Thursday, July 2, 2015

Ghasia: Halmashauri ziache kuwa tegemezi



Na Juma Mohamed, Mtwara.

Serikali imezitaka halmashauri kuacha tabia ya kutegemea fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na badala yake zijiendeshe zenyewe kwa kubuni vyanzo vya mapato .
Hayo yamezungumzwa jana mjini Mtwara na waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Hawa Ghasia, katika ufunguzi wa kongamano la  utekelezaji wa ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya serikali za mitaa ambayo kilele chake ni Julai 1 mwaka huu.
Alisema, halmashauri zinapaswa kujenga masoko na vituo vingine vya biashara na kuacha kutegemea pesa zinazotokana na ktoza ushuru, kodi na faini, kwa kufanya hivyo watafanikiwa kupata mapato mengine ya ziada  ya kuweza kuendesha miradi mbalimbali.
“Serikali ikichelewa kupeleka pesa kidogo utakuta ni malalamiko malalamiko, kwasababu wenyewe hawakusanyi..lakini pia tunazihamasisha halmashauri badala ya kutegemea ushuru, kodi, faini..sasaivi wabadilike waanze kuwa na vitega uchumi, wajenge masoko, vituo vya kibiashara ambavyo vitawawezesha kupata mapato mengine zaidi ya yale ambayo walikuwa wanategemea..” alisema.
Aliongeza, “Kazi ya serikali kuu ni kutunga sera na kusimamia pamoja na kuweka viwango, lakini ikumbukwe serikali za mitaa kazi yake ni kutekeleza kwani zipo karibu na wananchi kwahiyo mwanachi wa kawaida akilalamika moja kwa moja analalamnikia mamlaka za serikali za mitaa.”
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Jumuia ya Umoja wa Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) na Meya wa jiji la Dar es Salaam, Didas Mwasaburi, amesema serikali iwapo itaendelea na utaratibu wake wa kuchelewesha fedha za miradi, itafika kipindi halmashauri zitakufa.
“Hizi halmashauri zisipoweza kujikwamua, kwa maana ya serikali kuu kuleta fedha kwa wakati na za kutosha na rasilimali zingine kama vile rasilimali watu na vitendea kazi, hizi halmashauri zitafikia ukomo wake..zitafikia mahala ambapo haziwezi kujiendesha zenyewe, haziwezi kutoa huduma stahiki na hatima yake ni kwamba zitaparalaizi au kwa lugha nyingine zitakufa..”

……………………….mwisho………………………………………………..

No comments: