TIMU ya soka
ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na wenyeji Botswana
(Zebras) katika moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za kalenda ya Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo (Agosti 15 mwaka huu)
usiku.
Hadi
mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Molepolole ulioko Kilometa 40
nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Stars ndiyo
iliyokuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 17 lililofungwa kwa penalti na beki
Erasto Nyoni.
Mwamuzi
Lekgotia Johannes Stars alitoa adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile Ncenga wa
Zebras kumuangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyekuwa
akimkabili kipa Mompoloki Sephekolo.
Bao hilo
halikudumu muda mrefu, kwani Zebras walisawazisha dakika ya 26 baada ya shuti
kali lililopigwa na
Lemponye
Tshireletso nje ya eneo la hatari kumshinda nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja.
Dakika tano baadaye kiungo mshambuliaji Mwinyi Kazimoto aliifungia Stars bao la
pili kwa shuti la mbali.
Tshireletso
aliisawazishia tena Zebras dakika ya 37. Mfungaji alifunga bao hilo kwa kichwa
akiunganisha mpira wa krosi kutoka wingi ya kushoto uliopigwa na Tebogo Sembowa
ambaye kabla alimtoka beki Aggrey Morris.
Kipindi cha
pili kilianza kwa Kocha Kim Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo na Salum
Abubakar na nafasi
zao
kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman Idd. Safari hii Zebras ndiyo walioanza
kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo Michael Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa
kichwa akiunganisha krosi fupi iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika 13 za
mwisho Stars walicheza pungufu baada ya beki Erasto Nyoni kutolewa nje kwa kadi
nyekundu kutokana na kumchezea rafu mshambuliaji Lovemore Murirwa.
Mrisho Ngasa
ambaye alikuwa nyota kwenye mchezo huo aliisawazishia Stars dakika ya 84 baada
ya kugongeana one-two na mshambuliaji Simon Msuva aliyetokea benchi kuchukua
nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha ya
timu kucheza vizuri, tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ulinzi ambapo mabeki
waliruhusu mipira mingi ya krosi na kuwaacha washambuliaji wa Botswana wakifunga
bila bughudha. Mabeki hawatakiwi kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima
wahakikishe wanawadhibiti washambuliaji wa timu pinzani.
"Kwa upande
wa washambuliaji, Said Bahanuzi alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya
kimataifa akiwa na Stars tangu nilipomjumuisha kwenye timu kwa mara ya kwanza.
Kuna makosa madogo madogo ambayo niliyatarajia, hivyo nitamrekebisha polepole,"
alisema Kocha Poulsen mara baada ya mechi hiyo.
Stars; Juma
Kaseja, Erasto Nyoni, Amir Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank
Domayo/Shabani Nditi, Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd, Said
Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi
Kazimoto.
Zebras;
Mompoloki Sephekolo, Tshepo Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin Olerile, Oscar
Obuile Ncenganye, Mompati Thuma, Patrick Motsepe/Jackie Mothatego, Lemponye
Tshireletso, Michael Mogaladi, Tebogo Sembowa, Ntesang Simanyana na Galabgwe
Moyana/Lovemore Murirwa.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inarejea nyumbani kesho (Agosti 16
mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya Airways.
No comments:
Post a Comment