Tuesday, May 31, 2016

Mtwara yawakusanya waathirika 156 wa Dawa za kulevya.





Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akimkabidhi Mwenge wa Uhuru mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, leo katika Tarafa ya Mpapura halmashauri ya wilaya ya Mtwara.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

Katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli za kupiga vita matumizi na biashara ya madawa ya kulevya nchini, mkoa wa Mtwara umefanikiwa kuwakusanya vijana 156 waathirika wa madawa hayo na kati ya hao, vijana 104 tayari wameunganishwa katika mpango wa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa huo, Ligula.
Hayo yameelezwa mkoani hapa jana na mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, baada ya kukabidhiwa Mwenge wa Uhuru na mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, katika Tarafa ya Mpapura, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, kabla ya kumkabidhi mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally.
“Mkoa wetu nao ni mwathirika wa madawa ya kulevya, tumeendelea kubanana, kupambana na kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanaoleta madawa kusambaza na watumiaji, mpaka leo nimesimama hapa kuna kesi 38 ziko kwenye mahakama mbalimbali lakini kuna vijana 156, na kati yahoo waathirika 104 tumewaunganisha katika mpango wa matibabu katika hospitali yetu ya mkoa ya Ligula..” alisema Dendego.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Halima Dendego akikumbatiana na mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally baada ya kumkabidhi Mwenge wa Uhuru.



Aidha, alisema ukiwa mkoani Mtwara, Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuzindua jumla ya miradi 40 katika halmashauri zote tisa na wilaya tano za mkoani humo yenye thamani ya sh. Bilioni 49.8 huku mchango wa wananchi ukiwa ni sh. Bilioni 1.8 katika fedha hizo.
Awali akizungumza kabla ya kukabidhi mwenge huo kwa mkuu wa mkoa wa Mtwara, mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi, alisema Mwenge huo ukiwa mkoani mwake uliweza kuzindua jumla ya miradi 48 yenye thamani ya sh. Bilioni 11.6, na kwamba kati ya fedha hizo, ruzuku kutoka serikalini zilikuwa ni sh. Bilioni 8.9 huku michango ya wananchi ikiwa ni sh. Bilioni 1.5.

Makabidhiano ya Mwenge Lindi na Mtwara

Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, akimkabidhi Mwenge wa Uhuru mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, leo katika Tarafa ya Mpapura, halmashauri ya wilaya ya Mtwara.



“Wahisani walituchangia sh. Milioni 911.4 halmashauri zilichangia sh. Milioni 305.7..Mhe. mkuu wa mkoa wa Mtwara, mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2016 zimebeba ujmbe usemao ‘Vijana ni Nguvu Kazi ya Taifa, Washirikishwe na Wawezeshwe, mkoa wa Lindi kwa kutambua umuhimu wa vijana unaendelea kwa kuwashirikisha katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuwapatia mikopo yenye ria nafuu, kutenga maeneo rasmi ya uzalishaji, kukuza masoko ya bidhaa zao na kuwapatia kazi mbalimbali..” alisema.
Naye, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally akizungumza baada ya kukabidhiwa Mwenge huo na mkuu wa mkoa wa Mtwara, alisema katika wilaya yake Mwenge utakimbizwa kwa siku mbili huku miradi 12 yenye thamani ya sh. Milioni 12 ikitarajiwa kuzinduliwa.


No comments: