Na Juma
Mohamed, Mtwara.
SERIKALI
imeitaka Mamlaka ya Usimiamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuongeza makusanyo
yake kwa mwaka kutoka sh. Bilioni 600 ambazo walijipangia mpaka kufikia
Trilioni 1 ili fedha zisaidie kutatua matatizo ya wananchi, kuliko kuacha
zikipotea kwa uzembe wa watendaji.
Akizungumza
mkoani hapa baada ya kufanya ziara katika Bandari ya Mtwara, Waziri wa
Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Mhe. Makame Mbarawa, alisema serikali ya awamu
ya Tano imejikita katika kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji, na haitokuwa na
huruma kwa mtu yeyote atakayefanya kinyume na hayo.
Alisema,
serikali haitowaagiza wakusanye mapato ambayo hayapo isipokuwa ni yale
yaliyopangwa kukusanywa kwa mujibu wa sheria na ambaye hakubaliani na maagizo
hayo anapaswa kuondoka mwenyewe bila kungoja kufukuzwa.
“Sasa hivi
sitokufukuza kama nakuhamisha, nakufukuza moja kwa moja..utakwenda huko kwenye
chama cha wafanyakazi lakini naamini na chama hicho hakitomsaidia mtu ambaye hakusanyi
kodi, kitakua ni chama cha ajabu kinampigania mtu ambaye hataki kufanya kazi
yake ipasavyo, chama cha wafanyakazi najua kinatetea wananchi ambao
wanastaili.” Alisema.
Alisema,
bandarini kuna udhaifu mkubwa sana ambao serikali haiwezi kuuvumilia na kwamba
itaendelea kuchukua hatua mpaka pale itakapojiridhisha kuwa pamekaa vizuri hata
ikibidi kubakiza wafanyakazi wachache kuliko kuwanao wengi ambao hawaleti tija
inayohitajika.
Alisema, maamuzi
hayo hayatofanywa kwa kumuonea mtu bali kwa wale ambao hataweza kutimiza wajibu
wao kwani bandari inauwezo wa kukusanya mapato mengi zaidi na kuahidi kwa
bandari ya Mtwara kuwapa malengo yao ya makusanyo kwa mwaka.
“Leo mnasema
tunatumbua majipu, majipu hapa ni mapato tunataka..kama tukipata mapato
yanayotokana na sheria sisi wala hatuna shida na bandari, lakini hivi
inavyokwenda lazima tujipange, Bandari ya Mtwara nyie lazima tutawapa ‘Target’
mpya kwasababu tumemwambia mkurugenzi mkuu tunataka ‘Target’ ya Trillion 1
atutafutie ‘This yer’..” alisema Waziri na kuongeza:
“Sio yeye
mwenyewe ajipangie Bilioni 600, kwanza haiwezekani mwenyewe unajipangia
inatakiwa bosi wako ajue alafu akuambie kwamba mimi nataka ukusanye hiki, wewe
unahangaika na ile ‘Target’ lakini ilikuwa haifanyiki hivyo..serikali
imeshamwambia, mwaka unaokuja wa fedha atupatie Trilioni 1 sasa kama hakupata
atatueleza kwamba nimeshindwa kukusanya kwasababu hizi..” aliongeza.
Kwa upande
wake, meneja wa Bandari ya Mtwara, Prosper Kimaro, alisema miongoni mwa mipango
waliojiwekea ni kuongeza Gati 4 katika Bandari hiyo ambapo kwa kuanzia wataanza
kwa ujenzi wa Gati moja ambayo tayari mamlaka imeshaamua na ujenzi wake
utatumia fedha za ndani.
Alisema
tayari tebda kwa ajili ya ujenzi wa Gati hilo ilishatangazwa na ilishafunguliwa
ambapo baada ya kukamilika ujenzi huo ndipo mchakato kwa ajili ya Gati nyingine
Tatu utaanza.
No comments:
Post a Comment