Monday, June 22, 2015

Serikali yatakiwa kuuhurumia mkoa wa Mtwara.




 

Na Juma Mohamed, Mtwara.

SERIKALI imetakiwa kuungalia kwa jicho la huruma mkoa wa Mtwara ili kuhakikisha unapiga hatua kimichezo kutokana na uhaba wa wachezaji wanaowakilisha mkoa katika timu za taifa.

Wito huo ulitolewa wiki iliyopita mkoni hapa na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi, alipozungumza na NEWS ROOM baada ya kumalizika kwa kozi ya utawala wa kimichezo kwa walimu na viongozi wa michezo wa wilaya za Tandahimba, Mtwara vijijini na Mtwara manispaa.

Alisema mkoa huo unamchango mkubwa sana katika michezo hapa nchini hasa katika mchezo wa mpira wa miguu, kutokana na kuwa na wanamichezo mahiri miaka ya nyuma ambao walikua ni tegemeo kubwa kwa taifa.

“Kuna akina mzee Chuma, Mahadhi wote wametokea hapahapa..vijana wa karibuni kama akina Mmachinga (Mohamed Husein) wote hao, mi nafikiri mkoa wa Mtwara viongozi wa serikali wauangalie kwa jicho la huruma kuweza kurudisha michezo, mkoa huu una dhamana sana kwa michezo na tuna wanamichezo wengi tub ado tuwafuatilie.” Alisema Bayi.

Aidha, alisema mafunzo waliyoyatoa kwa muda wa siku nne yatakuwa na msaada mkubwa sana kwa walimu na viongozi wa michezo wa wilaya na mkoa kwasababu wao ndio wameshika mpini wa michezo katika mkoa.

Alisema moja ya mambo waliofundishwa ni namna ya kutengeneza mikataba ya vyama vyao ambalo ni jambo muhimu sana kwa chama chochote cha michezo, kwa lengo la kuepuka kuendesha chama kiholela na kuyumbisha kanuni za mchezo husika.
Kwa upande wake, Idefonce Amlima, ambaye ni mmoja kati ya waliohudhuria kozi hiyo alisema imemsaidia kumpanua kimawazo na kumjenga katika kazi yake ya uwalimu wa mpira wa miguu, ambapo anatarajia kuwafikishia wanafunzi wake kile alichokipata kutoka kwa wakufunzi wa kozi hiyo kutoka TOC.

…………………MWISHO…………………

No comments: