Friday, March 11, 2016

Bodi ya Korosho yajivunia mafanikio 2015/2016 kwa utooaji leseni.

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Juma.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

BODI ya Korosho Tanzania (CBT), imesema msimu huu uliomalizika mwezi Januari ulikuwa na mafanikio makubwa ukilinganisha na misimu mingine, ambapo kwa mara ya kwanza wamefanikiwa kutoa leseni kwa wanunuzi 120,000 kununua zao hilo.
Hayo yalielezwa jana mkoani hapa na mkurugenzi mkuu wa Bodi hiyo, Mfaume Juma, wakati akifanya mahojiano katika kituo kimoja cha redio kwa ajili ya kuelezea tahmini mzima ya zao hilo kwa msimu wa 2015/2016.
Alisema mafanikio mengine ambayo yameonekana katika msimu huu uliomalizika ni kuboreka kwa bei ambapo kwa mujibu wa mkutano wa wadau uliofanyika mwezi Agosti mwaka jana mkoani Lindi, bei dira ilikuwa ni sh. 1,200 huku malipo ya kwanza ikiwa ni sh. 900.
“Mkutano ule ambao unawakutanisha wadau mbalimbali wa zao la korosho wakiwamo wakulima wenyewe, ndio unapanga mikakati na hata bei dira kwa msimu husika..na msimu huu bei dira ilikuwa sh. 1,200 huku malipo ya kwanza yalikuwa ni sh. 900..na niseme tu kwamba kuna sehemu minada ya korosho iliuzwa mpaka sh. 2,900, hii ni kuonesha korosho msimu huu ulikuwa nzuri..” alisema.
Alisema, pamoja na kuwepo kwa changamoto kadhaa ikiwamo ya wanunuzi wasio rasmi maarufu kama Kangomba, lakini vyama vya msingi vilijitahidi kukusanya korosho kwa wingi na hata uuzaji ulikuwa mzuri kiasi cha kuwafanya wakulima wapate malipo yao vizuri na kwa wakati tofauti na misimu mingine.
Aidha, aliwataka wakullima kuachana na kuuza korosho kwa Kangomba ambao ni mfumo unaodidimiza kipato chao, kwani hata wao wanaonunua kwa mtindo huo wengine wanauza katika maghala yaleyale ya vyama vya msingi ambayo wakulima wangeweza kuuza korosho zao huko kwa bei nzuri tofauti na ile wanayoipata kwa Kangomba.
“Wakilma wanapaswa kupunguza au kuacha kuuza korosho kwa kangomba kwasababu wanadidimiza kipato chao..kwanza suala la kangomba ni uvunjifu wa sheria na mamlaka zote zinafaa kushirikiana katika kuhakikisha tunalimaliza hili..na mtu wa kwanza kushughulikia hili ni mkulima mwenyewe..” alisema.
Alisema mafanikio hayo katika msimu huu ni kutokana na sehemu kubwa zinazolima zao hilo kutekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani huku mkoa wa Pwani ukiwa umetekeleza kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kuwa nje mfumo huo kwa miaka kadhaa iliyopita.
Aliwaponngeza Mnazimmoja kupitia chama chao cha msingi kwa kuwa wawazi kwa wakulima wao na kujitahidi kutoa mchanganuo wa kila hatua inayoendelea katika mchakato wa kukusanya na kuuza korosho na kisha kubandika sehemu za wazi ili kila mkulima aone kiasi alichokusanya na kuuza.
Alivishauri vyama vya msingi kujitahidi kutokopa fedha benki jambo ambalo linapeleka kumlipa mkulima kidogokidogo na kumfanya hasione manufaa ya zao hilo na baadala yake wajitahidi kulipa fedha hzio kwa pamoja.







No comments: