Meneja wa Wakala wa Vipimo mkoa wa Mtwara, Augustine Maziku, akitoa elimu ya Mizani kwa wakulima wa korosho katika kijiji cha Kitama ya Kwanza wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara. |
Juma Mohamed, Mtwara.
Mkoa wa
Mtwara ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kufanya vizuri katika kuzalisha
zao la korosho ambalo ndio zao kuu la biashara mkoani humo, huku matarajio ni
kuvuna tani laki nne ndani ya kipindi cha miaka Mitatu ijayo kutoka tani laki
moja na nusu za sasa.
Licha ya
kufanya vizuri zao hili, wakulima wanakabiliwa na changamoto kadhaa ambazo
zinahitaji kupatiwa utatuzi wa haraka, ikiwa ni pamoja na kukosa elimu ya
kuweza kusoma mizani zinazotumika kupima korosho zao.
Changamoto
hii kwa kiasi kikubwa inalalamikiwa na wakulima wa kijiji cha Kitama ya Kwanza,
ambao wanadai kuwa hali hiyo inawafanya wakose kuwa na uhakika na kudhani kama
wanaibiwa korosho zao baada ya kupimwa na makarani.
“Kwanza mimi
kama mimi yani sijui Mzani yani sijui kilo ngapi na hapa kilo ngapi hata
sijui..na hapa sasa hivi nilipo wala nilikua sijui kama kuna mkutano humu ndani
nimekurupushwa tu, kwahiyo sisi akina mama tumewekwa nyuma sana..” alisema
Jazila Machenje, ambaye ni mkulima katika kijiji cha Kitama.
Mmoja wa wakulima wa zao la korosho katika kijij cha Kitama ya Kwanza wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara akitoa maoni yake juu ya changamoto za Mizani. |
“Mali ile
ninapoipeleka ghalani kama Mzani siujui basi naona kama nadhurumiwa kwasababu
ninaweza nikazikadiria nyumbani kwamba hizi zinaweza zikafika kilo hamsini
nikija huku nikiambiwa kilo arobaini na tano kwakweli nakubali kwasababu
kwasababu si nimeshazipeleka sokoni lakini kwa moyo wangu siamini kama kweli
hizi hapa ni kilo hamsini..” aliongeza Said Samli.
Kwa kuona
umuhimu wa utatuzi wa changamoto hiyo, serikali kupitia kwa Wakala wa Vipimo
Nchini (WMA) iliamua kuendesha zoezi la kutoa elimu kwa wakulima hao kabla ya
kuanza kwa msimu mpya wa mauzo, pamoja na kuhakiki ubora wa Mizani.
Akiwa katika
zoezi la kutoa elimu hiyo, afisa vipimo mkuu wa WMA, Moses Ezekiel, alisema wamebaini
idadi kubwa ya wakulima ambao hawawezi kusoma Mizani pale walipowaambia wasome
Mizani ambapo walionekana kushindwa kutoa majibu sahihi.
“Tumejitahidi
kutoa elimu wapo wanaodai kwamba wanafahamu lakini unapomwambia kwamba pima
utaje kilo zako sahihi hawawezi..hilo tumeliona lipo na tunaendelea kutoa elimu
kwa Oparesheni maalumu ya wakala wa vipimo lakini pia kuhakiki Mizani hizi kwa
mtindo wa tofauti na pale nyuma..” alisema Moses.
Augustine Maziku akitoa elimu ya Mizani |
Kwa upande wake,
meneja wa WMA mkoa wa Mtwara, Augustine Maziku, alibainisha baadhi ya vifungu
vya sharia vinavyotafsiri adhabu wanazopaswa kuchukuliwa watu wanaokiuka sheria
ya vipimo.
“Sheria ya
vipimo sura namba 340 inabainisha vizuri adhabu ambazo mkosaji wa biashara ya
mizani anapaswa kuadhibiwa..kwa kosa la kwanza anapigwa faini ya sh. 10,000 kwa
kila kosa linalohusiana na kosa alilofanya au kifungo kisichozidi miaka
mitatu..” alisema.
Wadau wa zao
hilo wanatarajiwa kukutana Agosti 26 na 27 mwaka huu mjini Bagamoyo kujadili
masuala mbalimbali pamoja na kuzindua msimu mpya wa korosho.
No comments:
Post a Comment