Monday, November 9, 2015

Wananchi kata ya Shangani wafanya sherehe ya kumpongeza Diwani..


Diwani wa kata ya Shangani, manispaa ya Mtwara Mikindani, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ahmad Mbarale, akifurahi kwa pamoja na wananchi wa kata yake, ambao waliandaa hafla ya kumpongeza kwa kuwa mshindi wa kata hiyo


Wananchi wa kata ya Shangani, Manispaa ya Mtwara Mikindani, wakifurahi kwa pamoja katika hafla ya kumpongeza Diwani wao kutokana na kushinda uchaguzi, Ahmad Mbarale, wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)

 Na Juma Mohamed.

WANANCHI wa kata ya Shangani, manispaa ya Mtwara Mikindani, waliandaa hafla ya kumpongeza Diwani wao mteule kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ahmad Mbarale, baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu uliopita.

Wananchi hao wamemtaka diwani huyo kushughulikia na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili ikiwa ni pamoja na changamoto zinazowakabili akina mama katika hospitali ya rufaa ya Ligula wakati wa kujifungua.
Katika hafla hiyo, baadhi ya kina mama wameelezea kutoridhishwa kwao na huduma za uzazi zinazotelewa katika hospitali hiyo.
Fatuma Namanoro, alisema wamemchgua diwani huyo ili awe kimbilio la wanawake kutokana na kukabiliwa na changamoto nyingi hasa upande wa afya, ambapo alisema kumekuwa na lugha zisizo nzuri kwa wahudumu wakati wanapokwenda kujifungua hospitalini hapo.
Alisema, awali kupitia sera za Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kilikuwa kinaongoza kata hiyo, waliambiwa kuwa huduma za uzazi kwa kina mama zitakuwa zinapatikana bure lakini imekuwa tofauti.
“Sasaivi wanawake tunazaa kule hospitali tunaambiwa tulete kilakitu ni juu yetu, sasaivi wale ambao wanatuhudumia inakuwa ni maneno matupu, wanatupwa nje, manesi wanakuwa ni wakali wakati sivyo inavyotakiwa, nesi anatakiwa awe mpole kutokana na kazi yake..wanawake tunateseka, kwahiyo ndio maana sasaivi tumeona tufanye haya mabadiliko katika uchaguzi ili tuwapate watu wengine, na mungu ametujaalia tumepata UKAWA na tumepata ‘jembe’..” alisema.
Alisema, anaimani kuwa diwani huyo atakuwa na msaada mkubwa kwa wananchi hasa wanawake, na atakuwa ni mtu wa kusikiliza na kutatua kero sio tu kwa wanawake wa Chadema, bali ni kwa wanawake wote.
“Diwani tuliyemchagua Ahmad Mbarale, tunahitaji atusaidie kama ‘wamama’hasa katika kituo cha afya cha hospitali ya Ligula, tunapokuwa tunajifungua huduma ni za shida, tunahitaji atutetee kama wanawake..na kwenye vikundi mbalimbali kwa ahadi alizoziaidi tunahitaji azitekeleze kama alivyoahidi katika manispaa akazitekeleze hasa wanawake asituangushe kwa sera zote alizozitoa..” alisema Monica James, mkazi wa mtaa wa Ligula.
Akitolea ufafanuzi wa namna ya kutatua kero za afya kwa kina mama wakati wa kujifungua, diwani huyo alisema wataboresha Zahanati zilizopo katika kata hiyo ambazo ni Zahanati ya Shangani na Zahanati ya Polisi, ambapo alisema mkakati uliopo ni kuziongezea uwezo na kuhakikisha kunakuwa na vifaa tiba ambavyo vitawawezesha kina mama kujifungulia pasipo kuwa na matatizo.
“Kumekuwa na malalamiko makubwa sana ya huduma za kina mama katika hospitali ya Ligula ambayo ni hospitali ya rufaa, ile ni hospitali ya mkoa na ya wilaya pia, japo haipo kwenye kata yangu lakini inagusa kata zote, kitu cha kwanza tukiingia katika baraza la halmashauri tutajaribu kutembelea pale ili kuweza kugundua wenyewe kwa macho yetu ili iwe rahisi kutatua kero hizo..´alisema.
Alisema, moja ya jitihada atakazozifanya ni kutafuta wafadhili ambao anaamini kupitia wao kero hizo zitapungua kwa kiasi kikubwa kama sio kwisha kabisa, pamoja na kuishinikiza serikali iweze kuandaa bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutatua kero hizo ambazo zinalalamikiwa katika maeneo mengi ya huduma za afya.  
Kwa upande wake, mbunge mteule wa viti maalumu kupitia Chadema, Tunza Issa Malapo, alisema atashirikiana ipasavyo na mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maftaha Nachuma, kuhakikisha wanatetea masilahi ya wananchi wa Mtwara hasa akina mama juu ya kero wanazozipata wakati wa kujifungua.
“Kina mama walikua wanalala chini pale Ligula hospitali wakati wanasubiri watu wajifungue, sisimizi wakwetu, mvua yakwetu, jua lakwetu ‘Ngwangwalati’ wakwetu..tunasema imetosha, na nilikuwa nasema katika mikutano yangu, hawa madiwani na sisi wabunge kama hatutekelezi haya 2020 ‘mtupi chini’..” alisema.



No comments: