Tuesday, January 19, 2016

Tanesco Mtwara wakamata wezi wa umeme.


Mkazi wa kata ya Chikongola manispaa ya Mtwara Mikindani, Jema Hamisi, akipandishwa kwenye gari la Tanesco kwa ajili ya kuelekea kituo cha Polisi akiwa chini ya ulinzi wa askari baada ya nyumba anayoishi kubainika kuwa inatumia umeme wa wizi

Mmoja wa mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Mtwara akichunguza Mita ya Luku katika nyumba ya Hamisi Namwelenu, kata ya Chikongola, manispaa ya Mtwara baada ya kubaini kuwa wanatumia umeme wa wizi


Na Juma Mohamed, Mtwara.

SHIRIKA la Umeme Tanzinia (Tanesco) mkoani hapa limefanikiwa kumkamata Jema Khamisi, mkazi wa kata ya Chikongola manispaa ya Mtwara kutokana na kubaini kuwa anatumia umeme wa wizi kwa muda ambao haukuweza kubainika haraka.
Hatua hiyo imetokana na shirika hilo kupitia maofisa wake kuendesha oparesheni ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza kwa wateja wake, wakiambatana na Mhandisi wa shirika hilo mkoa wa Mtwara Daniel Kyando, iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akizungumza nyumbani kwa mteja huyo baada ya kubaini tukio hilo, Athuman Saidi ambaye ni fundi wa shirika hilo, alisema walibaini kuwa kuna wizi unafanyika katika nyumba hiyo baada ya kuona mita ya Luku imefunguliwa ambapo walipochunguza wakaona waya mmoja umetolewa katika sehemu yake na kufungwa katika sehemu nyingine.

Fundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Mtwara, akikata umeme katika nyumba ya Hamisi Namwelenu, mkazi wa kata ya Chikongola, manispaa ya Mtwara Mikindani, baada ya kubaini kuwa inatumia umeme wa wizi.


Alisema, kitendo hicho kinapelekea umeme kuingia kwenye nyumba moja kwa moja ambapo hata mita ikiwa imeishiwa salio la Luku bado umeme utapatikana pasipo malipo yoyote.
“Tulivyoiangalia ile mita yenyewe umeme iliisha lakini bado mteja ndani umeme anapata, hizi mita zetu za Luku umeme ukiisha zinajiandika ‘No Credit’ ikishajiandika hivyo inamaana Yule mteja hawezi kupata umeme mpaka aweke salio ndio umeme utawaka ndani..ila kwasababu yeye amechukua kabla ya mita ndio maana umeme bado unaendelea kuwaka.” Alisema.
Alisema, aina ya wizi uliofanywa katika nyumba hiyo inaonyesha umefanywa na mtu ambaye ana ujuzi wa masuala ya umeme kwasababu siku hizi kuna vyuo vingi ambavyo vinafundisha ufundi wa umeme na kupelekea mitaani kuwepo watu wenye taaluma hiyo.
Akitoa utetezi wake baada ya kukamatwa, Jema, ambaye katika nyumba hiyo anaishi na mume wake ambaye hata hivyo hakuweza kupatikana kwa madai kuwa alikuwa kwenye majukumu yake ya kila siku, alisema hajui lolote kwani toka wamefunga mita ya Luku hakuwahi kuingiza umeme na baadala yake jukumu hilo linatekelezwa na mume wake.
“Kwangu mimi jambo hili limenisikitisha na kunihuzunisha kwasababu mimi ni motto wa kike na sielewi lolote katika mchakato huu, yani kuelewa kwangu ni baada ya hao mafundi kufungua hapo na kunielekeza ndio hili suala nalijua liko hivi kwahiyo sielewi chochote na mimi..” alisema.
Hata hivyo juhudi za kumpata mume wake aliyemtaja kuwa ni Khamisi Namwelenu, hazikuweza kufanikiwa mara moja baada ya simu yake kuto patikana ndipo askari polisi waliombatana na maofisa wa Tanesco kuamua kumkamata mama huyo aliyekutwa na mototo mdogo na kumfikisha kituoni.

Mhandisi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoa wa Mtwara, Daniel Kyando, akimhoji mkazi wa kata ya Chikongola Jema Hamisi, ambaye nyumba anayoishi inayomilikiwa na Hamisi Namwelenu ilibainika kuwa inatumia umeme wa wizi.


Kwa upande wake, Mhandisi wa mkoa, Daniel Kyando, alisema kwamujibu wa sheria za nchi, kitendo hichi ni kosa kisheria na kwamba kwa taratibu za Tanesco muhusika anapaswa kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
“Na taratibu zetu, tutakukatia umeme na taratibu zingine za kisheria zitafuata ikiwa ni pamoja na kukufikisha mahakamani..na ndio maana leo tuko na vyombo vya habari hapa waone kinachoendelea pamoja na askari ambao watatusaidia wewe kukufikisha mahakamani, na hili liwe fundisho kwa watu wengine katika mkoa wa Mtwara kufanya hivi..” alisema Kyando.
Katika hatua nyingine, Tanesco ilibaini tabia ya kujiunganishia umeme kinyume na taratibu iliyofanywa na Fatuma Athuman, mkazi wa kata ya Magomeni ambaye aliunganisha umeme katika maeneo mawili tofauti ambayo moja lilikua la biashara na lingine la makazi huku akitumia mita moja.
Maafisa wa shirika hilo waliamua kumkatia umeme katika maeneo yote na kumtaka alipe faini ambayo hata hivyo haikuelezwa moja kwa moja ni kiasi gani alichotakiwa kulipa.




No comments: