Monday, June 29, 2015

CHADEMA: Gesi kuididimiza Mtwara katika umasikini.

 
Na Juma Mohamed, Mtwara.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema rasilimali ya gesi ilioko mkoani hapa inakwenda kuudidimiza zaidi mkoa huo katika lindi la umasikini kutokana na serikali kutokuwa na taarifa sahihi juu ya mapato na matumizi yatakayotokana na rasilimali hiyo.
Akizungumza wiki iliopita mkoani hapa katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Nkanaredi, naibu katibu mkuu wa chama hicho Visiwani Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema sababu nyingine ni kutokana na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuingia mikataba ya muda mrefu na wawekezaji.
“Hatuna kauli sio tu Wanamtwara, Watanzania hatuna kauli..na tutapiga kelele, tutabisha, tutatukana, tutaandamana, tutagoma mwisho wa siku mzungu anakuja na mkataba..mkishindwa kuzuiliwa na ‘field force’ wataleta askari wao wawazuie kwasababu wana mkataba.” Alisema.
Alisema serikali ya CCM ikotayari kurudi madarakani kwa gharama yoyote kwasababu ya kutaka kuendelea kunufaika na mikata walioingia na wawekezaji, ambapo alionya wananchi wanaodhani kuwa kuwarudisha madarakani viongozi wa CCM kutawasaidia juu ya kunufaika na rasilimali hiyo.
“Hakuna gesi hapa ya kuendelea kupatikana miaka mitano ijayo..lakini kitu tunachoweza kufanya Watanzania ni kudhibiti mikataba hii kabla ya gesi haijaanza kutoka kwa wingi, na njia pekee ya kudhibiti ni kuikataa CCM mwezi Oktoba, tupeni UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi) tukaizime mikataba ya kiovu..” aliongeza Mwalimu.
Awali akizungumza katika ukumbi wa chuo kikuu huria wakati wa kuwatunuku vyeti wanafunzi 34 wa chuo kikuu kishiriki cha SAUT tawi la Mtwara, ambao ni wanachama wa Taasisi ya Wanafunzi wanachama wa Chadema wa Vyuo Vikuu (CHASO), Mwalimu alisema, chama hicho sasa kinatumia mtindo wa kocha wa Chealsea Josee Mourinho wa kuwashambulia wapinzani wao CCM.
“Walizoea kutuonea onea hawa kwasababu tulikuwa tunatumia ‘formation ya 4,4,2 kwamba viongozi wa chama ndio 4 yakwanza, 4 ya katikati ndio ya wabunge alafu mbele kule yuko sijui dkt Silaa na mwenyekiti Mbowe, tumebadilisha sasaivi..sasaivi tunatumia ‘Mourinho style’, tumetoa washambuliaji tumejaza viungo, wakiangalia namba sita wanamuona Prof. Lipumba, pale katikati wanamuona Mbatia, ukigeuka huku unamuona Mnyika, ukisogea mbele unamuona Mwalimu..yani tunawapiga ‘Mourinho style’ ndiomana wameacha kufurukuta wako kimya..” alisema.
Kwa upande wake, katibu wa balaza la vijana la chama hicho (BAVICHA) Edward Simbei, alisema CCM wanachokifanya kwa sasa hata hawajielewi na kusema kuwa ni sawa na kuruka sarakasi wakati wamevaa taulo.
“ Hakiamungu tutawipiga katafunua hawajawahi kuona..tumejipanga mwaka huu kuigawanya nchi hii katika vipande vinne, kutakuwa na kikosi cha anga, kikosi cha miguu, kutakuwa na kikosi cha kamati ya ushindi..” alisema Simbei.

………………….mwisho…………………………………..

No comments: