Na Juma
Mohamed, Dar es Salaam.
WANANCHI na
wakulima wa zao la korosho wametakiwa kula kwa wingi zao hilo ili kuimarisha
afya zao na kukuza soko la ndani litakalopelekea kukua kwa uchumi wa taifa.
Hayo
yamezungumzwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mfaume Juma,
alipozungumza na NEWS ROOM muda mfupi baada ya kumalizika kwa sherehe ya
kuadhimisha siku ya kuhamasisha kula korosho Tanzania, iliyofanyika katika
ukumbi wa Mfaume Kawawa katika viwanja vya Mwl. J.K. Nyerere (Sabasaba) jijini
Dar es Salaamm.
Alisema zao
hilo linafaida nyingi kwa binadamu ambazo sio za kubuni na kwamba hata nchi
zilizopiga hatua katika uuzaji wa korosho zilizo banguliwa ambazo ni Vietinam
na India, zinatangaza manufaa yake katika soko la kimataifa.
Alizitaja baadhi ya faida ambazo mtu anaweza
kuzipata baada ya kula korosho kuwa ni kuongeza viini lishe mwilini ambavyo ni
muhimu zaidi kwa watoto wadogo wanaoanza kula, akina mama wanaonyonyesha na
hata kwa wagonjwa, kuwawezesha kupata nguvu na maendeleo ya ukuaji wa mwili.
“Korosho
vilevile zina viini vingine vingi tu vya kuongeza madini na joto katika mwili,
kwa mfano korosho zina ‘protine’ nyingi sana na ni mara mbili zaidi ya mtu
anaekula samaki au nyama wakati zenyewe sio nyama wala sio samaki..ndio maana
katika nchi kama India, kwa kufahamu umuhimu huo wengi wao hawali nyama kabisa
na badala yake wanakula korosho kwa lengo la kupata kile ambacho kinapatikana
katika nyama..” alisema Mfaume.
Akizungumzia
kuhusu kufanya maadhimisho hayo katika viwanja vya sabasaba, alisema dhamira
yao sio kuiadhimisha tu katika sherehe za sabasaba bali wanafanya hivyo
kwasababu ni maonyesho makubwa ya kibiashara, na kwamba wanahamasisha ulaji wa
korosho hata katika maonyesho ya wakulima (siku ya nae nane) ambayo yatafanyika
mkoani Lindi, lengo likiwa ni kuendana na matukio makubwa ya kitaifa ya
kibiashara.
“Mwaka huu
tumedhamiria kupeleka ujumbe huu kwenye Nane Nane katika mikoa mingine ambayo
hailimi korosho, kwa mfano Mwanza, Arusha au Mbeya..kwahiyo dhamira hii ni
endelevu na inaendana na matukio kwasababu lengo sio kufanya katika ngazi ya
mkoa, tunaangalia matukio yanayokusanya jamii kubwa zaidi ili ujumbe ufike kwa
pamoja..” aliongeza.
Kwa upande
wake, katibu mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho (WAKFU) Suleiman
Lenga, alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaboresha ubanguaji wa zao hilo
ambapo kwa sasa wameshapata maeneo matatu kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vitatu
vya ubanguaji.
“Tunao
utaratibu wa ujenzi wa viwanda vitatu vya ubanguaji wa korosho, tunavijenga
maeneo ya Mangamba Mtwara, ambako tumepata hekari 20 lakini vilevile Mkuranga
na hatimae Tunduru, tutajenga viwanda vyenye uwezo wa kubangua tani 30, 000 kwa
maana ya tani 10, 000 kwa kila kiwanda.” Alisema.
Naye mjaasiliamali
anaejihusisha na uuzaji wa zao hilo kutoka wilayani Masasi mkoani Mtwara,
Bernadeta Ndemanga, alisema wananchi wanahamasika kwa kiasi kikubwa kula
korosho lakini hakusita kueleza changamoto zinazowakumba kuwa ni malighafi kuwa
ghali zaidi na kupelekea wao kuuza ghali zao hilo.
Alisema changamoto
nyingine wanayokumbana nayo ni uhaba wa vifungashio, ambapo wanalazimika kutumia
vinavyotoka nchini China jambo ambalo linakua kikwazo kwa wajasiliamali wadogo
na hata wale waliopo wilayani kufikiwa kwa wakati na kujikuta wanatumia gharama
kuvifuatilia jijini Dar es Salaam.
…………………………..mwisho………………………………………………..
No comments:
Post a Comment