Monday, July 9, 2012

AZAM WATINGA FAINALI ZANZIBAR, SIMBA WANALO KWA ALL STARS USIKU HUU

Wachezaji wa Azam (Picha kutoka maktaba)

 
MABAO mawili ya mshambujliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Herman Tcheche, jioni hii yametosha kuivusha Azam FC hadi fainali ya Kombe la Urafiki, baada ya kuwafunga mabingwa wa Zanzibar, Super Falcon 2-0 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Tcheche alifunga bao la kwanza dakika ya 67, akiunganisha krosi ya Hamisi Mcha wakati bao la pili, alifunga kwa penalti, dakika ya 77, baada ya Samir Haji Nuhu kuangushwa kwenye eneo kla hatari na Samir Said dakika ya 77.
Kwa matokeo hayo, Azam inasubiri mshindi wa mechi kati ya Simba SC na Zanzibar All Stars, mechi inayoanza saa 2:00 usiku huu Uwanja wa Amaan kucheza naye fainali keshokutwa.
Katika mechi hiyo, Azam ilipata pigo dakika ya 54, baada ya mshambuliaji wake Gaudence Exavery Mwakimba kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 54 kwa kumpiga kiwiko Abdul Ally.
Katika mechi yake ya mwisho ya Kundi A, Simba iliifunga kwa taabu Karume Boys 1-0, bao pekee la mshambuliaji wake Mzambia, Felix Mumba Sunzu Jr, wakati Azam iliifunga Mafunzo 3-2.
Kuna uwezekano mkubwa Simba na Azam zikakutana katika Fainali Jumatano, kwani Wekundu wa Msimbazi, ambao ni mabingwa wa Tanzania Bara, wanapewa nafasi kubwa ya kushinda mechi yao hiyo, ingawa pia haitarajiwi kuwa kazi nyepesi kwani hata nyota wa Zanzibar nao ni wazuri.
Kikosi cha Azam, inayonolewa na Muingereza Stewart Hall, kilikuwa: Deo Munishi ‘Dida’, Samir Hajji Nuhu, Ibrahim Shikanda, Said Mourad, Joseph Owino, George Odhiambo ‘Blackberry’, Ibrahim Mwaipopo/Himid Mao Mkami, Kipre Herman Tcheche/Hamisi Mcha, Kipre Michael Balou/Abdulhalim Humud, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Gaudence Mwaikimba na George Odhiambo ‘Blackberry’/Zahor Pazi.
Katika mchezo wa baadaye leo, huenda kocha wa Simba Profesa Milovan Cirkovick akapanga kikosi hiki; Juma Kaseja, Haruna Shamte, Paul Ngalema, Lino Masombo, Shomary Kapombe, Amri Kiemba/Edward Chirtopher, Mwinyi Kazimoto/Salim Kinje, Mussa Mudde/Jonas Mkude, Felix Sunzu/Abdallah Juma, Kanu Mbivayanga/ Uhuru Suleiman na Danny Mrwanda/Abdallah Seseme.

No comments: