Tuesday, November 3, 2015

Mama Makaidi awachimba mkwara CCM Uchaguzi wa Lulindi.

Bi Modesta Makaidi, akiwa na aliyekuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Dekrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiungwa mkono na UKAWA, Mhe, Edwatd Lowassa. wakati wa moja ya mkutano wa kampeni wilayani Masasi.(PICHA-MTANDAO)



Na Juma Mohamed.

Mgombea Ubunge wa chama cha National League for Democracy (NLD) katika jimbo la Lulindi, wilayani Masasi, mkoani hapa, Modesta Makaidi, amewataka makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutorudia vitendo vya kugawa kanga na unga kwa wananchi ili kuwashawishi kumchagua mgombea wao katika uchaguzi ujao jimboni humo.
Akizungumza na wilayani humo, amesema siku moja kabla ya kupiga kura katika uchaguzi wa ubunge ambao bado haujapangwa, atapita kila kijiji kwa ajiji ili kuwabaini watakofanya hivyo ambao ameahidi kuwashushia kipigo kwa kutumia vijana wake.
Alisema, makada hao walifanya hivyo awali katika kipindi cha kampeni kabla ya tume kuahirisha uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo kutokana na dosari katika karatasi ya mgombea mmoja, na kwamba alishindwa kuwachukulia hatua kutokana na kukubwa na msiba wa mume wake, Dkt. Emmanuel Makaidi, ambaye alikuwa mwenyekiti mwenza wa vyama vinavyounda UKAWA.

Modesta Makaidi (PICHA-MTANDAO)


“Siku moja kabla ya kupiga kura nitapita kila kijiji..sisi hatutakua na uwezo wa kuwakamata na kuwapeleka TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) katikati tutashindwa, nitaalika vijana ‘wakung’utwe’ wote wanaopokea na wanaotoa, kwasababu CCM haitaki amani na haitaki kuingia madarakani kwa mapenzi ya wananchi.” Alisema.
Aliongeza kuwa, wananchi wa jimboni humo wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha na kipato chao ni hali ya chini, hivyo ni rahisi kurubuniwa kwa kupewa hongo ili kuwabadilisha kisiasa.
Aidha, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza mapema tarehe rasmi ya kufanyika uchaguzi huo ili wananchi ambao ndio wapiga kura waweze kujiandaa na kupanga vizuri ratiba zao kutokana na wengi wao kuwa na majukumu mengine hasa ya kilimo.
Alisema, awali wananchi walitangaziwa kuwa wangepiga kura Oktoba 28 lakini ilishindikana na kwamba msimamizi alilazimika kutangaza tarehe hiyo ili kutuliza morali ya wananchi ambao walikuwa na kiu ya kutaka kupiga kura ya kuchagua wabunge wao.
“wananchi wametaharuki, waliambiwa tarehe 28 na wasimamizi na wasimamizi walisema vile kwa kutaka kujinusuru na wasinge sema vile wangefanyiwa vurugu siku ile..sasa wanataka tarehe maalumu ili wajiandae kwasababu sasaivi ni kipindi cha kulima watu wako mashambani..” aliongeza.
Alimtaka msimamizi wa uchaguzi kutenda haki kwa kumtangaza mgombea atakeshinda kihalali baada ya uchaguzi, ili kuhepusha shari kwasababu wananchi watamjua mshindi kupitia matokeo yakayobandikwa katika vituo vyao vya kupigia kura.




No comments: