Sunday, May 29, 2016

Viongozi MTWAREFA washinda uchaguzi kwa asilimia 100.


Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), Athuman Kambi (katikati) akitoa neno la shukrani baada ya kumalizika kwa uchaguzi. kulia ni makamu mwenyekiti, Edward Kapwapwa.




Mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF na mmoja wa wakurugenzi wa timu ya Ndanda Fc ya Mtwara, Mohamed Remtula (Mamu) akipiga kura.


Wajumbe wakipiga kura.


Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya MTWAREFA Hussein kingi akiwahusia viongozi wapya chama hicho


Athuman Kambi akivishwa taji na swahiba wake Ally Mchokoleka baada ya kushinda uchaguzi


Kizito Mbano akivishwa taji kwa ushindi wa katibu wa MTWAREFA




Katibu msaidizi Baraka Jamali akiwa na viongozi wenzake wa MTWAREFA baada ya kumalizika uchaguzi


Edward Kapwapwa akivishwa taji baada ya kuitetea nafasi yake ya makamu mwenyekiti.






Baadhi ya viongozi wapya wa MTWAREFA wakiwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi.




Na Juma Mohamed, Masasi.

CHAMA cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA) kimefanikiwa kupata viongozi wapya kufuatia kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa chama hicho uliofanyika leo wilayani Masasi mkoani hapa.
Uchaguzi huo uliohudhuriwa na wajumbe 30 wa mkutano mkuu, ulitanguliwa na mkutano mkuu ambao uliendeshwa kwa muda mfupi na mwenyekiti wake Athumani Kambi ambaye baadaye alijiuzulu kwa ajili ya kugombea upya nafasi yake.
Jumla ya wagombea 14 walikuwa wakiwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo ambapo wagombea watano walikuwa wakiwania nafasi tatu za ujumbe wa mkutano mkuu wa MTWAREFA huku nafasi za mweka hazina, mwakilishi wa vilabu na mjumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zikiwa na mgombea mmoja kila nafasi ambao walipigiwa kura za ndiyo na hapama.

Atuman Kambi akivishwa taji baada ya kufanikiwa kuitetea nafasi yake ya mwenyekiti wa MTWAREFA.



Nafasi nyingine ambazo zilikuwa na mgombea mmoja ni katibu mkuu, makamu mwenyekiti na mwenyekiti huku nafasi ya katibu mkuu msaidizi ikiwaniwa na watu watatu ambao ni Baraka Jamali, David Paul na Abasi Mkuwaje.
Katika matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na  mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya MTWAREFA, Hussein Kingi, yalimfanya Athuman Kambi kufanikiwa kuitetea nafasi yake kwa kupata ushindi wa kishindo wa asilimia 100 baada ya kupigiwa kura za NDIYO na wajumbe wote 30 wa mkutano huo.
Aidha, Edward Kapwapwa pia amefanikiwa kuitetea nafasi yake ya makamu mwenyekiti kwa kupata kura za NDIYO 29 kati ya 30 za wajumbe wote huku kura moja ndio ambayo ilikuwa ya HAPANA.
Viongozi wengine waliochaguliwa kihalali kupitia uchaguzi huo watakaoongoza kwa muda wa miaka mine ni Kizito Mbano ambaye amepata nafasi ya katibu mkuu wa chama kwa kura za NDIO 29, Baraka Jamali anayekuwa katibu mkuu msaidizi kwa kupata kura 16 na kuwashinda wapinzani wake David Paul kura 9 na Abasi Mkuwaje kura 5.

Baraka Jamali akivishwa taji kwa ushindi



Nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF imeendelea kusalia kwa Mohamed Remtula (Mamu) ambaye amepigiwa kura za NDIO 29, huku nafasi ya mwakilishi wa vilabu ikibakia kuwa kwa Yahaya Jamali aliyeitetea kwa kupata ushindi wa asilimia 100 kwa kupata kura za NDIO 30 na Thomasi Mhanga akipata nafasi ya mweka hazina baada ya kupewa kura 21 na NDIO huku kura 9 zikimkataa.
Nafasi tatu za wajumbe wa MTWAREFA zilizokuwa zikiwaniwa na wagombea watano na idadi ya kura zao kwenye mabano, zilienda kwa Hamisi Kangomba (25), Fredrick Nachinuka (24) na Keneth Kilinga (21).

Wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa MTWAREFA wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa wilaya ya Masasi, Bernad Nduta baada ya kuwafungulia mkutano huo.



No comments: