Tuesday, March 15, 2016

Wazee Nanyamba walia na kero za afya.



Mzee Chikomele Jabir, mkaazi wa halmashauri ya mji Nanyamba, akieleza changamoto zinazowakabili wazee katika huduma mbalimbali za kijamii.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

BAADHI ya wazee katika halmashauri ya mji Nanyamba, wamelalamikia kero za matibabu wanazozipata zinazotokana na kukosekana kwa kituo cha afya cha serikali na kuwalazimu kutumia gharama kubwa katika kituo cha Nanyamba kinachomilikiwa na shirika la kidini la Mkombozi.
Wakizungumza na Juma News, wazee hao wamesema wanapata changamoto katika kuhudumiwa wanapokwenda katika Zahanati ya Dinyecha kutokana na kukosa utaratibu nzuri wa kuwahudumia wazee na kujikuta wanatumia muda mrefu kupata huduma.
Chikomele Jabiri, ni mzee ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa Kisukari, alilalamikia ukosefu wa dawa za ugonjwa huo katika Zahanati ya Dinyecha iliyo katika Halmasahuri hiyo na kudai kuwa dawa hizo anazipata katika kituo cha afya cha Nanyamba kwa gharama kubwa.
“Natakiwa kwenda kupima pale sukari kila wiki, nikifiika kwanza naandika cheti kwa sh. 2,000 alafu nakwenda kupima damu kwa sh. 2,000 alafu nikisharudi huko naandikiwa dawa ambazo zinaweza kufikia sh. 8,000..sasa hiyo ukichanganya na 4,000 ni sh. 12,000 ndio nipate dawa za kutumia wiki moja zikiisha nakwenda tena mchezo ndio huo, yani wagonjwa sukari wengi inawanyonya sana..” alisema.
Alisema hali hiyo inawapa shida sana hasa wazee ambao uwezo wao wa kujitafutia kipato umekuwa mdogo wengi wao wakiishi kwa kuwa tegemezi ambapo hata katika Zahanati ya Dinyecha hakuna utaratibu mzuri wa kuwathamini wazee.

Mzee Chikomele Jabir

“Tukifika hospitali tunakuwa sawa na vijana hakuna cha kutusitiri kama sisi wazee..na kama hauna kijana wa kuchangamka unaweza kunyanyasika sana hospitalini..naiambia serikali iliyochukua majukumu yote ya nchi izidi kutuboreshea maana kama dawa zikija kwa wingi na utaratibu ule ukawa unafuatwa kisheria, mimi nafikiri mengine yatapungua..” alisema Hamisi Kamwendo.
Kamwendo pia alilalamikia shida ya maji ambayo imekuwa ni kero ya kipindi kirefu sasa kutokana na miradi mbalimbali ambayo pengine waliitegemea kutatua kero hiyo kukwama ukiwemo mradi wa AMREF ambao uliishia kusambaza matenki na mabomba ambayo hayajawahi kuwa na maji.
Alisema chanzo cha maji kinachotumika kusambaza maji katika halmashauri hiyo ni kimoja na hata hivyo kina changamoto ya kukosekana kwa nishati ya umeme kiasi cha kuifanya halmashari kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua mafuta ya kuwasha Jenereta ambalo haliwezi kutoa huduma mfululizo.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Oscar Ng’itu, alikiri kuwapo kwa changamoto hizo huku kuhusu afya akidai kuwa zinatokana na ukosefu wa kituo cha afya hali inayopelekea wananchi wake kulazimika kutumia gharama kubwa katika kupata matibabu katika Kituo cha afya cha Nanyamba ambacho sio cha serikali.

Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Nanyamba, Oscar Ng'itu, akifafanua masuala mbalimbali yakimaendeleo yaliyopo katika halmashauri yake.

Alisema kwa sasa wanafikiria namna ya kupunguza changamoto hiyo kwa kuingia ubia na shirika linalomiliki kituo hicho ili kiwe kituo teule amacho kitatoa huduma zake kwa gharama zile ambazo zinapatikana katika vituo vya afya vya serikali, huku wakiendelea na mpango wa kuwa na Zahanati ya halmasahuri.
Kuhusu changamoto wanazozipata wazee wanapokwenda kupata matibabu, alisema alishatoa maagizo katika vituo vya afya juu ya kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kuhudumia wazee, hivyo aliahidi kurudi tena kwa ajili ya kwenda kuhakiki na kujua kwanini maagizo yake hayatekelezwi.
Akizungumzia kero ya maji, Ng’itu alisema tatizo lililopo ni kwamba nishati inayotumika katika chanzo cha maji ni Jenereta ambalo halina uwezo wa kufanyakazi kwa muda mrefu kwasababu ya uhitaji wa mafuta.
Alisema halmashauri inalazimika kutumia gharama za kununua mafuta kaisi cha lita 200 kila siku kwa ajili ya huduma ya Jenereta ambazo hata hivyo pesa inayopatikana kwa mwezi kupitia mradi wa maji hazilingani na gharama zinazotumika kununua mafuta.
“Sasa hilo lilishaonwa nadhani kwanzia mwaka juzi wizara ya maji kwa kushirikiana na wizara ya nishati na madini waliweka utaratibu ili umeme uweze kufika kwenye kile chanzo..wiki moja iliyopita nilikutana na meneja wa Tanesco mkoa, ameniambia mchakato umefikia hatua za mwisho na stage iliobaki ni kwa mkandarasi kusaini mkataba ili aweze kwenda saiti..” alisema.
Mhandisi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)  mkoa wa Mtwara, Daniel Kyando, aliwaondoa hofu wakazi wa Nanyamba kwa kuwaambia kuwa sasa mambo yamekaa sawa na ndani ya wiki hii mkandarasi ataanza kazi ya kupeleka umeme katika chanzo hicho.


  

No comments: