![]() |
Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Hawa Ghasia, akihutubia katika sherehe za ufunguzi wa wiki ya serikali za mitaa, katika viwanja vya Mashujaa mjini Mtwara. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
WAZIRI
wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Hawa Ghasia, amezitaka
mamlaka za serikali hizo kuanza mapema maandalizi ya mchakato wa kura ya
maoni ya katiba pendekezwa na uchaguzi mkuu, ili kuepukana na
changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita.
Akizungumza
wiki iliyopita mjini Mtwara katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya
serikali za mitaa katika viwanja vya mashujaa, ambayo kitaifa
yanafanyika mkoani humo, amesema mamlaka hizo zinatakiwa kudumisha hali
ya ulinzi na usalama ili wananchi waweze kushiriki katika mazingira ya
amani na utulivu.
Alisema maadhimisho hayo ya 11 yanafanyika
ikiwa ni baada ya kukamilika kwa uchaguzi katika ngazi za mitaa, vijiji
na vitongoji na kwamba kilichobaki sasa ni kujiandaa na uchaguzi mkuu wa
madiwani, wabunge na Rais mwezi Oktoba mwaka huu, bila kusahau mchakato
wa kura ya maoni ya katiba pendekezwa.
“Napenda nitumie fursa
hii tena kuziagiza mamlaka zote za serikali za mitaa nchini kufanya
yale yote yanayofanikisha mazoezi haya..nikisema hivyo nadhani
wakurugenzi mnanielewa na mnafahamu waliofanya vibaya katika uchaguzi wa
serikali za mitaa yaliyowakuta, japo siombei yatokee tena katika
uchaguzi mkuu.” Alitahadharisha.
Aidha, alizitaka halmashauri
zote ambazo bado hazijachangia maadhimisho hayo, kufanya hivyo kabla ya
Julai 1 mwaka huu ambapo ndio itakuwa kilele chake huku yakitarajiwa
kufungwa na waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo
Pinda.
“Taarifa nilizonazo ni kwamba zipo baadhi ya
halmashauri ambazo zinasuasua kuchangia maonyesho haya tangu miaka
iliyopita na hata ya mwaka huu..napenda kutoa kauli kwamba halmashauri
zote ambazo hazijachangia zihakikishe zinafanya hivyo kabla ya
julai 1, na hata zile ambazo hazijashiriki, mpaka kufikia tarehe hiyo
ziwe zimefika katika mji wa Mtwara.” Aliongeza.
Kwa upande
wake, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akizungumza kwa niaba ya
mkuu wa mkoa, Halima Dendego, alitaja miradi ya maendeleo inayotekelezwa
ndani ya mkoa ambapo ni pamoja na hospitali ya rufaa ya kanda ambayo
ujenzi wake umeshaanza na tayari serikali imeshatenga bajeti yake kwa
mwaka 2015/2016 ambayo ni sh. Bilioni 3 ili kuhakikisha ujenzi huo
unaendelea.
“Pia tuna mradi wa ujenzi wa reli ya mchuchuma
Luganga, Mbamba bay..yapo makampuni matano ambayo yanashirikiana na kwa
sasa bado wanaendelea na zoezi la upembuzi yakinifu.” Alieleza.
Naye,
katibu mkuu wa TAMISEMI, Juma A. Sagini, alisema madhumuni ya
maadhimisho hayo yenye kaulimbiu inayosema “Mwananchi pigia kura katiba
pendekezwa na chagua kiongozi bora kwa maendeleo endelevu baada ya 2015”
pamoja na mambo mengine, ni kutoa fursa
kwa wadau wa serikali za mitaa kutafakari shughuli mbalimbali
wanazozifanya kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya mamlaka zao na taifa
kwa ujumla.
……………………mwisho………………………………………..
No comments:
Post a Comment