Thursday, May 12, 2016

DC Tandahimba awaweka ndani viongozi 37 wa vyama vya msingi>>>>> www.jumanews.blogspot.com



Mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Emmanuel Luhahula.




Na Juma Mohamed, Mtwara.

VIONGOZI 37 wa vyama vya msingi 26 vilivyo chini ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba, Newala Cooperation Union (TANECU), wamekamatwa na polisi kwa amri ya mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Emmanuel Luhahula kutokana na kushindwa kuwalipa wakulima wa kororsho malipo yao ya tatu.
Akizungumza na Juma News, mkuu huyo wa wilaya alisema, aliamua kutoa amri hiyo kwa kamanda wa polisi wa wilaya ya Tandahimba, kufuatia viongozi hao kushindwa kulipa deni hilo ambalo ni sh. Bilioni 1.2 kama fedha za malipo ya ziada kwa wakulima.
Awali deni hilo lilikuwa ni zaidi ya sh. Bilioni 1.4 ambapo vyama ambavyo vilikuwa vinadaiwa vilikuwa 49 kabla ya vyama 11 kulipa na kubakia vyama 38 ambavyo vimeshindwa kutekeleza agizo ambalo lilitolewa tangu Aprili 7 mwaka huu na kuwataka walipe ndani ya siku 7.
“Siku saba zilipoisha vyama 11 vilikubali kulipa, nikawapa muda mpaka tarehe Tisa mwezi watano kwa maana ya mwezi mzima ikawa ni vile vyama 11 tu ambavyo vimelipa na tumebakiza deni la Bilioni 1.2..kwahiyo jana (Mei 9) niliamua kuwakamata wote, nilimtumia OCD (Kamanda wa Polisi wa Wilaya) na kamati yangu ya ulinzi na usalama..” alisema.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya wilaya za Tandahimba na Newala, vilivyo chini ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba, Newala Cooperation Union (TANECU).



Alisema, kabla ya kukamatwa kwao, alipata taarifa kuwa viongozi hao wanafanya kikao katika eneo la Maghalani wilayani humo ndipo alipomuagiza katibu tawala wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri waandae magari kwa ajili ya kuwasafirisha kuwapeleka mahakamani wilayani Newala.
Alisema, ili kuhakikisha madeni hayo yanalipwa bila kujali kuwa wahusika watakuwa kizuizini, ameagiza kwa watendaji wa vijiji kuhakikisha wanafuatilia dhamana zao ambazo wote wameweka saini kuwa iwapo watashindwa kulipa fedha hizo ziuzwe mali zao kwa ajili ya kulipa.
“Nilichofanya, wajumbe wa bodi wote wako tisa kwa kila chama, wameshaandika dhamana zao ‘commitment letter’ za kuonesha kuyatambua madeni yao, kila ‘Body Member’ kwa nafasi yake amekiri kwamba hili deni nalitambua na hili deni nitalilipa kwa kuweka dhamana..ameweka aidha nyumba au shamba..” aliongeza.
Alisema yupo tayari kutoa ushirikiano kwa mahakama pale itakapohitajika juu ya uthibitisho wa watuhumiwa hao, na kwamba hategemei kuona mahakama ikianza kuzungusha kesi hiyo kwa kudai ushahidi wakati tayari vielelezo vipo.


No comments: