Tuesday, March 8, 2016

Biashara ya Uji yampa umaarufu na Kiwanja Mtwara mjini..

Mfanyabiashara maarufu ya Uji Shuwea Salum, akisafisha vitendea kazi vyake baada ya kumaliza kazi.




Na Juma Mohamed, Mtwara.

KUMILIKI kiwanja katika manispaa ya Mtwara Mikindani kwa miaka hii sio kazi rahisi kwani wapo vijana wengi na hata watu wazima ambao bado wanapambana kwa hali na mali ili kuweza kufikia hatua hiyo amayo inaaminika kuwa ni hatua mojawapo kubwa ya mafanikio katika safari ya maisha.
Ardhi inapanda thamani kwa kasi na kwamba katika manispaa hiyo inakuwa sio kitu rahisi kutokana na ukweli kwamba kumekuwa na kasi ya maendeleo kutokana na uwekezaji unaofanyika zaidi ukitokana na uwepo wa rasilimali za mafuta na gesi zilizopo katika mkoa huu wa Mtwara, kiasi cha kuwafanya wawekezaji kuhitaji maeneo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa hoteli, ofisi, shule, vyuo na viwanda.
Wapo baadhi ya wajasiliamali wadogo ambao ukiambiwa kuwa wanamiliki ardhi ndani ya manispaa hii kwa biashara zao ndogondogo za kila siku wanazozifanya pengine hutoamini kwa haraka, lakini ukweli ni kwamba wapo na miongoni mwao ni wanawake.
Shuwea Salumu Mpatane ‘Mama Uji’ ni mama maarufu sana katika mtaa wa Ligula hasa katika eneo la kuzunguka uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, kutokana na biashara yake ya kuuza uji wa ulezi kwa kutembeza mtaani ambayo licha ya kumpa umaarufu huo, imemfanya kuwa miongoni mwa wanaomiliki viwanja ndani ya manispaa hiyo chenye thamani ya sh. Milioni 1 na mwaka huu ujenzi unatarajiwa kuanza.
Anasema katika harakati za kuanza kwa ujenzi huo katika eneo la nusu heka tayari ameshapata bati 25 ambapo anataraji kuanza kujenga nyumba yake itakayokuwa na uwezo wa kuwa na vyumba viwili na ukumbi.
Shuwea alianza biashara ya uji miaka sita iliyopita katika eneo hilo la Nangwanda akianza kwa kuuza kikombe kimoja sh. 200 kabla ya kupandisha mpaka sh. 300 na sasa ikiwa ni sh. 500 huku anadai sababu za kupandisha bei ni kutokana na kupanda kwa gharama za mahitaji.
Anasema mbali na kumiliki kiwanja hicho, mafanikio mengine anayojivunia kupitia biashara hiyo ni kuweza kumudu kulipa pango ya mahala anapoishi sasa na kuweza kuwasomesha watoto wake watatu huku mmoja akiwa amehitimu kidato cha Nne mwaka jana katika shule ya sekondari ya Chuno, mwingine ndio anaingia kidato cha kwanza mwaka huu na mwingine wa mwisho ana umri wa miaka tisa yupo darasa la kwanza.

Shuwea Salum

“Kipindi ambacho biashara ilikuwa nzuri kwasiku ilikuwa narudi na 40,000 lakini kwa sasa hivi nimepunguza kipimo kutokana na uchumi wenyewe umeshuka na pesa imekuwa ngumu, sasa hivi narudi na 25,000 au ikizidi sana 30,000..katika hiyo, nikitoa gharama za manunuzi ya mahitaji, naweza kupata faida ya sh. 15,000 kutokana na mahitaji yenyewe sasa hivi kuwa yamepanda bei..anasema Shuwea na kuongeza:
“Ulezi nakuwa nasaga tu unga kama kilo 20 hivi natumia muda wa wiki mbili, kwa siku nauza chupa 10 ambazo zinaingia vikombe saba, nauza na maandazi..sina biashara nyingine zaidi ya uji.” Anaongeza.
Kutokana na kufanya kazi na watu ambao miongoni mwao wapo wa kila aina ya tabia, yani zile zenye kuwa njema na zile ambazo humkwaza na kuwa kikwazo katika biashara, anasema wapo anaogombana nao juu ya malipo na wengine hata kumdhurumu ambapo anaamua kuachana nao na kuwakwepa kwa kutowapitishia tena siku nyingine.
Anasema akili ya kufanya biashara hiyo ilimkuta mara baada ya kuachika kutoka kwa aliyekuwa mume wake ambaye ndio alizaa naye watoto hao watatu, na kwamba alianza kwa kujaribu ili aone kama ataweza kuyamudu maisha huku akiwa hana mume.
“Wakati nimeanza ni pale baada ya kuachika na kuona ugumu wa maisha ndio nikaona nianze hii biashara, yani kujaribu kama nikifanya hii biashara je nitauza au..lakini baadae nikaona nina wateja, na hapa Umoja (Nagwanda) nilipoanza sijui kulikuwa na mabanda Matano tu ndio yalikuwa yamefunguliwa, hakukuwa na watu wengi kwakweli kama ilivyokuwa sasa hivi..na nilianza na uji chupa mbili kabla ya sasa kufikia hizo chupa 10..” anasema Mama Uji.
Mama Uji anasema malengo ambayo amejiwekea hapo baadae ni kubadilisha biashara kutoka kuuza uji na kuamua kufanya biashara ya kuuza nguo za kike aina ya Madera ambazo atakuwa akizifuata jijini Dar es Salaam na kwenda kuziuza huko vijijini.
Shuwea anasema katika familia yao wamegawanyika katika kufanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato ambapo wapo wafanyakazi na wafanyabiashara, huku yeye akiwa na ndugu yake mmoja wakuzaliwa nayeshirikiana naye katika majukumu mengine tangu mama yao mzazi alipofariki dunia mwaka 1995.
Anasema kutokana na kuachika katika ndoa mbili katika mazingira magumu na kunyanyasika, kwa sasa hafikilii suala la kuolewa tena labda mpaka pale atakapojiridhisha juu ya kujiweka sawa kimaisha ili hata akiamua kuolewa awe tayari ana vitu vyake mwenyewe na miradi ya kumuingizia kipato.
“Kwa sasa hivi kwasababu nilishapata changamoto za wanaume kunitelekeza, sitokubali mpaka pale nitakapofanikisha malengo yangu, kwasababu mume wakwanza ambaye ndio baba wa watoto wangu aliniacha katika mazingira magumu sana na ndio kisa cha kuanza kuuza huu uji..” alisema na kuongeza:
“Aliniacha kwenye mazingira ya utata nikawa naishi maisha ya shida nikasaidiwa tu na watu wakanilipia pango marafiki zangu ambao naongea nao vizuri, nikaolewa tena ndoa yapili vilevile ikawa mtihani kwahiyo nimejifunza kwamba sitoolewa mpaka mambo yangu yawe safi na akinusumbua niweze kuishi kwangu..” aliongeza.
Nilipata kuzungumza na mmoja wa wateja wake wakubwa wa biashara yake, Charles George, ambaye ni katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (Mtwarefa), ambaye ana zaidi ya miezi Minne tangu aanze kupata huduma hiyo alisifia na kudai kuwa kadiri siku zinavyoenda mama huyo ndio anazidi kuboresha huduma zake.
Anasema licha ya kupata huduma, muda mwingine anatumia utu uzima wake na uteja wake wa muda mrefu kuweza kumshauri namna ya kuishi vizuri na wateja wake ili azidi kuwavutia wengi zaidi.
“Kwa uzoefu wangu na kwasababu ni mtu mzima na najua maana ya biashara au uteja, mara nyingi huwa najitahidi kumpa maelezo ambayo yatamsaidia kuweza kuvuta wateja wengi, na kikubwa ambacho namshauri mara nyingi ni kuwa na lugha nzuri kwa wateja wake..” alisema.
Pamoja na jitihada anazozifanya Shuwea za kuhakikisha anafikia malengo yake, lakini bado anakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kukosa ofisi kwa ajili ya biashara yake na kukosa msaidizi ambaye anaweza kumsaidia iwapo atapatwa na dharura.
Anasema anajitahidi kufanya bidii za kumpata msaidizi lakini changamoto anayoipata ni wale anaowaomba kwa ajili hiyo kudai kuwa hawawezi kufanya kazi hiyo kwasababu ni ngumu kwao, ukizingatia hana ofisi maalumu hivyo itawalazimu na wao watembeze uji kama anavyofanya.
Kutokana na jitihada zinazofanywa na mifuko ya hifadhi ya jamii nchini za kuanzisha mafao mbalimbali ya kuwainua wajasiliamali wadogo, bado ‘Mama Uji’ hajatambua fursa za kujiunga na mifuko hiyo ambapo miongoni mwa faida anazoweza kunufaika nazo ni pamoja na kuwa na bima ya afya ambayo inaweza kumsaidia akipatwa na ugonjwa.
“Nilikuwa nae Bima ya Afya ila huyo mume ambaye nilikuwa naye alikuja kuninyang’anya..siku aliyokuja kuninyang’anya alisema inabidi zibadilishwe alafu atanirudishia lakini mpaka leo nikimkumbusha hakuna anachonieleza cha maana na mimi nikaamua ‘kupotezea’ lakini nilishamwambia kwamba mimi ni mzazi mwenzako na endapo nitafariki basi na wewe jukumu la watoto utakuwa nalo..” alisema.
Anasema bado hajawahi kuhudhuria mafunzo yoyote ya ujasiliamali na hata zinapotokea semina zinazoendeshwa na mifuko ya hifadhi ya jamii juu ya namna ya kuwafikia wajasiliamali wadogo, hajabahatika kuhudhuria kwahiyo hana elimu yoyote ya kuweza kunufaika na mafao yanayotolewa na mifuko hiyo.
Wiki mbili zilizopita nilipata bahati ya kuhudhulia semina ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF ambapo pamoja na mambo mengine, ilikuwa na lengo la kutambulisha mafao mapya mawili ambayo ni fao la Uzazi na fao la Wote Scheme ambalo linawanufaisha wajasiliamali wadogo.

Meneja Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF kanda ya kusini.

Meneja wa PPF kanda ya Kusini, Kwame Temu, anasema kutakuwa na programu maalumu ya kukutana na wadau wa sekta zisizo rasmi miongoni mwao ni hawa wajasiliamali wadogo hapo baadae lakini wameona ni bora kupitia semina hiyo kutoa elimu juu ya mafao hayo ambapo aliwataka wanachi wa Mtwara kuchangamkia fursa za kujiunga na mfuko huo.
Shuwea iwapo ataamua kujiunga na mfumo wa Wote Scheme wa PPF, miongoni mwa huduma atakazo faidika nazo ni pamoja na kupata kadi ya bima ya afya na kuweza kupata mikopo ya Elimu au Timiza Ndoto Yako kupitia benki ya posta, huduma ambazo zinatolewa kwa kuchangia kiasi kinachoanzia sh. 20,000 kwa mwezi.
Pia nitoe rai kwa mifuko hii kuweza kupanua wigo wa kuwafikia hawa wajasiliamali wadogo na kuhakikisha wanapata taarifa na elimu ya kutosha juu ya namna watakavyoweza kunufaika na huduma wanazozitoa.








No comments: