Saturday, May 14, 2016

Ndanda watia mchanga 'kitumbua' cha Yanga Taifa



wachezaji wa Ndanda na Yanga wakisalimiana kabla ya kuanza mchezo



Wachezaji wa Ndanda wakiwapigia makofi wachezaji wa Yanga wakati wanaingia uwanjani kwa ajili ya kuanza mchezo, kitendo hicho ni kutokana na Yangwa kutangwaza mabingwa huku ligi ikiwa bado haijamalizika.


Pongezi


Wachezaji wa Ndanda wakiwasubiri wachezaji wa Yanga waingie uwanjani ili wawapigie makofi




Wachezaji wa Ndanda wakipongezana baada ya kupata bao la kuongoza






Na Juma Mohamed, Dar es Salaam.

KUTOKA hapa uwanja wa Taifa Dar es Salaam, mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara kati ya wenyeji Ndanda Fc dhidi ya Yanga imemalizika huku timu hizo zikishindwa kutambiana baada ya kwenda sare ya magoli 2-2.
Ndanda walianza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 28 mfungaji akiwa ni Omary Mponda kwa mkwaju wa penaiti baada ya mshambuliaji Atupele Green kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari, ambapo bao hilo lilidumu kwa dakika sita kabla ya Saimon Msuva kuisawazishia Yanga baada ya kuunganisha krosi ya Geofrey Mwashiuya.

Kipa wa Yanga akijaribu kuufuata mpira wa penalti uliopigwa na Omary Mponda na kuifungia timu yake ya Ndanda bao la kuongoza



Dakika ya 40, Donald Ngoma aliipatia Yanga bao la pili baada ya kugongeana vyema na washambuliaji wenzake, na kuifanya Yanga waende mapumziko ikiwa kifua mbele kwa mabao 2-1.
Kabla ya kwenda mapumziko, Ndanda walifanya mabadiliko ya mapema baada ya kocha Malale Hamsini kuamua kumtoa Buruhan Rashid na kumuingiza Salum Minelly.
Mabadiliko hayo yalizaa matunda kipindi cha pili baada ya Minelly kuisawazishia Ndanda bao kufuatia shambulizi la kushtukiza langoni mwa Yanga.
Kipindi cha pili Yanga walifanya mabadiliko ya kuwatoa Mwinyi Haji, Donald Ngoma na Haruna Niyonzima na nafasi zao kuchukuliwa na Matheo Damian, Oscar Joshua na Mbuyu Twite lakini hata hivyo hayakuwa na faida kwao kwasababu mpaka dakika 90 zinamalizika matokeo yalikuwa ni mabao 2-2.

Wachezaji wa Yanga wakipongezana baada ya kupata bao la kusawazisha



Kadi za njano zilitoka kwa wachezaji Kigi Makassy na Azizi Sibo wa Ndanda pamoja na Kalvin Yondan wa Yanga kwa kucheza madhambi.
Mfungakji wa bao la kusawazisha kwa Ndanda, salum Minelly, alisema amejiskia furaha kufunga goli lake la kwanza tangu aanze kucheza ligi kuu na timu yake hiyo lakini zaidi ni kuifunga timu ya Yanga na kuahidi kuendeleza kufunga katika mchezo mmoja uliobaki dhidi ya Mbeya City na michezo mingine ya msimu ujao.


No comments: