Wachezaji wa Ndanda Fc wakishangilia bao katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City jana katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara. Ndanda walishinda kwa goli 4-1 |
Na Juma
Mohamed, Mtwara.
BAADA ya
kusota kwa muda mrefu bila kupata matokeo ya ushindi hatimae timu ya soka ya
Ndanda Fc ya mkoani hapa hapo jana ilifanikiwa kuondoa ‘gundu’ baada ya
kuisambaratisha Mbeya City ya jijini Mbeya kwa jumla ya magoli 4-1 katika
mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika katika uwanja wa
Nangwanda Sijaona mkoani hapa.
Katika mchezo
huo wa kukamilisha mzunguko wa kwanza wa michuano hiyo wenye michezo 15 ambao
ulichezeshwa na mwamuzi Endrew Shamba kutoka Pwani, iliwachukua Dakika 11 tu
Ndanda kuweza kuandika bao la kwanza lililokwamishwa na mshambuliaji Atupele
Green aliyeitendea haki pasi ya mlinzi wa kulia Hemed Khoja na kasha kuwatoka
walinzi wa City na kumchambua mlinda lango Juma Kaseja.
Dakika saba
badae, Mshambuliaji pacha wa Atupele, Omar Mponda alitumia vema makosa ya Juma
Kaseja aliyeshindwa kuutuliza mpira aliyerudishiwa na mlinzi wa City ambapo
Mponda aliyemzidi mbio Kaseja aliukwamisha wavuni na kuandika goli la pili kwa
Ndanda dakika ya 18.
Wachezaji wa Ndanda wakipongezana baada ya kufunga goli |
Hakika ilikuwa
ni siku njema kwa Mponda ambaye alikuwa na ukame wa mabao baada ya kukaa muda
mrefu bila kufunga, ambapo katika dakika ya 28 akicheza kwa ushirikiano mkubwa
na Atupele, alikwamisha tena wavuni na kuandika bao la Tatu kwa Wanakuchele
mara hii akipokea pasi kutoka kwa Atupele kutoka wing ya kulia.
Ndanda
walienda mapumzikko huku tayari wana akiba ya magoli 3-0 katika mchezo huo
ambao City walionekana kuuanza kwa kasi lakini walinzi na kipa Juma Kaseja
wakionekana kufanya makosa binafsi mengi sana kiasi cha kuwarahisishia kazi
washambuliaji wa Ndanda ambao leo walionekana kuwa moto wa kuotea mbali.
Kipindi cha
pili kilipoanza City walionekana kuja juu kutafuta mabao ya kusawazisha huku
Ndanda wakiilinda zaidi na kupanga mashambulizi ya kushtukiza langoni mwa City
ambao walifanikiwa kupata kona nyingi katika mchezo huo ambazo hazikuweza kuzaa
matunda.
City walifanikiwa
kupata goli la kufutia machozi kunako dakika ya 63 kufuatia kazi nzuri
iliyofanywa na mlinzi wa kulia John Jerome ambaye alimtengezea krosi nzuri
winga Joseph Mahundi ambaye alituliza mpiara na kumuangalia mlinda lango wa
Ndanda Jeremia Kisubi, na kasha kuukwamisha mpira wavuni na kuipatia City bao
pekee katika mchezo huo.
Mlizi wa kushoto wa Mbeya City, Hassan Mwasapile akiondoa hatari upande wa lango lao. |
Alikuwa ni
Atupele tena aliyeiandikia bao la Nne Ndanda na kuhitimisha karamu ya mabao
hapo jana, mara hii akiunganisha kwa shutu kali mpira uliochongwa kutokea
upande wa kushoto na mshambuliaji aliyekuwa ameingia muda mfupi kabla ya
kufungwa kwa bao hilo, Buruhani Halfan aliyechukua nafasi ya Omar Mponda.
Mchezo ulikuwa
ni wa kuvutia kutokana na viwango vilivyoonyeshwa na timu zote mbili na ufundi
kutoka kwa baadhi ya wachezaji, burudani zaidi ikiwa katikati ya uwanja lakini
ubabe pia ulichukuwa nafasi na kushuhudiwa kadi kadhaa za njano zikitoka huku
kadi nyekundu ikitolewa kwa Mlinzi Harouna Shamte baada ya kuonyeshwa kadi
mbili za njano.
Makocha wote
walizungumza baada ya mchezo huo ambapo kocha wa Mbeya City, Meja Mstaafu Abdul
Mingange, alisema matokeo ameyapokea na Ndanda walistaili kwasababu walicheza
vizuri zaidi yao.
“Mchezo
ulikuwa nzuri Ndanda walicheza vizuri nawapongeza wameshinda Ndanda..wachezaji
hawakuzidiwa bali ni mchezo tu, huu ndio mpira, anafungwa Barcelona sasa
unategemea Mbeya City wasifungwe!.. ‘This is Football’ tumefungwa tunajipanga
upya, mimi nasema Ndanda wamecheza vizuri wameshinda, sisemi mabeki wamefanyaje,
tuna points 14 sasa usilaumu mabeki ‘forward lines’ hapana huu ndio mpira.” Alisema.
Naye kocha
wa Ndanda, Amimu Mawazo ambaye alionekana kuwa mwenye furaha hii leo kwa
ushindi huo ambao ni wa pili msimu huu toka pale alipoilaza Coastal union ya
Tanga katika mchezo wa pili wa ligi katika uwanja huo kwa goli 1-0, alisema mwanzoni
kabla ya kuanza mchezo alikua na wasiwasi kufuatia kikosi chake kuwakosa wachezaji
Watano wa kikosi cha kwanza ambao walianza katika mchezo uliopita dhidi ya
Yanga ambao walipoteza kwa goli 1-0.
“Yani
kwakweli tunajipongeza sana, tulikuwa na uwezo wa kufunga goli zaidi ya Nne,
kwahiyo tunajipongeza na haya maeneo mengine ambayo yalikuwa na matatizo
tutakwenda kuyafanyia kazi na ‘next time, tutafanya vizuri zaidi.” Alisema.
Kwa upande
wa mashabiki wa Ndanda, walionekana kuwa na furaha hii leo huku wengine
wakimshangilia na kumpongeza kocha wao Amimu Mawazo ikiwa ni mchezo wa tatu
baada ya mashabiki hao kumshinikiza aliyekuwa kocha msaidizi wa timu hiyo
Ngawina Ngawina kuweza kuachia ngazi ya kumsaidia Mawazo.
Mwenyekiti
wa masahabiki hao, Mohamed Yusufu, aliwataka mashabiki wenzake waendelee
kushikamana kwa kuipa hamasa timu ambapo baadhi yao walianza kujiondoa kutokana
na mwenendo mbaya wa timu.
Naye, Shani
Christopher, alisema katika mchezo huo waamuzi walijitahidi kuchezesha bila
upendeleo na ndio sababu ya ushindi huo huku akidai kuwa katika mechi nyingine
zinazowakutanisha Ndanda na timu “kubwa” waamuzi watendi haki kwani wanaonyesha
upendeleo kwa timu hizo.
No comments:
Post a Comment