Sunday, December 6, 2015

MAMCU warejesha tani 4,000 za korosho kutoka kwa walanguzi.


Kaimu Meneja mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Kalvin Rajab, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), juu ya hali ya mauzo ya zao la Korosho tangu msimu wa 2015/2016 ulipozinduliwa mwezi Septemba mwaka huu.




Na Juma Mohamed-Mtwara.

JUMLA ya Tani 4,000 za korosho zimekusanywa na Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU kutoka kwa wanunuzi holela wa zao hilo (Kangomba), kufuatia jitihada zinazofanywa na Bodi ya Korosho Tanzania za kudhibiti ununuzi huo katika maeneo mbalimbali yanayolima korosho.
Akizungumza mkoani hapa, kaimu meneja mkuu wa chama hicho, Kalvin Rajabu, alisema, kumekuwa na jitihada za dhati zinazofanywa na bodi kuhakikisha wanatokomeza ulanguzi huo ambao umekithiri katika maeneo ya vijijini na kwamba jitihada hizo zinaonesha kufanikiwa.
“Pale katikati kulikuwa na changamoto, vyama vya msingi vilikuwa vinakosa korosho kutokana na wanunuzi hawa holela, lakini tunashukuru jitihada zilizofanywa na bodi ya korosho wameza kusimamia na kuhakikisha wale waliokuwa wakinunua kwa Kangomba wanawadhibiti na korosho kurudishwa kwenye vyama vya msingi..kwahiyo ukija kuangalia wastani wa Tani 4,000 tumeweza kuzipata baada ya bodi ya korosho kufanya kazi yao vizuri..” alisema.
Alisema, hali ya mauzo kwanzia mwezi septemba ulivyozinduliwa na bodi, inaenda vizuri na kwamba mpaka kufikia Novemba 27 mwaka huu chama hicho tayari kimeshafanya minada saba ambapo jumla ya Tani 30,588 ziliingizwa sokoni na kuuzwa.
Aidha, alisema, chama kilifanikiwa kusambaza fedha katika halmashauri za Mtwara manispaa, Mtwara vijijini, Masasi, Masasi mjini na Nanyumbu kiasi cha zaidi ya sh. Bilioni 99 ambazo anaamini zimeshawafikia wakulima kutokana na mauzo ya korosho zao.
Alisema, halmashauri za wilaya za Mtwara manispaa na Nanyamba zilisambazwa jumla ya sh. Bilioni 12.9, wakati upande wa halmashauri ya Masasi ni bilioni 23.5 huku Masasi mjini wakipatiwa kiasi cha bilioni 2 na bilioni 10.5 zikienda katika halmashauri ya Nanyumbu.
“Hali ya biashara katika minada mbalimbali ilikua nzuri, tulianza na bei ya sh. 2,407 mpaka kufikia bei ya sh. 2,700..hali imeonekana sio mbaya sana kwamba soko linakua na mwelekeo nzuri, lakini mpaka kufikia mnada wa mwisho, jumla ya makusanyo katika maeneo yote ya MAMCU ambao tunafanya kazi katika wilaya tatu za Mtwara, Masasi na Nanyumbu, jumla ya tani 33,933 tumeweza kukusanya na kuuza.” Aliongeza.


No comments: