Saturday, January 9, 2016

Meneja kiwanda cha Dangote Mtwara kufikishwa mahakamani

Afisa Uhamiaji mkoa wa Mtwara, Naibu kamishna Zakayo Mchele, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya uwepo wa raia wa kigeni wapatao 360 wanaofanya kazi katika kiwanda cha Saruji cha Dangote Mtwara bila kuwa na vibali vinavyowaruhusu kufanya kazi hapa nchini, na kushikiliwa kwa meneja wa kiwanda hicho Vidya Sagar Dixit kutokana na kutotoa ushirikiano kwa maafisa wa Idara ya uhamiaji waliokwenda kiwandani hapo kutekeleza majukumu yao.


Na Juma Mohamed.

IDARA ya Uhamiaji mkoani hapa inamshikilia meneja wa kiwanda cha Saruji cha Dangote, Vidya Sagar Dxit kutokana na kubainika kwa uwepo wa raia wengi wa kigeni wanaofanya kazi kiwandani hapo bila kuwa na vibali vya kuwaruhusu kufanya kazi hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Afisa Uhamiaji mkoa wa Mtwara, Naibu kamishna, Zakayo Mchele, alisema hata hivyo meneja huyo hakutoa ushirikiano kwa maofisa wa uhamiaji walikwenda kiwandani hapo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao ya kazi kiasi cha kuwazuia kuingia ndani ya kiwanda hicho.
Alisema lengo la maafisa hao kutaka kuingia kiwandani humo ni kutaka kufanya ukaguzi kwa raia hao kutoka nchini China ambao jumla yao ni 360 kutokana na baadhi yao kudai kuwa waliwasilisha maombi yao ya vibali katika makao makuu ya Idara hiyo jambo ambalo alisema halina uhakika na juhudi zinafanyika ili kuweza kubaini ukweli.
“Wengine walibainisha kwamba maombi yalikuwa ‘submitted’ wengine hawana ‘details’ zozote kwasababu tulikosa ushirikiano kwa uongozi maana tulitaka kuhakiki mmoja baada ya mmoja na tulipeleka maafisa wengi kukagua mtu paspoti zake lakini hatukupata ushirikiano kwa ‘general manager’ na ikabidi tumkamate tulimleta hapa kusaidia Idara ya Uhamiaji na tutamfikisha mahakani kwa makosa ambaye ameyafanya.” Alisema.
Alisema zoezi la kufanya msako kwa wahamiaji haramu au raia wanaoishi nchini kinyume na taratibu ni utekelezaji wa agizo la Naibu waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mhe. Hamad Yussuf Masauni, na kwamba raia hao wengi wao wapo kiwandani hapo kwa muda wa miaezi mitatu hadi minne.
Alisema zoezi ni endelevu ambapo lilianza katika baadhi ya maeneo mkoani hapa ikiwa ni pamoja na mpakani mwa Tanzania na Msumbiji katika kijiji cha Kirambo na wilayani Tandahimba ambako huko waliweza kuwakamata raia 48 ambao walidai kuwa walisafirishwa kwa malori kutokea nchini Kenya.
“Na tulikamata raia wawili wa Msumbiji ambao walikuwa na hati za kupigia kura na hao tuliwandoa maeneo ya Mtambaswala..tunaendelea na uchunguzi wa makampuni mbalimbali ‘in facts’ ni zoezi endelevu na tulianzia Mikindani, tulienda kwenye kampuni ya Trade Aid ambao tuligundua kwamba wote wanaishi kihalali kuna raia wawili wa Uingereza ambao tuligundua wana vibali halali..”  alisema na kuongeza:
“Hii misako pia tunashiriksha wananchi, kwasababu wanaishi katika maeneo yale na wana ‘very interagency information’ ambazo zinasaidia katika idara ya utendaji wa kazi..hapa mkoani tuna maafisa 45 ambao ni maafisa wachache ambao hawawezi kufika maeneo yote, lakini tunategemea wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama, jeshi la wananchi na watu wa usalama.” Aliongeza.




No comments: