IKIWA
imebaki siku moja kabla ya watanzania wapenda soka na Afrika kwa ujumla
kuelekeza macho na masikio nchini Kongo DRC, huko Lubumbashi ambako watanzania
wawili, Mbwana Ally Samatta na Thomas Ulimwengu wataiwakilisha Tanzania katika
mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), kati ya
wenyeji TP-Mazembe ambao watawakaribisha waarabu wa Algeria, USM Alger, haya ni
mambo muhimu kuyatambua kabla hujatazama mchezo huo.
-Baada ya
kupatikana bingwa mpya wa michuano hiyo ambaye atampokonya taji Al-Ahli ya
Misri, atakwenda kuliwakilisha bara la Afrika katika fainali za klabu bingwa ya
dunia ambazo zitafanyika nchini Japani.
-Wakati USM
wakiingia kwa mara ya kwanza katika fainali ya Champions League toka kuanzishwa
kwa klabu hiyo miaka 78 iliyopita, Mazembe wamechukua ubingwa wa Afrika mara 4
na sasa wanaufukuzia ubingwa wa 5.
-Tangu
kuanza kwa michuano hiyo mwaka 1965, Mazembe ambayo ilianza kucheza michuano
hiyo ikifahamika kama TP-Englebert, imecheza mechi 77 katika uwanja wa nyumbani
na kufanikiwa kushinda mara 59, sare mara 15 na kupoteza mara 3.
-Mara ya
mwisho kufungwa katika uwanja wa nyumbani, Mazembe ilikuwa ni mwaka 2009,
ambapo ilifungwa na Al-Hilal Omduman, ya Sudan kwa magoli 2-0 katika mchezo wa marudiano.
Katika mchezo wa kwanza ambao ulichezwa Omduman, Sudan, Mazembe walishindwa kwa
mabao 5-2, na kuwafanya wafuzu kucheza fainali kwa kukutana na Heatland ya
Nigeria ambapo baadaye walifanikiwa kutwaa ubingwa.
-Ushindi wa
magoli 2-1 walioupata Mazembe nchini Algeria ni wakwanza, katika mara sita
walizokwenda kucheza nchini humo na timu tofauti.
-USM hawana
matokeo mazuri ya kushinda ugenini/nje ya nchi yao, michezo mingi walioshinda
ugenini wameshinda nchini mwao katika hatua ya makundi.
-Ushindi
pekee walioupata nje ya Algeria ni pale walipowafunga Al-Hilal magoli 2-1.
-Ili USM
waweze kutwaa ubingwa wao wa kwanza, wanatakiwa wapate angalau ushindi sio
chini ya magoli 2-0, lakini matokeo chini ya hapo yatawapa Mazembe ubingwa.
-Wachezaji
wawili wa USM ambao ni Youcef Belaili na Hocine El Orfi, watakosekana katika
mchezo wa Jumapili. Belaili, ana adhabu ya muda mrefu kutokana na kesi ya
matumizi ya dawa za kulevya, huku El Orfi akiwa anatumikia adhabu ya kadi
nyekundu ambayo aliipata katika mchezo uliopita.
Ptrice Carteron
Kocha wa
Mazembe, mfaransa, Patrice Carteron, alikiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu na
lolote linaweza kutokea hapo Jumapili, licha ya kucheza nyumbani.
“Tunaujua
ubora wa USM. Ni timu nzuri katika michuano hii, na walifanya vizuri katika
baadhi ya michezo yao ya ugenini na wanaweza kutushangaza.”
“Algeria
wanafahamika kwa ubora wao ambao unawafanya waweze kuamua mchezo katika
mazingira yoyote. Lazima tuupe uzito wa kipekee mchezo huu.” Alisema.
Aidha,
aliwaahidi mashabiki kuwa timu yao itacheza kwa kushambulia kama kawaida yao.
| Patrice Carteron |
“Tumeshinda
ugenini, tuna namna nyingi za kufanya. Lakini bado tutacheza kwa tahadhari
kubwa na kwa kujilinda..mashabiki wetu wanapenda soka safi na tutawaridhisha. Hatuna
namna, timu yetu lazima icheze kwa kushambulia.” Aliongeza.
Mazembe,
watawakosa nyota wao wawili ambao ni mfungaji mahiri wa Zambia, Rainford
Kalaba, ambaye alipata kadi nyekundu katika mchezo wa kwanza, na Jean Kasusula,
ambaye anasumbuliwa na mkono alioumia baada ya kupata ajali ya pikipiki
Jumapili iliyopita aliporejea Lubumbashi wakitokea Algeria. Mlinzi huyo atakuwa
nje ya uwanja kwa majuma kadhaa.
Mchezaji
ambaye anategemewa kurejea uwnjani hapo Jumapili, ni Nahodha, Joel Kimwaga,
ambaye alikuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano alizopata katika hatua ya
makundi.
Naye, kiungo
wa timu hiyo raia wa Ghana, Daniel Nii Adjei, amewaonya wenzake kuelekea katika
mchezo huo.
“Bado kazi
haijaisha, tumeshinda mara moja lakini chochote kinaweza kutokea katika mchezo
wa pili..wanweza kuja Lubumbashi na wakatuduwaza. Tunatakiwa kujiandaa vizuri
ili tuwafunge na tuchukuwe ubingwa.” Alisema.
No comments:
Post a Comment