Wednesday, July 4, 2012

HUYU NDIYE THOM SAINTFIET, KOCHA ALIYEITWA NABII KWA KUFUNDISHA SOKA BAAB KUBWA

BIN ZUBEIRY na Saintfiet

Na Mahmoud Zubeiry
“NIMEKUWA nikisikia habari nyingi kuhusu Yanga, ni timu kubwa. Na ninafurahi kuja hapa, naamini nitafanya vizuri,”.
Ndivyo alivyoanza kuzungumza, Thom Saintfiet katika mahojiano na BIN ZUBEIRY mchana huu, baada ya kuwasili Dar es Salaam, tayari kusaini mkataba na kuanza kufundisha klabu hiyo.
Thom amepata mapokezi makubwa baada ya kuwasili na moja kwa moja alipelekwa makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam. Akiwa hapo, alionyeshwa ofisi na mataji mbalimbali ya klabu hiyo pamoja na Uwanja wa mazoezi na gym.
“Sifahamu sana kuhusu Yanga au Tanzania kwa ujumla, naamini mengi nitajifunza hapa, ila mimi kama mwalimu baada ya kukubali kuja Tanzania kufundisha, nilianza kujifunza kidogo kuhusu nchi hii na hususan Yanga,”alisema Thom alipoulizwa kama anaifahamu Yanga au soka ya Tanzania.
Kwa nini ameamua kuja kufanya kazi Tanzania, hususan Yanga? “Imetokea nimekubali, lakini nilikuwa nina ofa nyingine, ila nimetaka kubadilisha uzoefu wangu kwa sasa, kuwa kocha wa klabu badala timu za taifa,”alisema.

Thom Saintfiet akiwa na Kombe la Kagame
Jukumu lake la kwanza Yanga ni nini? “Kwa sasa unaliona Kombe lile (la Afrika Mashariki na Kati), nataka liendelee kuishi kwenye ofisi hii (ya Katibu wa Yanga), nina muda mfupi sana, lakini najua Yanga walitwaa Kombe lile mwaka jana na wanatakiwa kulitetea karibuni, nina uhakika hilo ndilo jukumu langu la kwanza,”alisema.
Alipoulizwa kuhusu muda, Saintfiet alisema kwamba Yanga imekuwa chini ya mwalimu msaidizi na ni mwalimu mzuri, hivyo anaamini alikuwa anafanya kazi yake vizuri. “Nitaungana naye, nianzie pale alipoishia tufanye pamoja kwa kushirikiana kuhakikisha, kwanza Kombe linabaki hapa.
Na viongozi wamenihakikishia timu ina wachezaji wazuri, nimeomba DVD za timu za karibuni ili nione wanachezaje katika mechi, na nikianza kazi naamini kila kitu kitakuwa sawa, Yanga ina wachezaji profesheno na wanajua wajibu wao, hivyo najua watakuwa vizuri na tutaelewana,”alisema.

Amesikia kuhusu Simba?
“Nimesikia kuhusu Simba, viongozi wangu wameniambia, nchi yenye timu za aina hii (wapinzani wa jadi), lazima soka yake inakuwa na msisimko mkubwa. Na upinzani huu ni changamoto kwangu. Lazima Yanga iongoze kila wakati. Najua kuna timu nyingine inasifika, Azam FC. Lakini mimi ni mpinzani wa kila timu ninayokutana nayo, na ninataka ushindi kila siku,”anasema.

Ametokea wapi huyu jamaa?
Tom Saintfiet anasema alizaliwa Machi 29, mwaka 1973 mjini Mol, Ubelgiji na kabla ya kuwa kocha alicheza soka katika nafasi ya kiungo kuanzia mwaka 1983 hadi 1997 alipostaafu na kuwa kocha akiwa ana umri wa miaka 24, akiweka rekodi ya kocha kijana zaidi kuwahi kutokea katika soka ya Ubelgiji.
Saintfiet anasema amefundisha nchi kadhaa kuanzia kwao Ubelgiji, Qatar, Ujerumani, Visiwa vya Faroe, Finland na Uholanzi.
Anasema pia ana uzoefu wa kutosha wa kufundisha soka Afrika akiwa amefundisha Namibia na Zimbabwe kama kocha Mkuu wa timu za taifa za nchi hizo.
Anasema kabla hajakwenda Namibia, Saintfiet alikuwa kocha wa klabu ya Ligi Kuu Finland, iitwayo RoPS Rovaniemi na mwaka 2002, alikwenda kuifundisha B71 Visiwa vya Faroe ambayo aliiwezesha kushika nafasi ya pili katika Ligi Daraja la kwanza. Anasema kutoka hapo, akaenda kuwa kocha wa Al-Ittihad Sports Club ya Qatar (sasa inaitwa Al-Gharafa SC) ambako alidumu hadi mwaka 2004 alipochukuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Qatar.
Anasema akiwa na U17 ya Qatar, aliiwezesha kushika nafasi ya tatu katika Kombe la Mataifa ya Asia na hivyo kufuzu kucheza Fainali za vijana za Kombe la Dunia la FIFA. Kuelekea Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, Saintfiet anasema alikuwa kwenye mpango wa kupewa timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, wakati huo akiwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo.
Anasema katika timu za taifa, mafanikio zaidi alipata akiwa na Namibia kwanza akiifikisha robo fainali ya michuano ya COSAFA kwa kuzifunga Comoro na Malawi na kutoka sare na Lesotho katika fainali zilizofanyika Afrika Kusini Julai mwaka 2008.
Hata hivyo, anasema Namibia ilitolewa na Afrika Kusini katika robo fainali, ambao mwishowe waliibuka mabingwa wakiwa wenyeji.
Anasema mafanikio yake akiwa na Namibia ni pamoja na kuifunga Zimbabwe 4-2 katika mechi ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) 4-0 katika mchezo wa kirafiki.
Anasema alipata heshima kubwa akiwa Namibia, kiasi cha kufikia hadi kuitwa ‘Nabii’ na Mtakatifu.
Anasema sababu ni kwamba, aliifanya Namibia ikawa inacheza soka nzuri na kupata pia mafanikio, ndiyo maana akawa anatukuzwa mno nchini humo.
Thom Saintfiet akizungumza na Waandishi wa Habari, makao makuu ya Yanga, Jangwani. Kulia ni Katibu wa Yanga, Celestine Mwesigwa na kushoto mmoja wa wafadhili wa klabu hiyo, Seif Ahmad 'Magari'.
Anasema moja ya matukio ya kukumbuka ni siku tatu baada ya kutoka sare 1-1 ugenini na Lebanon Aprili mwaka 2009, Namibia ilipata matokeo ya kuvutia ya sare ya bila kufungana ugenini na Angola.
Lakini matokeo mazuri zaidi na yaliyomfurahisha ilikuwa ni mjini Durban, wakati Namibia ilipotoa sare ya 1-1 na Afrika Kusini, baada ya kuongoza sehemu kubwa ya mchezo huo. Anasema kwa miezi kadhaa, Namibia ilikuwa imeshinda mechi moja tu kati ya 12 kabla ya kuwasili kwake nchini humo.
“Baada ya mafanikio makubwa, vyombo vya habari Namibia vilinipa jina la utani The Saint (Mtakatifu) na gazeti moja lilidiriki kuniita The Messiah (Nabii).
Baada ya hapo alisaini mkataba wa miaka minne na Shirikisho la Soka Zimbabwe (ZIFA) Oktoba 1, mwaka 2010, lakini anasema kutokana na matatizo ya kutopewa kibali cha kufanya kazi nchini humo, alifanya kazi katika mazingira magumu, hadi Desemba mwaka 2010 alipoamua kubwaga manyanga na kujiunga na Shabab Al Ordon.
Anasema alisaini mkataba wa miezi minne na mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Asia mwaka 2007, Shabab Al Ordon na alifanya kazi nzuri ya kutukuka huko, akijenga ukuta imara ambao katika mechi tano uliruhusu bao moja tu.
“Baada ya mechi sita, tukishinda tatu na kutoka sare tatu, nilitosheka na nikaiacha timu ikiwa katika nafasi ya pili na haijafungwa,”alisema.
Anasema baada ya kupokea ofa kutoka timu tatu za taifa za Afrika, aliikubali ya Ethiopia na mwishoni mwa Mei mwaka 2011 akaanza kazi.
Baada tu ya kusaini mkataba, Saintfiet anasema ndani ya siku 10 alikuwa ana mtihani mzito wa kucheza na Nigeria kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2012.
“Nigeria ilikuwa imetoka kuifunga Argentina 4-1 siku nne kabla ya mechi yetu na wao na pia iliifunga Ethiopia 4-0 katika mechi ya kwanza ya AFCON nyumbani, lakini hadi mapumziko niliiongoza timu kumaliza kwa kufungana 1-1. Tulifanikiwa kupata bao la kuongoza kipindi cha pili, lakini kwa bahati mbaya beki Joseph Yobo akasawazisha ikawa 2-2 mwisho wa mchezo,”anasema.
Kwa mara nyingine, Saintfiet anasema akajizolea sifa kemkem kwa staili yake ya ufundishaji baada ya kuifanya Ethiopia kuwa timu ya ushindani yenye kucheza soka maridadi hata dhidi ya vigogo kama Nigeria.
“Baada ya mechi, kocha wa Nigeria, Samson Siasia alisema amestaajabishwa mno na soka ya kitaalamu na nidhamu ya hali ya juu ya Ethiopia na Nigeria hawakupata majibu. Licha ya kukubalika sana, lakini Oktoba 28, mwaka jana nilijiuzulu, baada ya kupata ofa ya Nigeria” anasema.
Machi 28, mwaka huu, Mbelgiji huyo anasema alipewa mkataba wa miaka minne wa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Nigeria, lakini Juni, mwaka huu akaamua kuvunja mkataba huo baada ya kuvutiwa na ofa ya Yanga.

NONDOZ ZA ‘MTAKATIFU’ THOM
Saintfiet anasema ana leseni Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) ya kufundisha soka ya kulipwa popote barani humo, ambayo aliipata mwaka 2000.
Anasema kati ya mwaka 2006 na 2007 alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa FC Emmen ya Daraja la Kwanza Uholanzi na pia amewahi kufanya kazi kama Mshauri wa Ufundi wa Shirikisho la Soka la Kazakhstan.
Anasema amewahi kuwa Mchambuzi wa soka katika Televisheni katika nchi za Ubelgiji, Afrika Kusini na Namibia na alifanya kazi kama mkalimani DFB. Anasema amesomea Saikolojia ya Michezo na Uchumi.
Anasema anazungumza lugha kibao na kwa ufasaha zaidi ni Kiholanzi, Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kifaroe na ‘ana jua jua’ Kiarabu, Kiafrikana na Kispanyola.
Naam huyo ndiye Thom Saintfiet, ambaye anatarajiwa kusaini mkataba wa kuinoa Yanga, akiwa tayari amekuja nchini kikamilifu. Je, Yanga imepata mwalimu? Je, watadumu naye? Je, hayatajirudia yale yale? Bila shaka hayo ni mambo ya kusubiri na kuona, ila kwa mujibu wa wasifu wake, huyu ni mwalimu wa uhakika

No comments: