Saturday, March 12, 2016

Watoa huduma watakiwa kutumia mifumo thabiti kwa wateja.



Katibu mtendaji wa baraza la ushauri la Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Goodluck Mmari, akiongea na waandishi wa habari katika kikao cha kuelezea maandalizi ya wiki ya maadhimisho ya siku ya haki za watumiaji duniani yatakayofanyika kitaifa Machi 15 mwaka huu mkoani Mtwara.


Katibu wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (CCC), Mary Shao, akifafanua jambo. 


Na Juma Mohamed, Mtwara.

WATOA huduma za nishati na maji, usafiri wa anga, huduma za mawasiliano na huduma za usafiri wa nchi kavu na majini, wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na mfumo thabiti wa utoaji taarifa zinazowahusu wateja wao kila wakati taarifa hizo zinapohitajika au kupatikana.
Akizungumza kwa niaba ya kaimu mwenyekiti wa Jukwaa la Watumiaji (TCF), Thomas Mnunguli, katibu mtendaji wa Baraza la Ushauri la EWURA, Goodluk Mmari, alisema wakati Tanzania ikielekea katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki za mtumiaji ambayo kilele chake ni Machi 15 mwaka huu, watoa huduma hizo wanapaswa kutafakari mifumo ya utoaji taarifa wanayoitumia na kujipima ili kuona kama inakidhi mahitaji ya sasa kwa wateja.
Alisema, pamoja na ukweli kuwa uhitaji wa taarifa unaongezeka miongoni mwa watumiaji siku hadi siku, bado utoaji taarifa kwa watoa huduma unakumbwa na changamoto nyingi zikiwamo kutotoa taarifa kabisa ikiwa ni pamoja na katizo la huduma na ucheleweshwaji au kuahirishwa kwa safari.

Mhandisi Goodluck Mmari

“Siku za hivi karibuni tumeshuhudia watoa huduma kwa mfano wanatangaza kuwepo kwa katizo la umeme kuanzia muda fulani hadi muda fulani lakini watoa huduma hawa hawazingatii kilichotolewa katika taarifa, mara nyingi utekelezaji wa taarifa hizo haufuatwi kabisa..au wakati mwingine hakuna taarifa kabisa inayotolewa.” Alisema.
Aidha, aliongeza kuwa, mbali na kuwa na mikataba ya huduma kwa wateja, watoa huduma wote wa huduma zinazodhibitiwa wanapaswa kuwa na mkakati wa mawasiliano ambao pamoja na mambo mengine, utaainisha njia zitakazotumiwa na watoa huduma katika utoaji wa taarifa kwa wadau wao ili kuharakisha usambaji wa taarifa kwa lengo la kuwafikia wahusika kwa haraka zaidi.
Aliwaasa wakazi wa manispaa ya Mtwara na vitongoji vyake hususani kwa makundi yatakayowakilisha wakazi wa mkoa huo, kushiriki kikamilifu katika semia za uelimishaji zilizoandaliwa kwa makundi hayo na kuwaomba kuwa mabalozi wazuri wa kusambaza elimu kwa watumiaji wanaotumia huduma na bidhaa zinazodhibitiwa.

Mary Shao

Kwa upande wake, katibu mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (CCC), Mary Shao, alisema Tanzania pamoja na nchi nyingine za Kiafrika ziko nyuma katika suala la kutekeleza haki za watumiaji kwasababu nchi nyingi baada ya uhuru, serikali ndio ilikuwa mtoa huduma huku sekta binafsi zilianza kuingia katika kutoa huduma mwishoni mwa miaka ya 80.
“Kuwepo kwa sekta binafsi ambazo pia ni mzuri kwa uchimi na pia zinaleta ‘product’ nyingi kwenye soko, kwa wale ambao wamezaliwa nyuma kidogo watakumbuka kuwa zamani simu ilikuwa ni TTCL pekeake, ukija kwenye basi utakuta UDA pekeake kwenye maji hivyo hivyo sasa inapokuwa watoa huduma ni wengi ‘product’ zinakua nyingi..” alisema.





No comments: