Tuesday, March 8, 2016

Mtwara na Lindi watakiwa kujiandaa na kupanda kwa gharama za umeme.


Mmoja wa mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Mtwara, akitekeleza majukumu yake.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

WANANCHI wa mikoa ya Mtwara na Lindi wametakiwa kujiandaa na kupanda kwa gharama za kuvuta umeme majumbani (Service line) zitakazofikia kiasi cha sh. 177,000 kama maeneo mengine kutoka sh. 99,000 ya sasa.
Akizungumza juzi ofisini kwake, Mhandisi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Mtwara, Daniel Kyando, alisema punguzo hilo ilikua ni ofa maalumu ambayo ifikapo Machi 31 mwaka huu itafikia mwisho, hivyo watakohitaji kuunganishiwa umeme baada ya hapo watalipia gharama halisi.
“Na hii ilikuwa ikiongezeka kwasababu ulikuwa ni mpango wa mwaka mmoja toka mwaka 2012 na ilikuwa iishe mwaka 2013, lakini kutokana na ‘situation’ iliyokua Mtwara ikawa inaongezeka na wateja wengi Mtwara walikua bado hawajaunganishiwa umeme lakini sasa hivi maeneo yaliosambazwa umeme ni mengi sana kupitia miradi ya REA..” alisema.

Fundi


Alisema tangazo hilo ni kwa wananchi wote wa mikoa hiyo isipokua wale ambao wanapata punguzo kutokana na kupitiwa na mradi wa bomba la gesi asilia ambao wanalipia sh. 27,000, ambapo wao ofa yao itamalizika baada ya mradi huo kukamilika.
Aidha, aliwaondoa hofu wananchi ya Mtwara kutokana na hali ya kukatika kwa umeme mara kwa mara inayoendelea na kudai kuwa hali hiyo inatokana na marekebisho ya miundombinu ikiwamo nguzo pamoja na matengenezo makubwa ya mtambo mmoja ambao uliharibika kutokana na kuanguka kwa nguzo.

Mhandisi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Mtwara, Daniel Kyando, akimuhoji mkazi wa kata ya Chikongola ambaye nyumba anayeishi ilibainika kutumia umeme wa wizi.


“Hilo zoezi la kuzipitia nguzo hua linafanyika mara kwa mara lakini historia inaonesha kwamba suala la maintenesi kwenye mkoa wetu wa Mtwara kuna kipindi hapo nyuma halijafanyika kwa muda mrefu sana kwahiyo madhara yake ndio tunayaona sasa..unajua kama unakaa miaka miwili au mitatu hujabadilisha nguzo madhara yake ndio yanakuja sasa hivi nguzo nyingi zinaanguka kwa wakati mmoja..” alisema.
Alisema, wananchi wasiwe na wasiwasi kwani huduma hiyo itarejea katika hali yake ya kawaida ndani ya wiki hii kwasababu vifaa vilivyokuwa vikihitajika kwa ajili ya matengenezo ya mtambo huo tayari vimewasili.

No comments: