Monday, March 14, 2016

Mwanafunzi Mtwara Ufundi auwawa kwa Kiwembe.



Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe, akiongea na waandishi wa habari juu ya kifo cha mwanafunzi wa kidato cha Tatu wa shule ya sekondari ya Mtwara Ufundi, Tawfiq Hamisi, aliyeuawa kwa kukatwa na kiwembe na mwenzie.


Na Juma Mohamed.

MWANAFUNZI wa kidato cha Tatu katika shule ya sekondari ya Mtwara Ufundi mkoani hapa, Tawfiq Hamisi (17), amefariki dunia baada ya kukatwa na kiwembe katika mkono wake wa kulia na mwanafunzi mwenzake Issac Yohana (16).
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe, alisema kabla ya kifo hicho kulikuwa na ugonvi kati ya marehemu na mtuhumiwa ambaye ni Isssac anayedaiwa kuficha kiatu cha mwenzie ambapo baada ya mzozano akaamua kumkata na kiwembe mwnzie chini ya bega lake la kulia.
Alisema tukio hilo lilitokea usiku wa juzi kuamkia jana majira ya saa Tano usiku, ambapo marehemu alivuja damu nyingi kuanzia muda huo mpaka alfajiri alipochukuliwa na kukimbizwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula kwa ajili ya matibabu.
“Kwahiyo damu ilitoka nyingi sana usiku ule, lakini wale wanafunzi waliogopa kwenda kuuambia uongozi wa shule wakidhani kuwa ni jeraha la kawaida..lakini kadri muda ulivyoenda hali ya kijana ikawa inabadilika ndipo walipokwenda kutoa taarifa kwa uongozi majira ya saa 10 alfajiri kwamba mwenzetu hali yake sio nzuri kulitokea ugonvi..” alisema.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe.


Alisema, mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi kwa upelelezi zaidi huku akibainisha kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi kijana huyo mwenye umri wa miaka 16 ana haki ya kushitakiwa na kwamba zipo taratibu zinazopaswa kufanywa na jeshi hilo.
“Kwahiyo huyu kijana mshitakiwa Issac Yohana tunamshikilia, wote ni wanafunzi wa kidato cha Tatu, tunamshikilia kwa mauaji ya tukio hili na mwili wa marehemu unafanyiwa uchunguzi pale Ligula na tumeiachia shule kwa taratibu za kusafirishwa..” alisema.
Aliongeza kuwa marehemu ni mwenyeji wa mkoa wa Tanga huku mtuhumiwa ni mwenyeji wa wiayani Newala mkoani hapa, na kutoa wito kwa wanafunzi hasa wanaosoma katika shule za bweni kuepuka kuchukua maamuzi yenye kuleta madhara kama ilivyo kwa tukio hilo.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula, Dkt. Mdoe Mhuza, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya kupokelewa kwa mwili wa mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mtwara Ufundi.


Mganga mfawidhi wa hospitali ya Ligula, dkt. Mdoe Mhuza, alithibitisha kupokelewa kwa mwili wa marehemu majira ya saa 11 alfajiri na kudai kuwa bado uchunguzi zaidi unaendelea kwa ajili ya kuweza kubaini chanzo cha kifo chake.
“Kwa taarifa za awali ni kwamba ilionekana tu ana jeraha kwenye sehemu ya mkono, mpaka tutapofanya uchunguzi ndipo tutabaini nini kimepelekea mpka anapa umauti..Daktari wa zamu ambaye alikuwepo kwa zamu ya usiku (Dkt. Benardetha Mwambe) alisema kwamba walifika kwenye majira ya saa 11 alfajiri..” alisema.


No comments: