Saturday, August 20, 2016

Serikali yashauriwa kutowazuia wahamiaji haramu.


Wahamiaji haramu, raia wa Ethiopia.



Baadhi ya maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Mtwara, wakiwa katika kikao cha pamoja na waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba.


Juma Mohamed, Mtwara.

Serikali imeshauriwa kuona umuhimu wa kutowazuia wahamaiaji haramu raia wa Ethiopia ambao wanapita nchini Tanzania kuelekea nchi jirani ili kuhepuka kutumia gharama kubwa katika kuwahudumia pamoja na kusababisha mrundikano katika magereza yaliyopo.
Ombi hilo lilitolewa mkoani Mtwara na naibu kamishina wa Uhamiaji, afisa uhamiaji mkoa wa Mtwara, Rose Mhagama, mbele ya waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba, na kudai kuwa serikali inapata hasara nyingine ya kuwasafirisha kwa kuwagharamia shilingi laki tatu kwa kila mmoja baada ya kumaliza azabu zao.

Afisa uhamiaji mkoa wa Mtwara, Rose Mhagama



“Lakini kama hiyo haitoshi watu hao kumuhudumia mtu mmoja anahitaji haki za binadamu, apewe chakula, malazi ‘sometimes’ matibabu..lakini baada ya mtuhumiwa kumaliza adhabu yake, inatulazimu sisi kama serikali kuwarudisha kwao, kichwa kimoja ni 300,000..” alisema Mhagama.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara, kamishina mwandamizi msaidizi wa polisi (SACP) Henry Mwaibambe, alieleza baadhi ya changamoto zinazolikabili jeshi la polisi kuwa ni pamoja na ukosefu wa magereza katika wilaya za Tandahimba na Nanyumbu.

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba, akiongea na watumishi na maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Mtwara.



Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba akizungumzia suala la wahamiaji haramu, alisema atakaa na wataalamu wake katika wizara ili kulijadili suala hilo huku akiunga mkono kuwa hakuna haja ya kuwazuia kuendelea na safari zao.
“Ni ‘logic’ kama wale watu tuhangaika nao wakati hawajaja kuishi kwetu, tunahangaika nao wao wanapita na kwamba kule wanakoenda wanawasubiri, kwahiyo nimeiona hiyo ‘logic’ nitaenda nitakaa na wataalumu kuweza kuichambua kuweza kuona njia nzuri ya kuifanya..” alisema.
Aidha, alisema katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa miundombinu ya majengo katika makazi ya askari pamoja na ukosefu wa magereza katika baadhi ya wilaya, serikali itatumia nguvu kazi iliyopo ikiwa ni pamoja wafungwa kwa ajili ya ujenzi huo.
Waziri huyo wa mambo ya ndani, amefanya ziara fupi ya kikazi mkoani Mtwara pamoja na kuongea na watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama.

No comments: