Tuesday, January 19, 2016

Watanzania watakiwa kuiombea Zanzibar


Askofu mkuu wa kanisa Katoliki jimbo la Mtwara, Mwashamu Titus Mdowe, akipeana mikono na mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego, wakati wa zoezi la kusimikwa kwa Askofu huyo lililofanyika jana mjini hapa katika ukumbi wa Kanisa hilo



Na Juma Mohamed, Mtwara.

WAUMINI wa dini nchini na Watanzania kwa ujumla wametakiwa kuliombea Taifa la Zanzibar ili liendelee kuwa la amani na utulivu kutokana na kukabiliwa na mvutano wa kisiasa baada ya Tume ya Uchaguzi visiwani humo kufuta matokeo ya Uchaguzi na kuamuru uchaguzi huo urudiwe baada ya siku 90.
Wito huo ulitolewa jana mkoani hapa na Askofu mkuu wa kanisa Katoliki Jimbo la Mwanza Mwasham Tadeus Rwaichi, katika sherehe za kumsimika Askofu mkuu wa jimbo katoliki la Mtwara, Mwasham Titus Mdowe, zilizofanyika katika ukumbi wa Kanisa Katoliki mjini hapa na kuhudhuriwa na waumini wa kikristo kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.

Maaskofu kutoka katika majimbo mbalimbali ya kanisa katoliki nchini Tanzania wakisali kwa pamoja na Askofu mkuu wa kanisa katoliki jimbo la Mtwara, Mwashamu Titus Mdowe, wakati wa zoezi la kusimikwa kwa Askofu huyo lililofanyika jana katika ukumbi wa kanisa hilo mjini hapa. 


“Mnaweza mkasema bara tumeshafanya uchaguzi wa Rais na ameshapatikana na maisha yanaendelea, lakini haiwezi kuwepo ndoa ambapo mmoja wa wanandowa ni mgonjwa mkasema kwamba sisi tuko sawa, hatuko sawa kama Watanzania, ningependa kuwaalika Watanzania wote tuiombee nchi yetu tudumishe umoja, upendo na amani ya Taifa hili kama familia ya Mungu.” Alisema na kuongeza:
“Nawaomba na kuwaasa wote wenye uwezo wachangie kupatia ufumbuzi wa kufaa swala linalorindima kule Zanzibar, tusifurahie wenzetu kuendelea kuvutana, tusifurahie wenzetu kuendelea kutishiana kuuwana, hilo sio jema Zanzibar pakiwaka na Bara hapatokuwa shwari..” aliongeza.

Waumini wa dini ya kikristo kutoka sehemu mbalimbali nchini waliohudhuria sherehe za kusimikwa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mtwara, Mwashamu Titus Mdowe, zilizofanyika jana mjini Mtwara katika ukumbi wa Kanisa hilo.


Kwa upande wake, Waziri wan chi ofisi ya waziri mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Jenister Mhagama, aliwataka waumini wa dini kuzidi kuliombea dua taifa la Tanzania chini ya serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ili liendelee kuwa la amani na utulivu kama ilivyokuwa katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015.
Alisema, suala la kulinda na kudumisha amani ya nchi ni la kila mmoja na kwamba viongozi wa dini watumie nguvu waliyonayo ya ushawishi kuubili amani na upendo ili kuzdi kuijengea heshima nchi.
“Tumetoka kumaliza uchaguzi mkuu, na kwa mara ya kwanza uchaguzi huo na hasa kwa upande wa Tanzania Bara umefanyika kwa amani haijapata kutokea, na uchaguzi huo umeweza kufikia hatua hii ni kwasababu ya waumini wa dini mbalimbali kupiga magoti na kumuomba Mungu kuliokoa Taifa letu..na uchaguzi huo ukamuweka madarakani Dkt. John Pombe Magufuli kupata nafasi ya kuongoza kwa miaka Mitano.” Alisema,
Alisema, Dkt. Magufuli amejipanga na amedhamiria kuleta mapinduzi ya kimaendeleo na zaidi ikiwa ni kupambana na mafisadi na wavunjaji wengine wa maadili kwa vitendo, hivyo anahitaji sana msaada was ala kutoka kwa waumini wa dini ili kufanikisha hadhma yake hiyo ambayo sio kazi rahisi kuweza kuifanikisha.

Askofu mkuu wa kanisa katoliki jimbo la Mtwara, Mwashamu  Titus Mdowe, akitoa neno la shukrani kwa waumini wa kikristo waliohudhuria katika sherehe za kusimikwa kwake na kuwa Askofu mkuu wa jimbo hilo zilizofanyika jana mjini Mtwara katika ukumbi wa kanisa katoliki


Kwa upande wake, Askofu Titus Mdowe, akizungumza mwishoni baada ya kusimikwa, aliwashukuru waumini wote waliohudhuria na kufanikisha kwa sherehe hizo na kuahidi kufanya kazi kwa juhudi zote na kwamba yeye ni kiongozi wa wote hivyo atafanya kazi na kila mtu.
Alisema, atahakikisha anakiendeleza vyema kijiti alichokipokea kutoka kwa Askofu mstaafu wa jimbo katoliki la Mtwara, Gabriel Mmole ambaye ametumikia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 31.


No comments: