Tuesday, May 22, 2012

RAMADHAN KUMBELE ATWAA MKANDA WA UBINGWA WA TAIFA TPBO, AMCHAPA MOKIWA KWA KO RAUNDI YA PILI


Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azan, akimvisha mkanda wa Ubingwa Taifa (TPBO) Bondia Ramadhan Kumbele kutoka TMK, baada ya kumchapa mpinzani wake James Mokiwa wa Kinondoni, katika pambano lao la Raundi 10, ambalo lilimalizika katika raundi ya pili tu ya mchezo lililofanyika katika ukumbi wa Vijana Kinondoni jana. Kumbele alishinda kwa KO katika raundi ya pili.
Mbunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azan, akimwinua mkono juu Ramadhan Kumbele kutoka TMK, baada ya kumchapa mpinzani wake James Mokiwa wa Kinondoni, katika pambano lao la Raundi 10, ambalo lilimalizika katika raundi ya pili tu ya mchezo lililofanyika katika ukumbi wa Vijana Kinondoni jana. Kumbele alishinda kwa KO katika raundi ya pili.
Ramadhan Kumbele, akimpeleka chini mpinzani wake James Mokiwa katika raundi ya pili, Konde ambalo lilimfanya kushindwa kurejea na kuendelea na mchezo.
Mwamuzi akimwesabia Bondia James Mokiwa bila mafanikio, kwani Bondia huyo hakuweza kuinuka ili kuendelea na mchezo, jambo lililomfanya mwamuzi huyo kumpatia ushindi Kumbele.
Bondia Swedy Hassan (kushoto) akichapana na mpinzani wake, Mwaite Juma, katika pambano hilo, Swedy alishinda kwa KO,
Doi Miyeyusho, (kulia) akimwadhibu mpinzani wake, Jumanne Mtengela. Katika pambano hilo, Doi alishinda kwa TKO.
Watoto, Martin Richard na Yohana Thomas, wakionyeshana umwamba katika mapambano ya utangulizi.
Msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka Singida, Chungai,
Source: superdboxingcoach.blogspot.com

Kiungo Mpya Simba atamba

Mudde Musa
Sosthenes Nyoni
KIUNGO mpya wa Simba, Mudde Musa toka Uganda amesema amejiunga na Wekundu hao wa Msimbazi akiamini ni timu nzuri na yenye rekodi ya inayovutia.
Musa amesajiliwa na Simba akitoka klabu ya Sofapaka ya Kenya ambayo amachana nayo kufuatia kumalizika mkataba wake.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu toka Uganda, Musa alisema kujiunga kwake Simba kutamfungulia fursa ya kucheza soka la kulipwa Ulaya.

"Ni kweli, nimesaini kucheza Simba miaka miwili. Siku zote sipendi kurudi nyuma, hivyo nataka kutumia fursa hiyo kusonga mbele zaidi. Nikuambie jambo moja, unapotaka mafanikio wakati mwingine hutakiwi kuangalia fedha tu, Simba inashiriki michuano mikubwa mara nyingi hivyo ni sehemu nzuri ya mtu mwenye malengo kuweza kufikia matarajio," alisema Musa.

Musa alisema ili kuonyesha hakusajiliwa kimakosa atahakikisha anaisaidia Simba kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Kagame litakalofanyika baadaye mwezi ujao.

"Kwa sasa nipo timu ya taifa tunajiandaa na mechi dhidi ya Angola Juni 3, lakini nawaambia watu wa Simba wasiwe na hofu, Mungu akipenda wataniona Kagame," alisema kiungo huyo mkabaji.


Nsa Job kumwaga wino Coastal

Mshambuliaji wa Villa Squad iliyoshuka daraja, Nsa Job yuko kwenye hatua za mwisho kusaini mkataba wa kujiunga na Coastal Union ya Tanga. Awali Nsa aliyezichezea klabu za Yanga, Azam, Moro United na Villa Squad za jijini Dar es Salaam alidai anahitaji Sh20 milioni na mshahara wa Sh2 milioni kwa mwezi ili aweze kumwaga wino wa kujiunga na mabingwa hao wa ligi mwaka 1988.
Nahodha huyo wa Villa aliliambia Mwananchi jana jijini Dar es Salaam: "Tumefika kwenye hatua nzuri ya makubaliano ya kusaini mkataba na Coastal." Nsa aliyeweka rekodi nzuri ya kupachika bao kila mechi kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
"Siwezi kuweka wazi ni kiasi gani cha fedha tulichokubaliana na Coastal, ni siri yangu na uongozi huo." alisema Nsa aliyefunga mabao 11 kwenye Ligi Kuu iliyofika kikomo Mei 6, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Coastal, Ahmed Aurora alisema: "Ni kweli Nsa ni chaguo letu la kwanza, tumemfuatilia kwa ukaribu sana na kubaini ni aina ya mchezaji tunayemuhitaji kwenye kikosi chetu."

Viongozi Toto African lawamani

Sweetbert Lukonge

BENCHI la ufundi la timu ya soka ya Toto African ya jijini Mwanza, limeulalamikia uongozi wao kwa kushindwa kuimarisha uchumi wa klabu hiyo.

Hayo yamo kwenye repoti ya tathimini ya benchi hilo baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi.
Akizungumza jana mmoja wa viongozi wa benchi hilo ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema kuwa baada ya tathimini hiyo waligundua mambo mengi ambayo yamekuwa yakisabibisha timu hiyo kutofanya vizuri kila mwaka kwenye michuano ya Ligi Kuu.

Alisema kiufundi timu hiyo siyo mbaya lakini kinachoiangusha ni viongozi wake kutokuwa na mipango thabiti ya kuimarisha uchumi wa klabu hiyo.

"Kila mwaka ukata, klabu inamiliki jengo kubwa katika ya jiji la Mwanza lenye vumba zaidi ya 12 vya maduka ambavyo vinawapangaji. Kwa haraka haraka, kila mpangaji analipa siyo chini ya Sh500,000 kwa mwezi. Kwa hali hii, jengo pekee lina uwezo wa kuingizia timu yetu zaidi ya sh 72,000,000," alisema kiongozi huyo.

Alisema fedha hizo zingeweza kuisadia timu katika mambo mengi ikiwa pamoja na kulipa mishahara

‘Sophia, Ito wamechangia kipigo cha Twiga’

KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya wanawake Twiga Stars, Charles Mkwasa amesema kuwa kukosekana kwa wachezaji wake wawili, Sophia Mwasikili na Ito Mlezi, kumechangia kufungwa mabao 5-2 na timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Banyanabanyana’.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo juzi kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Mkwasa alisema kuwa timu yake ingeweza kufanya vizuri zaidi kwa kuwa wachezaji hao wana uwezo na wangeweza kuwakilisha vema.

Alisema safu yake ya ulinzi ilipwaya kutokana na kukosekana kwa beki Sophia aliyeko Uturuki kwa sasa na hivyo hakukua na beki wa kuziba pengo lake.

Nahodha huyo wa Twiga anatarajiwa kuwasili nchini kuungana na wenzake kabla ya safari ya Addis Ababa. Alisema kuwa mchezaji wa JKT, Ito Mlezi hakuwapo pia kutokana na kutopewa ruhusa kazini kwake na hivyo kuweka pengo katika timu hiyo.

Hata hivyo, Mkwasa alikiri kuwa kikosi chake kilielemewa katika mchezo huo na kuongeza kuwa kupitia mchezo huo amebaini makosa mbalimbali ambayo alisema kuwa yanatakiwa kufanyiwa kazi.

Katika mchezo huo wa kirafiki, Twiga Stars ilifungwa 5-2 ambapo wachezaji wa Twiga walipoteza mipira mbalimbali huku wengine walionesha kucheza bila ya kujiamini na wakiacha mipira ikiwapita.

Mbali na kubanwa katika kipindi cha kwanza Twiga ilianza kutoa matumaini baada ya kufunga mabao mawili na walipata nafasi zaidi ya matatu ambapo kama wangezitumia vizuri wangeweza kuwafurahisha mamia ya Watanzania waliofurika uwanjani hapo.

Hii ni mechi ya pili ya kimataifa Twiga inafungwa, wiki mbili zilizopita ilicheza na Zimbabwe na kufungwa mabao 4-1.

Timu hiyo ipo kwenye maandalizi ya mechi ya kuwania kucheza fainali za Kombe la mataifa Afrika dhidi ya Ethiopia mwishoni mwa mwezi huu.

Fainali hizo zimepangwa kufanyika Equatorial Guinea na Gabon Novemba

Ubingwa wa Super Falcon wapigwa fitna

Mohamed Said Abdullah, Zanzibar

BAADHI ya mashabiki wa soka kisiwani Pemba wamekitaka Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kuivua ubingwa timu ya Super Falcon baada ya kuitia kwenye makosa Kikwajuni kwa madai ya kuhusika na upangaji wa matokeo.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, mashabiki hao wamedai, adhabu dhidi ya Kikwajuni pekee bila Falcon, ni uonevu.

Kwa mujibu wa wadau hao, adhabu hiyo kwa Kikwajuni, mbinu ya viongozi kujisafisha kutokana na uendeshaji mbovu wa ligi ya msimu uliopita.

Wamedai kuwa madudu yaliyojitokeza ni baada ya ZFA-Pemba kushindwa kuwajibika kutokana na mizengwe iliyo kwenye chama hicho.

Khamis Mwinyi, alidai hata baadhi ya vifungu vilivyotumiwa na ZFA-Pemba kuiadhibu Kikwajuni, ni kutaka kujikosha kwa wadau dhidi ya utendaji wake.

Wameitaka ZFA kwenda mbali zaidi ya Kikwajuni kwa kuchukua hatua dhidi ya timu au watu walioshirikiana na Kikwajuni kupanga matokeo.

Meneja wa Jamhuri, Mohammed Abeid, aliishauri ZFA kuwa makini katika maamuzi yake, akiitaka kuzingatia sheria na kanuni.

ZFA Taifa Pemba iliishusha Kikwajuni madaraja mawili, kuifungia kucheza soka miaka miwili na kuitwanga faini kutokana na kukimbia mechi ya kumalizia msimu dhidi ya Jamhuri

DC bosi mpya RT

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), wamempa kura za kishindo Antony Mtaka kuwa Rais wa Shirikisho hilo akimbwaga Kanali mstaafu, Juma Ikangaa.
Katika nafasi hiyo, Mtaka ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mvomelo, Morogoro, alishinda kwa kura 50 dhidi ya 29 za Ikangaa, Katibu Mkuu wa zamani wa shirikisho hilo wakati huo ikijulikama kama TAAA.
Mtaka alipata kura hizo katika kura za marudio baada ya raundi ya kwanza kukosekana mshindi wa moja kwa moja miongoni mwa wagombea wanne waliokuwa wamejitosa katika nafasi hiyo kwa Ikangaa kupata kura 25 na Mtaka kura 36.

Waliochemkia raundi ya kwanza ni Francis John aliyeambulia kura 15 na Henry Nyiti aliyepata kura 7, hivyo raundi ya pili kushudia ushindani mkali kati ya Ikangaa na Mtaka.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo majira ya saa 3:30 usiku, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi huo, Henry Tandau, alisema kurudiwa kwa nafasi ya Rais na Katibu Mkuu, ilitokana na wagombea kushindwa kufikia asilimia iliyohitajika kwa mujibu wa kanuni.

Ushindani mwingine ulikuwa kwenye nafasi ya Katibu Mkuu iliyokuwa ikishindaniwa na watu wanne, akiwemo Suleiman Nyambui aliyekuwa akitetea, John Bayo, Zainab Mbiro na John Manyama, lakini Nyambui alishinda kwa kura 41 dhidi ya 38 za Bayo, katika raundi ya pili.
Wagombea wawili katika nafasi tofauti, Makamu wa Kwanza wa Rais (Utawala) ilikwenda kwa William Kallaghe, aliyekuwa mgombea pekee kwa kura 78.

Katika nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais (Ufundi), iliyokuwa ikiwaniwa na wagombea wawili, Dk. Hamad Ndee alishinda kwa kura 55, akimbwaga Herman Ndisa aliyepata kura 42.
Nafasi nyingine iliyokuwa na ushindani ni Katibu Mkuu Msaidizi , iliyokuwa ikiwaniwa na watu wanne, lakini Ombeni Zavalla akishinda kwa kura 40, Julius Murunya (32), Lucas Nkungu na Leonard Mandara, kila mmoja akipata tatu.

Nafasi ya Mweka Hazina ilikuwa na mgombea mmoja, Is- Haq Seleman, aliyepata ushindi wa kimbunga wa kura 78 kati ya 79. Mbali ya nafasi ya Rais na Katibu Mkuu, kivumbi kingine kilikuwa kwenye nafasi 10 za ujumbe wa shirikisho hilo, zilizokuwa zikiwaniwa na wanachama zaidi ya 30.

Hata hivyo, mhariri wa michezo wa gazeti la Tanzania Daima, Tullo Chambo, alifunga pazia la nafasi zilizokuwa zikiwania baada ya kupata kura 37, akiungana na Mwinga Mwanjala ( 53), Lwiza John (50), Peter Mwita ( 50) na Zakaria Gwandu ( 47).

Wajumbe wengine ni Meta Petro Bare ( 46), Zakaria Barie (45), Rehama Killo ( 42), Robert Kalyahe ( 41) na Christian Matembo (38).

No comments: