Monday, April 25, 2016

Serikali Mtwara yalalamikia TFS tozo za mbao za madawati.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, akiongea na waandishi wa habari baada ya kukagua shughuli za uchongaji wa madawati zinazoendelea katika karakana ya halmashauri ya wilaya ya Mtwara.



Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Zacharia Nachoa, akiongea na waandishi wa habari katika karakana na uchongaji madawati ya halmashauri yake.



Fatma Ally.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

SERIKALI mkoani hapa imewataka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupunguza tozo katika mbao zinazosafirishwa kwenda sehemu mbalimbali kwa ajili ya kutengezea madawati kwa matumizi ya wananfunzi wa shule za msingi na sekondari.
Akizungumza baada ya kutembelea karakana ya kutengenezea madawati iliyopo katika manispaa ya Mtwara Mikindani, mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, alisema jitihada mbalimbali zinafanyika kwa ajili ya kutafuta fedha za kutatua tatizo hilo lakini pesa nyingi zinatumika katika kilipia tozo hizo.
“Kinachooneka wenzetu wa Maliasili bado hawajalitambua vizuri hili jambo la madawati, kwasababu kunakuwa na vikwazo vingi tunavyovipata kutoka kwao hata pale sheria zinapofuatwa unakuta bado tunakumbana na vikwazo..lakini kwasababu wote ni serikali sisi tumeshaanza taratibu za kufanya mazungumzo nao ili waweze kutupunguzia tozo zisizokuwa na msingi hasa kwenye hizi mbao za madawati..” alisema.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara Fatma Ally, akiwa amekaa katika dawati kwa ajili ya kujiridhisha juu ya ubora na kujua kama linakidhi kwa matumizi ya wanafunzi wa shule za msingi.


Aidha, alisema kasi ya utatuzi wa changamoto hiyo imekuwa kubwa kwa halmashauri zote tatu za wilaya yake na kutoa matumaini kuwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu tatizo hilo litakamilika kwa asilimia 100.
Alisema kwa upande wa wilaya ipo mikakati ya aina tatu tofauti ambayo imejiwekea, miongoni mwake ikiwa ni kuhakikisha kila halmasahuri inabadilisha matumizi ya fedha za miradi mbalimbali na mapato yake ya ndani, na kuelekeza fedha hizo katika shughuli za uchongaji wa madawati.
“Lakini pia tumekuwa na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao tumewashirikisha ambao tumewaomba misada na wanaendelea kuchangia, wapo ambao wameshangia na wapo ambao tumewaomba na wameahidi watachangia..lakini sehemu ya tatu ni mfuko wa mkuu wa wilaya ambao tumeanzisha kampeni inaitwa Haba na haba, hii moja kwa moja inahusisha jamii na wadau ambao wapo mkoa wa Mtwara..” alisema.

Mafundi wanaochonga madawati ya halmashauri ya wilaya ya Mtwara.


Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Zacharia Nachoa, alizitaka jamii kuunga mkono jitihada hizo zinazofanywa na viongozi wao za kutatua changamoto hiyo huku akiwapongeza wananchi wa tarafa ya Ziwani ambao kupitia kata zao wamehamasika kwa kiasi kikubwa kuchangia kwa hiyari utatuzi wa tatizo hilo.
Salumu Juma, mkazi wa manispaa ya Mtwara, aliipongeza serikali ya wilaya na mkoa kwa ujumla kwa jitihada za dhati wanazozifanya katika kuhakikisha wanawaokoa wanafunzi kutoka katika adha ya kukaa chini.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Zacharia Nachoa, akiongea na waandishi wa habari katika karakana na uchongaji madawati ya halmashauri yake.


“Mazingira ya elimu yalikuwa ni magumu, kwahiyo sasa hivi kama serikali inachukua upeo huu wa kuweza kunufaisha elimu kwa wakazi wake wa Mtwara sisi tunashukuru na tunaomba waendelee hivihivi wawe na moyo wakibinadamu watusaidie hivi kama wanavyotusaidia, na wanavyovifanya vinaonekana na hii ndio serikali ambayo sisi tulikuwa tunaihitaji..” alisema.

Mafundi wakiwa kazini




No comments: