kabisa za kufunga akiwa
amebaki yeye na kipa, lakini hiyo ndiyo soka na sisi tumekubali
matokeo.
Tunawapongeza
Simba SC, tunarudi kambini kuanza kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii, ambayo
tutacheza tena na Simba,”alisema.
Wakati jana
Simba ilicheza timu ya vijana na Azam ilitumia wachezaji wengi wa akina, Mechi
ya Ngao timu zote zinatarajiwa kushusha vikosi vyake kamili vya Ligi
Kuu.
Mara ya
mwisho, vikosi kamili vya timu hizo vilikutana kwenye mechi ya Robo Fainali ya
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita na Simba
ilichapwa mabao 3-0, yote yakitiwa kimiani na John Raphael Bocco ‘Adebayor’,
ambaye kwa sasa yupo Afrika Kusini akifanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa
katika klabu ya Super Sport United.
MECKY MEXIME ASEMA WATOTO WA SIMBA HAWAMNYIMI USINGIZI
Mecky Mexime |
KOCHA wa
Mtibwa Sugar ya Morogoro, Mecky Mexime amesema kwamba ana matumaini ya kuwafunga
Simba B na kubeba na Kombe la Bank ABC katika fainali itayapopigwa keshokutwa
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza
na BIN ZUBEIRY jana, Mecky alisema kwamba amewaona Simba wakati wanaitoa Azam
kwa kuichapa 2-1 ni wazuri na wanacheza kwa uelewano sana, lakini Jumamosi
anaamini atawafunga tu.
“Kabla
sijawa kocha wa Mtibwa ya wakubwa, nilikuwa kocha wa vijana, na nilikuwa pia
kocha wa vijana wa Morogoro katika Copa Coca Cola, ambayo ilikchukuja ubingwa.
Kwa hiyo nawajua vijana, hivyo vijana wa Simba hawanipi hofu,”alisema
Mecky.
Mexime
alisema anajua namna ya kuwapoteza vijana uwanjani na kuvuna ushindi, tena wa
mabao ya kutosha kabisa,
Mtibwa Sugar
ilitinga Fainali kwa kishindo, kwa kuinyuka Jamhuri ya Pemba, mabao 5-1, ambayo
yalitiwa kimiani na Babu Ally Seif dakika ya 15, Salvartoy Ntebe dakika ya 17,
Mfaume Shaaban aliyejifunga dakika ya 38, Vincent Barnabas dakika ya 43 na Awadh
Juma dakika ya 85 wakati la kufutia machozi la Jamhuri lilifungwa na Mbarouk
Chande dakika ya 62.
Hadi sasa,
Mtibwa ndio timu pekee ambayo haijapoteza pointi hata moja kwenye mashindano
hayo baada ya kushinda mechi zake zote tatu za Kundi B, 2-1 dhidi ya Polisi
Moro, 2-0 dhidi ya Azam na 5-0 dhidi ya Super Falcon na jana 5-1 dhidi ya
Jamhuri katika Nusu Fainali.
Simba B
yenyewe ilitoa sare moja tu ya kufungana 1-1 na Jamhuri katika mchezo wa kwanza,
lakini mechi zake nyingine ilizifunga 2-0 kila timu, Mtende na Zimamoto ya
Zanzibar.
HUYU NDIYE PASCHAL OCHIENG, KISIKI KIPYA SIMBA SC KILICHOWAHI KUKIPIGA YANGA
JINA | Pascal Ochieng | ||
---|---|---|---|
KUZALIWA | Mei 15, 1986 | ||
ALIPOZALIWA | Kenya | ||
NAFASI | Beki | ||
KLABU ALIZOCHEZEA | |||
KLABU YAKE | Simba SC | ||
TIMU ZA WAKUBWA | |||
MWAKA | TIMU | ||
2000-2001 | Mathare United | ||
2001-2002 | Mazarea Dina | ||
2003-2004 | World Hope FC | ||
2004-2005 | Re-Union Nairobi | ||
2005 | Young Africans S.C. | ||
2005-2006 | Brabrand IF | ||
2006-2008 | Young Africans S.C. | ||
2008-2009 | Kenya Commercial Bank FC | ||
2010 | Posta Rangers F.C. | ||
2012 | Johor FC | ||
National team | |||
Tangu 2001- | anachezea timu ya taifa Kenya | Mechi 23 | (Bao 1) |
No comments:
Post a Comment