Wanafunzi wa shule ya msingi Nanyati. |
Wanafunzi wa shule ya msingi Nanyati. |
Na Juma
Mohamed.
WAKATI
Halmashauri ya wilaya ya Mtwara vijijini mkoani hapa ikijidai kwa mafanikio ya
kuongoza kimkoa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba, baada ya kutoa
shule tatu bora, wanafunzi wa shule ya msingi Nanyati, kata ya Mkunwa katika
halmashauri hiyo wanalazimika kusomea chini ya mti kutokana na kukosa madarasa.
Shule hiyo
iliyoanzishwa miaka mitatu iliyopita ambayo ina jumla ya wananfunzi 210 kuanzia
darasa la awali mpaka la tatu, inakabiliwa na changamoto lukuki huku zaidi
ikiwa ni vyumba vya madarasa ambapo kuna chumba kimoja kinachotumiwa na
wanafunzi wa darasa la pili huku wale wa awali na darasa la tatu wakisomea
chini ya mti.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nanyati, Shaibu Hoja, akielezea changamoto zinazoikabili shule hiyo |
Akizungumza
na Nipashe shuleni hapo, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Shaibu Hoja, alisema
changamoto nyingine zilizopo ni uhaba wa walimu ambapo mpaka sasa shule ina
walimu wawili wa serikali na mmoja wa kujitolea, jambo ambalo linapelekea
wanafunzi kukosa masomo inapotokea mwalimu mmojawapo amepatwa na dharula ya
kutohudhuria kazini kwa muda Fulani.
Alizitaja
changamoto nyingine, kuwa kukosa vyoo, nyumba za walimu, ofisi za walimu pamoja
na ukosefu wa madawati ambapo yaliyopo ni madawati 26 huku shule ikihitaji
madawati 88.
Alisema, kwa
kukosa madarasa, wanafunzi wanakuwa katika mazingira magumu ya kupata masomo
hasa kinapofika kipindi cha mvua kwasababu wanalazimika kukimbia kueudi nyumbni
kwao na kukatisha masomo.
“Mpaka sasa
shule ina madarasa matatu pamoja na la awali na kufanya idadi ya madarasa
manne, lakini sasaivi shule ina chuma kimoja tu kilichokamilika na kingine bado
hakija kamilika..tunaongea huu ni mwezi wa 11, Januari tunataka kuanza darasa
la nne lakini chumba kilichokamilika ni kimoja, inamaana madarasa manne yatakua
nje hayana mahala pakusomea..changamoto yatatu ni ukosefu wa madawati, kwani
nilitonayo ni 26 tu na ninahitaji nipate madawati 88..” alisema.
Na kuongeza,
“ile changamoto ya kukosa madarasa imechukua nafasi ya kwanza kwasababu
wanafunzi wanasomea chini ya miti, wanasumbuliwa na mvua, jua kali, wanapata
maumivu ya vichwa kwa kukaa maeneo yanayopitisha jua, wanaloa maji na mvua
inaponyesha na shule inafungwa siku hiyo hata ikiwa siku tatu hakuna shule..”
aliongeza.
Aliziomba
serikali za kijiji na halmashauri ya wilaya kushughulikia kero hizo kwa haraka
ili kuwaokoa wanafunzi hao kuondokana na vikwazo hivyo katika kujitafutia
elimu.
Wanafunzi wa
shule hiyo, wameitaka serikali kuwatatulia changamoto hizo ambazo wamezitaja
kuwa ni kikwazo katika safari yao ya kujipatia elimu kutokana na muda mwingi
kukosa masomo hasa pale inaponyesha mvua na inapotokea mwalimu mmoja
amekosekana.
“Tupate
viwanja vya mpira, tupate madarasa, tupate madawati..wanafunzi wengi wanakaa
chini, tunasomea chini ya mkorosho, uandikaji wetu ni wa matatizo na mvua
inatunyeshea na tunarudi nyumbani tunakosa masomo..mwalimu akimwa tunafunga
shule tunakosa kusoma, mimi inaniuma sana..” alisema Asha Selemani, mwanafunzi
wa darasa la tatu.
Nao,
wananchi wa kijiji hicho ambao nguvu zao kwa pamoja ndio zimefanikisha ujenzi
wa shule hiyo, wameitaka serikali kuwasaidia kuboresha miundombinu ya shule na
kuongeza eneo kwa kuwahamisha wananchi wanaoishi kuizunguka sule hiyo.
“Pia
serikali tunaiomba itujengee choo cha kudumu kwa ajili ya wale watoto kwasababu
tulichonacho ni cha muda mfupi..pia itupatie walimu wakutosha kwasababu
hatukuanzisha ile shule iwe kwa ajili ya wanakijiji pekee, na tunawapokea
watoto kutoka vijiji jirani wanaokuja kusoma hapa.” Alisema Issa Chonga.
Naye, Fidea
Chiponde, ambaye ni wenyekiti wa kamati ya shule, alisema shule inamahitaji
katika sehemu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na waalimu ambao wanahitajika wapatao
wanne, madarsa matano, matundu manane ya vyoo pamoja na nyumba saba za walimu,
huku wakkabiliwa na changamoto nyingine ya ukosefu wa vitendea kazi.
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Nanyati, Fidea Chiponde, akielezea changamoto za shule hiyo. |
Alisema bado
hawajapata msaada kutoka serikalini ukiachiliambali fedha sh. Milioni 3 kutoka
halmashauri ambazo zilitumika katika ujenzi wa darasa moja ambalo hata hivyo
bado halijakamilika, pamoja na msaada uliotolewa na mbunge wa jimbo la Mtwara
vijijini, Mhe. Hawa Ghasia, ambaye alichangia mabati 100.
Katika hatua
nyingine, wakazi wa kijiji hicho wanakabiliwa na ukosefu wa Zahanati kiasi cha
kulazimika kusafiri umbali mrefu wa hadi km 5 kufuata huduma hiyi inayopatikana
kijiji jirani na kupelekea baadhi ya kina mama wajawazito kujifungulia
majumbani mwao.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Nanyati, akizungumzia kero za kjijini hapo zinazowakabili wananchi |
Mtendaji wa
kijiji hicho, Hassan Mohamed, alisema anapata malalamiko mara kwa mara kutoka
kwa wananchi wake juu ya hadha wanayoipata kutokana na ukosefu wa huduma hiyo
ambayo inapatikana katika kijiji cha Kawawa.
Alisema,
wadau wa afya waliwahi kutembelea kijijini hapo na kutaka kujua jamii imefikia
wapi katika jitihada za kuanza kutatua tatizo hilo ambapo waliambiwa kuwa
tayari limepatikana eneo kwa ajili ya ujenzi lakini imeshindikana kuanza kwa
wakati kutokana na kutatua kero ya elimu ambayo bado inategemea nguvu za
wananchi.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Mtwara vijijini, Tamimu Komba, akifafanua juu ya changamoto zinazolalamikiwa na wakazi wa Nanyati kuhusu huduma za kijamii. |
Kwa upande
wake, kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tamimu Kambona, ambaye pia ni afisa
elimu shule za msingi, akizungumzia changamoto za shule, alisema wanazo taarifa
juu ya shle hiyo na kwamba tatizo lililokwamisha ujenzi wa madarasa ni kutokana
na kuwekeza nguvu nyingi katika ujenzi maabara ambao ulitiwa mkazo na mkuu wa
mkoa kwa kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete.
Alisema
juhudi zinafanyika katika kutekeleza ujenzi wa shule hiyo, ambapo bajeti ya
mwaka 2015/2016 yatatekelezwa hayo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo
unaotegemewa kutekelezwa kupitia wafadhili wanaoshughulikia katika sekta hiyo.
“Makusanyo
ya mwaka jana mengi yalikimbilia katika ujenzi wa maabara, tulishindwa
kukamilisha lile, lakini nafikiri kwa mwaka huu sasa nguvu yetu tutaielekeza
huko baada ya kukamilisha maabara..kuhusu suala la walimu ni kweli kuna walimu
wawili, na ikitokea mmoja ni mgonjwa tayari kunakua na shida, tumeliona hilo na
kwa mwaka huu kwa bahati mbaya TAMISEMI haikutupatia mwalimu hata mmoja, lakini
tunafanya juhudi ifikapo likizo ya mwezi Desemba tuweze kufanya uhamisho..”
alisema.
Alisema,
walishindwa kufanya uhamisho kipindi hiki kutokana na kukumbwa na madeni ya
fedha za uhamisho ambazo zilifikia zaidi ya milioni 70, lakini kwasasa madeni
hayo yamelipwa na serikali na uwezekano wa kufanya uhamisho upo.
Kuhusu suala
la zahanati, aliwataka wananchi kuwa na subira kwani zamu yao itafika kwasababu
sera ya taifa ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kwahiyo kwasasa
kuna vijiji ambavyo vinatekelezewa huduma hizo na baada ya hapo yatafuata
maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Nanyati.
No comments:
Post a Comment