Sunday, December 6, 2015

MWETA: Timu ya Taifa iandaliwe kwa miaka 5-10.


Golikipa na Nahodha wa timu ya soka ya Ndanda Fc, Wilbert Mweta, akiwa katika mahojiano maalum na mtandao huu wiki iliyopita juu ya maendeleo ya soka la Tanzania na juhudi zake binafsi anazozifanya katika kukuza soka la vijana hapa nchini.



Wilbert Mweta, akiwa na baadhi ya wachezaji wenzake wa Ndanda Fc katika moja ya michezo ya Ligi kuu msimu uliopita.




Wilbert Mweta, (mwenye fulana jeupe) katika bonanza la michezo siku ya uzinduzi wa Taasisi yake ya Mweta Sports Center ya jijini Mwanza.



Na Juma Mohamed.

NAODHA wa timu ya soka ya Ndanda Fc ya mkoani Mtwara na mkurugenzi wa Taasisi ya michezo ya Mweta Sports Center ya jijini Mwanza, Wilbert Mweta, amesema ili Tanzania ifanikiwe katika soka ni lazima kuwe na mipango thabiti katika kukuza vipaji vya vijana.
Alisema, Watanzania wamekuwa watu wakupenda kuona mafanikio siku zote bila kuwa na mipango kwanzia ngazi za chini kwa ajili ya kuandaa mikakati ya kufikia mafanikio, jambo ambalo linakwamisha hasa timu ya Taifa ambayo mara nyingi imekuwa ikishiriki michuano mbalimbali ya Kimataifa bila mafanikio yoyote.
Alisema, iwapo wachezaji wengine wa Tanzania watakuwa na malengo kama yakwake ya kuamua kuanzisha vituo vya michezo kwa ajili ya kukuza soka la vijana, basi utakuwa ni mchango mkubwa kwa Taifa na kwao wenyewe kwasababu itakuwa ni fursa nyingine ya kujiajiri.

Nembo ya Kituo cha Michezo cha Mweta Sports Center (MSC) kinachomilikiwa na Nahodha wa timu ya soka ya Ndanda Fc, Wilbert Mweta, cha jijini Mwanza.



Mweta ambaye kituo chake kilipata usajili rasmi mwezi January mwaka huu na kuwa na jumla ya vijana 86 wenye umri kuanzia U-17 ambao wapo 36, U-14 walio 24 na U-12 ambao wapo 26, alisema iwapo atapata nafasi ya kukutana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, atakuwa na mambo manne ya kumshauri.
Jambo la kwanza alisema ni kuja na mpango wa muda mrefu wa kuwaandaa vijana ambao baada ya miaka mitano hadi kumi watalifanya Taifa kuwa na timu imara yenye kuweza kushindana katika mashindano makubwa.
“Mambo mengine ambayo nitamshauri Rias Jamal Malinzi ni kwamba waamuzi wa mpira wafanye kazi yao, wachezaji tufanye kazi yetu na vyama husika vya mpira ngazi zote kwanzia chini mpaka juu vifanye kazi zao kama kanuni na sheria zinavyosema na mwisho wa siku tutapata bingwa ambaye ni bingwa kweli..” alisema.
Kuhusu kuchezea timu ya Taifa, alisema kwasasa hafikirii kabisa suala hilo na hana ndoto hizo kwasababu anaamini kuwa Watanzania bado wanahitaji ushindani na kwenda katika michuano mikubwa kama Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) huku jitihada zilizoonyeshwa na wachezaji waliopo kwasasa zinaonekana kutofanikia na hata yeye anaona kiwango chake hakina tofauti na wachezaji waliopo katika timu hiyo, hivyo kuwepo kwake hakutoongeza kitu.

Wilbert Mweta akiwa mazoezini kujiandaa na moja ya michezo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara



“Nikiitwa timu ya Taifa nitauliza maswali mawili kwamba wameniita kwasababu gani, kwenda kucheza mpira nadhani jibu la kwanza litakuwa ni hilo..sasa nitauliza kwamba nakwenda kushindana au nakwenda kushiriki, wakiniambia kwenda kushiriki nitakwenda lakini kama kwenda kushindana sitoweza kwenda..” alisema Mweta ambaye wiki mbili zilizopita aliandaa bonanza lililohusisha wachezaji wenzake wanaocheza Ligi Kuu na kuambatana na uzinduzi wa kituo chake cha michezo.
Alisema, katika bonanza hilo lililohudhuriwa na baadhi ya wachezaji hao waliweza kuungana na kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya polisi na watu walijitokeza kwenda kuwashuhudia huku wakichangia kiingilio ambacho baadaye kilisaidia kutunisha mfuko wa kituo hicho ambacho bado kichanga na kimeweza kuajiri watu kadhaa ambao wanafanikisha maendeleo ya vijana.

Wilbert Mweta, (mwenye fulana jeupe) katika bonanza la michezo siku ya uzinduzi wa Taasisi yake ya Mweta Sports Center ya jijini Mwanza.



“Nawashukuru wale waliokuja kuhudhuria, ila wale walioshindwa naamini ni kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi na umbali waliokuwepo, lakini waliokuja tulicheza bonanza lile na vijana walicheza na sisi tulicheza mechi yetu na timu ya polisi na tulipata kiingilio pale ‘getini’..pesa iliyopatikana tuliweza kununua vifaa vya michezo, kwahiyo walichangia kwa nanma moja au nyingine, napenda wawe na moyo wa aina hiyo nikiwahitaji waje watoe ‘sapoti’ kituo sio cha Mweta bali ni cha Watanzania wote pengine itafika siku hata watoto wao watakuja pale tukawalea..” alisema.
Mweta alisema, kabla ya kuwa na kituo hicho, alikuwa anaendesha Klabu ambayo ilikuwa na wachezaji kadhaa ambayo alianza nayo toka mwaka 2013 lakini baadaye mawazo yake yakapanuka zaidi na kuamua kuanzisha kituo hicho ambacho kimepata usajili wake mwezi Januari mwaka huu.

Moja ya vikosi vinavyozalishwa katika kituo cha Mweta Sports Center (MSC) cha jijini Mwanza kinachomilikiwa na Golikipa na Nahodha wa timu ya soka ya Ndanda Fc ya mkoani Mtwara, Wilbert Mweta.



Alisema, katika Klabu hiyo, kulikuwa na wachezaji watano ambao walifanikiwa kusajiliwa katika timu za Kurugenzi ya Iringa inayoshiriki ligi ya Daraja la Kwanza ambao walisajili vijana wawili, huku wengine wakielekea kusajiliwa na timu ya Bulyanhulu Fc.
Alisema, Taaisi yake kwasasa inauongozi ambao unaaminika kiasi cha kumfanya asipatwe na wasiwasi wowote kwa kipindi ambacho anakuwa mbali nacho kwasababu ameajiri watu katika idara kadhaa ikiwa ni pamoja na Meneja Mkuu, Meneja Masoko, katibu pamoja walimu watatu ambao wanashirikiana kuhakikisha mambo yanaenda sawa.
Katika watumishi aliyonao, wapo ambao amewaajiri kabisa na wapo ambao wanajitolea kwa moyo wa dhati, na kwamba wale walioajiriwa ni jukumu lake mwenyewe kuweza kuhakikisha anawalipa huku akisema mpaka sasa bado hajaanza kuingiza faida ya kipato kutokana na Taasisi hiyo na kumfanya atumie ghalama zake zaidi kuweza kuiendesha.
Alisema, wapo baadhi ya wadau ambao wameonesha nia ya kutaka kumsaidia katika baadhi ya maeneo katika taasisi yake, huku akitoa wito kwa wadau wengine wa soka na wapenda maendeleo kwa ujumla kuweza kufika kituoni hapo kuona kile kinachofanyika na hatimae waweze kushawishika kwa kumuunga mkono jitihada zake kwa kumfadhili ili kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu hapa nchini.
Lengo lake ni kuwa miongoni mwa wanamichezo wanaomiliki vituo bora vya michezo barani Afrika hapo baadaye, ili kutoa mianya kwa wanamichezo wengine kuweza kufanya kama yeye na kulitoa Taifa hapa lilipo na kulisogeza katika hatua nyingine zaidi kimichezo.




No comments: