Wednesday, November 30, 2016

DANGOTE waibuka na kueleza sababu za kusitisha uzalishaji


Kiwanda cha Dangote Mtwara.



Juma Mohamed, Mtwara

Baada ya kuenea kwa taarifa takribani wiki mbili sasa juu ya kusitishwa kwa uzalishaji katika kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited mkoani Mtwara, uongozi wa kiwanda hicho umeibuka na kusema kuwa kusitishwa huko kumetokana na tatizo la hitilafu za kiufundi.
Akizungumza kwa niaba ya afisa mtendaji mkuu wa kiwanda hicho Harpreet Duggal, mkuu wa usalama wa kiwanda hicho, Benedict Kajukano alisema kiwanda kimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na tatizo hilo na kudai kuwa mafundi wanaendelea na kazi kwa ajili ya kurejesha huduma.
Aidha, amekiri kuwa kiwanda hicho kinatumia gharama kubwa za uzalishaji ukilinganisha na viwanda vilivyopo maeneo mengine, hali inayosababishwa na matumizi ya jenereta za mafuta ya Dizeli katika kuendesha kiwanda.
Hata hivyo, mkuu huyo wa usalama hakutoa nafasi kwa waandishi wa habari kuweza kumuuliza maswali kwa ajili ya kupata ufafanuzi zaidi kwa madai kuwa sio msemaji wa kiwanda hicho, huku wafanya biashara Saruji na bidhaa mbalimbali wakieleza kuathirika kwao.
Kiwanda hicho chenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 600, kina uwezo wa kuzalisha tani Milioni Tatu kwa mwaka na kutoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1,000 wa Mtwara

No comments: