Wednesday, April 27, 2016

Serikali Mtwara yasisitiza elimu kwa viongozi wa vijiji, kata na vitongoji.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akizungumza wakati wa maafali ya wahitimu wa mafunzo ya mradi wa elimu na demokrasia, yaliyoendeshwa na kituo cha demokrasia Tanzania na kufadhiliwa na serikali ya Norway.




Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akimkabidhi cheti mhitimu wa mafunzo ya mradi wa elimu na demokrasia.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

SERIKALI mkoani hapa imesema elimu ya ziada inahitajika kutolewa kwa viongozi katika ngazi za kata, vijiji na vitongoji ili kuwawezesha kutambua majukumu yao na mipaka ya kazi zao.
Hayo yamezungumzwa na mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally, wakati wa maafali ya wahitimu wa mafunzo ya mradi wa Elimu na Demokrasia, yaliyoendeshwa na kituo cha demokrasia Tanzania kwa ufadhili wa serikali ya Norway, ambapo alisema viongozi wengi wa ngazi za chini hawajui majukumu yao na kujikuta wanaingilia kazi za wenzao.
“Unakuta wakati mwingine kiongozi anakuwa hajui mipaka yake, anaweza kuwa ni Diwani akaenda kuingilia kazi za mkaguzi mkuu wa mahesabu ngazi ya kata, anaweza kuwa ni mwenyekiti wa kijiji akaenda kufanya kazi ya polisi..lakini yote hii ni kwasababu viongozi wale hawajui majukumu yao..” alisema.

Fatma Ally


Alisema, kazi za viongozi hao zinahitaji zaidi maelekezo kwasababu ni tofauti na kazi za kuajiriwa ambazo mtu anafanyiwa usaili baada ya kuomba nafasi anayohitaji akijua wazi kuwa ana ujuzi wa kutosha kwa kile alichokiomba.
 Alisema, pamoja na serikali ya wilaya yake kuwa imejipanga kutoa elimu kwa viongozi wa siasa katika ngazi hizo, bado kuna haja ya kupata msaada kutoka katika kituo hicho kwa ajili ya kutoa elimu hiyo ambayo itakuwa ni msaada mkubwa kwa madiwani, watendaji kata, vijiji na wenye viti wa vijiji.
Mratibu wa mradi huo ambao unatekelezwa katika halmashauri za wilaya ya Mtwara na ya mji wa Nanyamba ulioanza mwaka 2011, Lucy Agostino, alisema mradi huo unasimamiwa na makatibu wa wilaya kutoka katika vyama vinne vya siasa ambavyo ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Mapinduzi (CCM) na UDP.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akimkabidhi cheti mhitimu wa mafunzo ya mradi wa elimu na demokrasia.


Alisema, wahitimu hao 23 waliofanyiwa mahafali ni wahitimu wa awamu ya pili katika mradi huo ambao walianza kupata elimu hiyo mwaka 2012 baada ya wahitimu wa kwanza walioanza kupata elimu mwaka 2011 na kuhitimu mwaka 2014.
“Hawa wawezeshaji tulikuwa tunawapa mafunzo kuhusiana na dhana za demokrasia na utawala bora, mifumo ya serikali inavyofanya kazi nikimaanisha uongozi na uwakilishi katika ngazi za serikali za mitaa na hapa tulikuwa tunalenga kitongoji, kijiji, kata na bunge na pia walikuwa wanapata mafunzo kuhuisu dhana za jinsia.” Alisema.
Alisema, wawezeshaji hao walikwenda vijijini na kuanzisha vikundi kwa ajili ya kuendesha majadiliano kutokana na yale waliyofundishwa, ambapo yalionekana kuwa na manufaa kwa wanavikundi na wawezeshaji wenyewe ambao baadhi yao waliweza kupata nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akiwa katika katika picha ya pamoja na viongozi wa mradi wa elimu na demokrasia pamoja na wahitimu wa mafunzo ya mradi huo kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa.


Haji Machemba, ambaye ni mhitimu na mwezeshaji kutoka kata ya Nanyamba, alisema miongoni mwa faida alizozipata kupitia mafunzo hayo ni kuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa kupitia cha cha CUF pamoja na kikundi chake kutoa wajumbe saba katika serikali ya mtaa.
“Katika wajumbe hao, akina mama ni watatu na wanume wane..pia katika kikundi changu kumetokea mwanamama ambaye alijituma akajiingiza katika siasa na hivi ninavyozungumza ni diwani wa viti maalumu, kwahiyo ni mafanikio ambayo yametokea katika masomo haya..” alisema.





No comments: