Thursday, July 2, 2015

Ngeleja awataka wananchi kumpima kwa mambo 15.

 

Na Juma Mohamed, Mtwara.

MBUNGE wa Sengerema Mhe. Willium Ngeleja amewataka makada wenzie wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Watanzania kwa ujumla, wampime kwa mambo 15 likiwemo la ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Akizungumza wilayani Masasi alikokwenda kuomba wadhamini na kufanikiwa kuwapata 65, Ngeleja alisema mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na kusaidia taifa kuokoa kiasi cha zaidi ya dola za kimarekani trilioni 1.6, ulibuniwa kipindi ambacho yeye alikuwa waziri wa nishati na madini.
Alisema jambo lingine ambalo Watanzania wanapaswa kumpima nalo ni kudhibiti umeme wa mgao, ambapo kipindi ambacho alikabidhiwa wizara hiyo mwaka 2008 kulikuwa na matukio ya mgao wa umeme kwasababu ya miundombinu mibovu katika shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
“Mimi niliukuta mgao katikati kabisa, lakini baadae Novemba 2011 mimi ndio niliofanikiwa kudhibiti mgao wa umeme Tanzania..kwahiyo watanzania wenzangu kupitia CCM nawaomba wanipime kwa kutumia hicho kigezo.” Alisema.
Aliongeza kuwa, miradi mingi ya umeme vijijini inayotekelezwa sasaivi ilibuniwa katika kipindi ambacho alikuwa akiiongoza wizara ya nishati na madini ambapo ilipitishwa katika bajeti za mwaka 2008 mpaka ya 2012 na yeye ndio aliwasilisha bungeni bajeti hizo.
“Kumbukumbu zinaonyesha kwamba mimi nikiwa waziri wa nishati na madini, wizara hiyo na taasisi zake, kwamujibu wa mkaguzi na mdhibti mkuu wa hesabu za serikali (CAG), zilikuwa zinafanya vizuri na hatimae tulikuwa tunapata hati safi..maana yake tuliisimamia vizuri wizara na taasisi zake..” aliongeza.
Aliendelea kusisitiza vipaumbele vyake muhimu ambavyo ataanza navyo iwapo atafanikiwa kuingia ikulu kuwa ni kuimarisha uchumi, ambapo aliweka msisitizo katika sekta ya kilimo, utawala bora alitaja kuwa ni kipaumbele cha pili hasa katika jitihada za kupiga vita rushwa, ufisadi na mmomonyoko wa maadili.
Vingine ni kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo za maji, elimu na afya ambavyo vitatokana na kuimarika kwa uchumi huku uimarishaji wa miundombinu kikiwa ni kipaumbele chake cha nne.

…………………..mwisho…………………………………….

No comments: