Saturday, January 23, 2016

Ndanda waiadhibu Mshikamano..wavunja na kuweka Rekodi mpya.

Mfungaji wa magoli Matatu (Hat Trick), Atupele Green, katika mchezo wa kombe la Shirikisho, Azam Sports Federation Cup (FA) kati ya Ndanda na Mshikamano akipokea mpira uliotumika katika mchezo huo kama zawadi. (PICHA: MOSES MPUNGA)


Mashabiki wakifurahi na kupiga picha na Atupele Green, baada ya kufunga magoli Matatu (PICHA: MOSES MPUNGA)



Na Juma Mohamed, Mtwara.

BAADA ya kuivurumisha bila huruma Mbeya City Jumatano iliyopita katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara kwa jumla ya magoli 4-1, timu ya soka ya Ndanda Fc ya mkoani hapo jana iliendeleza wimbi la ushindi baada ya kuigaragaza Mshikamano ya jijini Dar es Salaam kwa magoli 5-0 katika mchezo wa mzunguko wa Tatu wa kombe la shirikisho la Azam Sports Federation Cup (FA) uliopigwa uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Wenyeji walionekana kuutawala mchezo kama ilivyokuwa katika mchezo uliopita, ambapo jana safu ya ushambuliaji ya Ndanda ilionekana kuwa hatari zaidi langoni mwa Mshikamano, ambapo mpachika mabao wao aliyesajiliwa msimu huu kutokea Kagera Sugar, Atupele Green aliendelea kuwadhihirishia Wanakuchele kuwa hawakufanya kosa kumsajili baada ya kurudi nyavuni mara Tatu huku William Lucian na nahodha Kigi Makasy wakihitimisha idadi hiyo ya 5-0.

Mfungaji wa magoli Matatu (Hat Trick), Atupele Green, katika mchezo wa kombe la Shirikisho, Azam Sports Federation Cup (FA) kati ya Ndanda na Mshikamano akipokea mpira uliotumika katika mchezo huo kama zawadi. (PICHA: MOSES MPUNGA)


Ushindi wa jana kwa Ndanda unaipa nafasi ya kusonga mbele katika mzunguko wa Nne wa michuano hiyo ambayo bingwa wake ndio atakayewakilisha nchi katika michuano ya kombe la Shirikisho Barani Afrika, ambapo hapo awali mshindi wa pili wa ligi kuu ndiyo alikuwa akishiriki.

Kocha wa Ndanda Fc, Amimu Mawazo, akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo. (PICHA: MOSES MPUNGA)


Kiwango cha Ndanda kimeonekana kuimarika kuanzia katika mchezo wao wa ligi kuu walipokutana na Yanga ambapo hata hivyo walipoteza kwa goli 1-0  kabla ya kuduwaza Mbeya City 4-1 huku hapo jana wakiichakaza bila huruma Mshikamano kwa 5-0 hivyo kuifanya iweke rekodi mpya ya ushindi mkubwa zaidi tangu ipande Ligi kuu msimu uliopita.
Kabla ya ushindi huo, ushindi mkubwa kwa ‘Wanakuchele’ ulikuwa ni wa magoli 4-1 ambapo waliupata msimu uliopita katika mechi yao ya kwanza ya ligi kuu katika uwanja wa Kambarage Shinyanga baada ya kuifunga Stand United, hivyo kupata tena ushindi kama huo msimu huu katika uwanja wa nyumbani dhidi ya Mbeya City.

Mashabiki wakifurahi na kupiga picha na Atupele Green, baada ya kufunga magoli Matatu (PICHA: MOSES MPUNGA)


Vilevile ushindi wa 5-0 unaifanya Ndanda kuivunja rekodi yake yenyewe ya ushindi wa 4-1 waliyoiweka Jumatano iliyopita dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Nangwanda Sijaona. Ikumbukwe kuwa kabla ya hapo Ndanda walikuwa hawajawahi kupata ushindi mkubwa kama huo katika uwanja wa Nyumbani.
Timu hiyo sasa imefikisha idadi ya magoli tisa katika michezo miwili huku yenyewe ikiruhusu goli moja pekee.


No comments: