Saturday, July 16, 2016

Shule ya Msingi Magomeni Mtwara yakabiliwa na uhaba wa madarasa, matundu ya vyo na nyumba za walimu.



Choo kinachotumiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Magomeni, manispaa ya Mtwara Mikindani.


Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akikata utepe na afisa mtendaji mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania, Ken Cockerill, kuashiria uzinduzi wa vyumba viwili vya madarasa yaliyojengwa na Benki hiyo katika shule ya msingi Magomeni, manispaa ya Mtwara Mikindani.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

Shule ya msingi Magomeni iliyopo manispaa ya Mtwara Mikindani inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa miundombinu ikiwa ni pamoja na upungufu wa vyumba vinane vya madarasa, matundu ya vyoo pamoja na ukosefu ya nyumba za walimu.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa jengo la vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu kutoka kwa Benki ya Stanbic, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Rashid Kajonjo, alisema licha ya msaada huo uliombatana na sare za wanafunzi, bado wanahitaji wadau kuwasaidia Zaidi.
“kimsingi tuna upungufu wa madarasa Manane kwa sasa kati ya madarasa 16 tunayohitaji lakini tuna upungufu wa ofisi moja ya walimu lakini hatuna nyumba hata moja katika eneo hili walimu wote wanatoka nje ya eneo hili sasa inakuwa ni hatari kidogo kwa usalama..” alisema Kajonje.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego na afisa mtendaji mkuu wa Benki ya Stanbic, Ken Cockerill wakifunua pazia katika jiwe la msingi katika jengo la vyumba viwili vya madarasa lililojengwa na benki hiyo katika shule ya msingi Magomeni, manispaa ya Mtwara Mikindani.

Baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wa shule hiyo, wameshukuru msaada huo na kuwaomba wadau wengine wazidi kusaidia shule hiyo, huku mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa Benki hiyo, Desderia Mwegelo akizungumza kwa niaba ya afisa mtendaji mkuu Ken Cockerill, ameahidi kuendelea kuisaidia shule hiyo.
“tunaomba na serikali ya Jamhuri ya Muungano akiwemo na Rais John Pombe Magufuli Mungu ampe maisha marefu kwakweli, azidi kutuunga mkono kwakweli azidi kutusaidia hiki alichokitoa azidishe hapa wakiwemo wadau, wadahamini na wawekezaji wanaokuja Tanzania kwa vile mkoa wa Mtwara tunawaombea kwakweli..” alisema Aisha Mwidini.
“Tumekuja kuzindua rasmi boksi mbili za madarasa na ofisi ya mwalimu mkuu, pia kuna michango kadhaa ilikuwa imeletwa na wafanyakazi wa Stanbickwa ajili ya kuwezesha ununuzi wa sare za shule kwa wananfunzi wa Magomeni Primary..” alisema Desderia Mwegelo.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akipokea zawadi ya picha kutoka kwa afisa mtendaji mkuu wa Benki ya Stanbic, Ken Cockerill, katika hafla ya kupokea jengo la vyumba viwili vya madarasa kutoka kwa benki hiyo.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego amemwagiza mkurugenzi wa manispaa hiyo kusimamia ujenzi wa chumba kimoja cha darasa ambacho amepiga marufuku kutumika kutokana na kuwa na nyufa, huku akiwataka wazizi kushiriki kwa kutoa michango katika ujenzi wa vyoo.
“Nimwagize mkurugenzi ndani ya siku saba pale ni padogo sana, awe amekarabati darasalile kabla ya watoto kuingia darasani..mkuu wa shule umenisikia watoto wasiingie, mkurugenzi umenisikia ndani ya siku saba mimi na DC tutakuja kukagua lile darasa.” Aliagiza Dendego.
Aidha, aliendesha zoezi la harambee ya kuchangia ujenzi wa vyoo vya wanafunzi wa shule hiyo ambapo aliwaamuru wazazi na walezi waliokusanyika shuleni hapo kwa kumtaka kila mmoja achangie alichonacho.
Mkoa huo umetekeleza agizo la kutatua changamoto ua uhaba wa madawati kwa shule za msingi kwa Zaidi ya asilimia 100, kutokana na kuwa na ziada ya madawati 265.


No comments: