Monday, June 22, 2015

Lukuvi: siko tayari kuona CCM ikiadhibiwa na wananchi kwa kudai fidia





Na Juma Mohamed, Mtwara.


WAZIRI wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, Mhe. Willium Lukuvi amesisitiza juu ya kulipwa fidia kwa wananchi wanaotoa ardhi zao na kusema kuwa hayupo tayari kuona serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiadhibiwa na wananchi ambao hawalipwi fidia zao stahiki baada ya kuchukuliwa maeneo yao wanayomiliki kihalali.

 Aliyasema hayo wiki iliyopita mkoani hapa na kuongeza kuwa hayupo tayari kuona taasisi yoyote au kiongozi yoyote anagombanisha wananchi na serikali, na atakaefanya hivyo hatakama itakuwa ni Taasisi ya Upimaji Viwanja (UTT) ambae ipo chini ya serikali, ataipinga na kutumia madaraka yake kuifuta kabisa katika shughuli ya biashara ya ardhi.

“Kwahiyo nimetoa waraka wangu unaosisitiza juu ya wajibu wa mtu yoyoyte anaechukua ardhi ya mtu kulipa fidia kabla ardhi ile haijachukuliwa..na fidia yenyewe imfanye huyu mwenye ardhi yake anaondoka huku anacheka, kama ni ardhi yake halali maana yake analipwa ardhi na vile vilivyopo ndani ya eneo lake..hii habari ya kunyang’anya watu kwanguvu halafu watu wananung’unika hawana pakusema, adhabu inakuja kwa serikali, na kwenye uchaguzi tena CCM inaadhibiwa huko, mimi hiyo sikubali..” aliongeza.


Aidha, alisema kuanzia Julai 1 mwaka huu gharama za upimaji viwanja kwa wananchi zitapungua kutoka shilingi laki nane kwa hekari moja mpaka kufikia laki tatu, kwa lengo la kuongeza kasi ya wananchi kumiliki hati kihalali  na kuongeza kuwa kodi watakayolipa kwa mwaka itapungua kutoka shilingi 1,000 mpaka shilingi 400.


Alisema wananchi wakimiliki ardhi kihalali kwa kuwa na hati, itasaidia kupunguza migogoro baina yao na serikali kwasababu ulinzi wa maeneo yao itakuwa ni majukumu yao wenyewe.

“Hali hii ya kuwa na ardhi na mashamba kiholela, bado serikali haitupi faida kwasababu hata sisi serikali haitupi mapato, mapato yetu yanatokana na wale tu ambao tumewamilikisha kihalali..kwahiyo kasi ya umilikishaji wa hati kwa viwanja na mashamba ni ndogo sana, ningeuliza hapa kwa mwaka mzima manispaa na halmashauri mumemilikisha mashamba mangapi kwa wananchi wa Mtwara mtaniambia hakuna..” alisema Lukuvi.

Alisema njia pekee ya kuwawezesha wananchi wa vijijini na kuwafanya waweze hata kwenda benki kuchukua mikopo ni kuwamilikisha hati za mashamba na viwanja ambazo ndio zitakuwa dhamana kwao.



…………………mwisho………………………………………….

No comments: