Monday, May 16, 2016

Serikali Mtwara yashauriwa kushiriki kutafuta udhamini kwa Ndanda Fc.



Mwenyekiti wa makampuni ya Kilua Steel Company Group, Mohamed Kilua, (kushoto) akiongea na mmoja wa wakurugenzi wa timu ya Ndanda Fc na mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), Athumani Kambi, alipomtembelea nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili namna ya kuisadia timu ya Ndanda. (PICHA: JUMA MOHAMED)




Mwandishi wa Juma News, Juma Mohamed, akifanya mahojiano na Mohamed Kilua, nyumbani kwake Mikocheni Jijini Dar es Salaam.


Na Juma Mohamed.

SERIKALI mkoani hapa pamoja na wadau wake wa maendeleo wameshauriwa kushiriki ipasavyo katika kuhakikisha timu ya soka ya Ndanda Fc iliyopo ligi kuu ya Tanzania Bara inapata udhamini wa kudumu kuanzia msimu ujao wa mashindano 2016/2017.
Akizungumza na Nipashe nyumbani kwake jijini Dar es Salaam,             mwenyekiti wa makampuni ya Kilua Steel Company Group, Mohamed Kilua, alisema wawekezaji waliowekeza mkoani Mtwara wanao uwezo mkubwa wa kuidhamini timu hiyo lakini lazima uongozi wa mkoa ushiriki kujenga ushawishi kwao na sio kuacha jukumu hilo kwa viongozi wa Ndanda pekeyao.
“Unapozungumza uwekezaji ni lazima uongozi wa mkoa ushiriki, kuanzia mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, wakurugenzi, mameneja wa mabenki na wengine wa taasisi tofauti wawe kitu kimoja hilo linawezekana..kwasababu hivi vitu vina ‘level’ unapoongea wewe au nikiongea mimi ni tofauti na akiongea mkuu wa mkoa, yani kuna ‘level’ Fulani ni ya kusikika nay a kusikilizwa..” alisema Kilua.

Mohamed Kilua



Aidha, alisema timu hiyo inaweza kuwa timu tajiri pengine kuliko zote hapa nchini kwa kipindi cha mwaka mmoja iwapo mashabiki na wapenda maendeleo wa mkoa wa Mtwara wataamua kujitoa kwa dhati kuweza kuichangia sh. 20,000 kila siku kwa muda wa mwaka mmoja kwa kila mtu, ambapo kiasi hicho kitaifanya timu kumiliki zaidi ya sh. Bilioni 7 kwa mwaka.
Alisema, kiasi hicho cha fedha kinaweza kuifanya timu kuanzisha miradi mikubwa ambayo haigharimu pesa nyingi ikiwapo kujenga viwanda vya Viwembe, Pini na hata cha Plastiki ambacho alisema kinaweza kukagharimu sh. Bilioni 1.2 ujenzi wake.
“Kwahiyo mkishakuwa na miradi hiyo maana yake tayari kampuni inajiendesha yenyewe yani timu inabadilika inakuwa kampuni ambayo inajiendesha..kitu cha kwanza ni umoja, bila hivyo hamuwezi kutoka na umoja sio tu kwa maneno bali kuwe na mapenzi ya dhati..” alisema.

Kilua na Kambi


Kilua ambaye alifikia kuyaeleza hayo baada ya kutembelewa na uongozi wa timu ya Ndand fc ukiongozwa na mmoja wa wakurugenzi wake Athumani Kambi na katibu mtendaji, Seleman Kachele, alisema ugeni huo ulikuwa na lengo la kutaka kujadiliana kwa pamoja namna ya kuweza kuisaidia timu hiyo ambayo inakabiliwa na ukata wa kifedha, ili iweze kuanza msimu ujao ikiwa katika halinzuri.
Alisema, viongozi hao walimweleza mengi yanayoikabili timu na kuhitaji kusaidiwa ambapo aliyapokea na kuwaahidi kuwa atayafikisha katika uongozi wa makampuni yake ili waone namna ya kuweza kuwasaidia huku akiwaagiza kwenda kuaandaa mchanganuo wa kuomba udhamini (Proposal) na kisha wamkabidhi ili auwasilishe kwa uongozi wake.
Katibu wa Ndanda, Selemani Kachele, alimshukuru Kilua kwa mchango wa mawazo alioutoa na kuonesha utayari wa kushirikiana na viongozi wa Ndanda kutatua changamoto zinazowakabili na kusema kuwa anaimani yakitekelezwa ipasavyo basi msimu ujao timu itakuwa katika hali nzuri.
Timu ya Ndanda inashika nafasi ya Tisa katika msimamo wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kucheza mara 29 na kuweza kujikusanyia alama 34 baada ya kupata alama moja katika mchezo wake uliopita dhidi ya Mabingwa wapya wa ligi hiyo Yanga Sc kwa kutoa sare ya mabao 2-2 uwanja wa Taifa.
Itamaliza michezo yake ya ligi kuu msimu huu Mei 22 mwaka huu pale itakaposafiri kuwafuata Mbeya City katika mchezo unaotarajiwa kupigwa katika uwanja wa Sokine jijini Mbeya.

  

No comments: