Friday, May 20, 2016

Wananchi watakiwa kufyatua Matofali ujenzi wa nyumba za walimu Madimba.




Walimu wa shule ya sekondari ya Madimba, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego (hayupo pichani) baada ya kufanya ziara shuleni hapo na kuzungumza na walimu kutaka kujua changamoto zao na kupokea maoni.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akipokea taarifa ya shule kutoka kwa mkuu wa shule ya sekondari ya Madimba, Ahmad Kwerendu, halmashauri ya wilaya ya Mtwara.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

WANANCHI wa kata ya Madimba, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, wametakiwa kushiriki kikamilifu zoezi la kufyatua Matofali lililolenga kutatua changamoto mbalimbali za miundombinu ya elimu zikiwamo nyumba za walimu na vyumba vya madarasa.
Agizo hilo limetolewa juzi mkoani hapa na mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, alipotembelea katika shule ya sekondari ya Madimba kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazoikabili shule hiyo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano anayoifanya mkoani mwake.
Mkuu huyo wa mkoa alimwagiza mwenyekiti wa kijiji cha Madimba, Mohamed Madiva, awahamasishe wananchi wake ili watekeleze zoezi hilo kwa haraka ili kutatua tatizo la uhaba wa nyumba za walimu ambalo linawakabili walimu wa shule hiyo ambao wengi wao ni wageni kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
“Kila kaya inakukusanyia matofali, wakitaka kufyatua kwa pamoja haya, wakiamua kila atafyatua atakuleta haya, mwingine atasema sitaki kushika tope nitanunua haya mradi mnatengeza kipimo ambacho watu wetu wameletewa kutoka halmashauri..sisi kule mtuachie tutafute bidhaa za viwandani kwa maana ya ‘cement’ na mabati..” alisema.
Alimtaka mkuu wa shule hiyo Ahmad Kwerendu, kuwa na tabia ya kufanya vikao na wazazi wa wanafunzi wa shule vitakavyosaidia kujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto zingine ndogondogo kulingana na uwezo wao.

Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akiongea na walimu pamoja na viongozi wa shule ya sekondari ya Madimba, halamashauri ya wilaya ya Mtwara, baada ya kufanya ziara ya kikazi shuleni hapo kukagua maendeleo ya elimu na kusikiliza kero na maoni ya walimu



“Zile siku za ‘graduation’ kwa wale ambao wanamaliza, utawaita wazazi na kuwa nao karibu lakini hata wewe pia ushiriki shughuli za kule kama vile kwenye ‘Ward C’ (Kamati ya maendeleo ya kata) wewe ni mjumbe..ule ushirikiano utakuwepo, sisi sasa hivi tumejikita kwenye madawati haya mpaka tarehe 30 mwezi Mei tutakuwa tumemaliza tatizo la madawati..” alisema.
Naye mwalimu wa shule hiyo, Herry Joseph, alisema licha ya kuupokea kwa mikono miwili mpango wa elimu bila malipo ambao unatekelezwa na serikali ya awamu ya tano, bado kuna changamoto kubwa kwa wanafunzi zaidi ikiwa ni ukosefu wa madawati na vyumba vya madarasa hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi kusomea katika vyumba vya Maabara.

Mkuu wa shule ya sekondari ya Madimba halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Ahmad kwerendu, akisoma taarifa ya shule yake mbele ya mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego alipofanya ziara shuleni hapo.


“Nawatakia kila la kheri katika kuitekeleza hiyo ilani, kikubwa madawati yamekosekana kwa kiasi kikubwa yanaathiri sana namna ya kujifunza kwa wale watoto..” alisema na kuongeza;
“lakini mengineyo ni sisite yanayohusu utawala, ninawaombeni sana kwamba sisi tunaofanya kazi katika maeneo kama haya tofauti na wanaofanya kazi huko halmashauri, tunaomba tuthaminiane tunavyoleta tatizo kwenye ngazi hizi zinazofuata chondechodne jaribu kuona kwamba huyu mtu anaeleta tatizo ni kwa ajili ya kulinda masialahi ya wale watoto wa mahali pale..” aliongeza Herry.
Mkuu wa shule hiyo, Ahmad Kwerendu, aliomba ushirikiano udumishwe baina ya uongozi wa shule, jamii pamoja na viongozi wa ngazi za juu ili kuweza kumaliza changamoto zilizopo.

No comments: