Saturday, March 12, 2016

TCRA watakiwa kutoa elimu ya simu bandia vijijini.



Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akiongea katika warsha ya kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa, iliyowalenga wanafunzi wa sekondari na baadhi ya wadau wengine, iliyoandaliwa na Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF)


Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa warsha ya kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa na wanafunzi wa sekondari, kutoka shule mbalimbali za manispaa ya Mtwara Mikindani.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

WADAU wa huduma za mawasiliano nchini ikiwamo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wametakiwa kufika vijijini kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kutambua simu bandia ambazo zitafikia mwisho wa matumizi yake mwezi June mwaka huu.
Wito huo ulitolewa juzi mkoani hapa na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, wakati wa ufunguzi wa warsha kwa wanafunzi sekondari na wadau wengine wa huduma zinazodhibitiwa, iliyoandaliwa na Jukwaa la watumiaji Tanzania (TCF), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki za mtumiaji itakayofanyika kitaifa Machi 15 mwaka huu mkoani Mtwara.
Alisema kutokana na maeneo mengi ya vijijini kuwa na miundombinu migumu kwa kuweza kufikiwa na vyombo vya habari ambavyo vinatumika kutoa elimu hiyo, wananchi wengi wanakosa kupata elimu na itawafanya waendelee kutumia na kununua simu hizo ambazo ni bandia.

Wanafunzi wa shule za sekondari za Manispaa ya Mtwara Mikindani, waliohudhuria warsha ya kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa, iliyoandaliwa na Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF)

“Kwahiyo mtakapoweza kufikisha elimu hii kwao mtatusaidia wananchi kuweza kujua uwepo wa hili naamini huko vijijini kuna simu ‘fake’ nyingi kuliko huku mjini..kutokana na hofu ya kushindwa kuziuza simu hizi bandia, nimeharifiwa kwamba sasa hivi zimeshushwa bei sana, na mnajua tumetoka kuuza korosho zetu kwahiyo wananchi wana hela na wanafanya ‘shopping’ ya vitu mbalimbali..” alisema.
Aliongeza kuwa, zoezi hilo litakapoanza wananchi wa vijijini ndio watakaoathirika zaidi kwasababu hela zao wanazipata kwa misimu, na simu ni miongoni mwa mahitaji muhimu kwa binadamu ambayo anakua na hamu ya kumiliki akipata hela.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally.

Kwa upande wake, katibu mtendaji wa baraza la ushauri kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Goodluck Mmari, alisema maadhimisho hayo yanafanyika kwa kuandaliwa kwa pamoja na mabaraza ya ushauri ya watumiaji wa taasisi za EWURA, Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Usafiri wa Nchikavu na Majini (SUMATRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Katibu mtendaji wa Baraza la Ushauri la Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Goodluck Mmari, akieleza juu ya maandalizi ya shughuli za maadhimisho ya siku ya haki za mtumiaji yatakayofanyika kitaifa mkoani Mtwara, Machi 15 mwaka huu.

Alisema, taasisi hizo kwa pamoja zilifikia makubaliano ya kufanya maadhimisho hayo mwaka huu mkoani Mtwara kwa kuzingatia sababu mbalimbali ikiwamo kuwapo kwa fursa nyingi za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa rasilimali za Mafuta na Gesi asilia zilizopelekea kujengwa kwa kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba na kiwanda cha Saruji cha Dangote.
“Mbali na hivi vitu ambavyo nimevitaja na ambavyo vinaonekana Mhe. Mgeni rasmi (Mkuu wa wilaya), kuna matarajio siku za usoni kwamba hapa Mtwara kitajengwa kiwanda cha Mbolea, na kitajengwa hapa kwasababu malighafi ya kiwanda cha Mbolea yanatokana na mabaki ya gesi..kuna matarajio ya siku za usoni kwamba itajengwa mitambo ya kuzalisha umeme hapa ambao utaingizwa kwenye gredi ya Taifa..” alisema.


  



No comments: