WATU watatu
wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa kutokana na kukutwa na vifaa
mbalimbali vya milipuko vinavyotumika katika uvuvi haramu wa kutumia baruti
katika bahari ya Hindi, katika oparesheni maalumu ya kuwakamata wanaojihusisha
na mtandao huo.
Wanaoshikiliwa
kutokana na oparesheni hiyo iliyofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na
Marine Park pamoja na kikosi maalum cha Taifa kinachoshughulikia uhifadhi wa
mazingira pamoja na Bahari, ni Mussa Kais (30), Dadi Selemani (31) na Hose
Chikota (24) ambao ni wakazi wa Mtwara vijijini.
Akizungumza mapema leo na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ACP-Henry Mwaibambe,
alisema katika upekuzi walioufanya juzi usiku nyumbani kwa Musa Kais,
walifanikiwa kukamata Viwashio (Fuse) 44, Detonator 39, Explogel-Nusu kipande,
Daftari moja la mauzo ya vifaa, fedha kiasi cha sh. 353,000 pamoja na simu moja
aina ya Tecno.
Aidha,
alisema watuhumiwa wengine katika nyakati tofauti, walikamatwa na malighafi za
kutengenezea milipuko hiyo ambayo ni, Mbolea Kg 6, Kg tatu zikiwa
zimechanganywa na Explogel, Chupa sita za milipuko ambazo zilikuwa tayari
zimechanganywa kwa ajili ya kulipuliwa, waya wa vilipuzi wenye urefu wa mita
tano na nusu na vipande vingine, pamoja na Majongoo ya Bahari 55.
“Wito kwa
wananchi wa Mtwara, watu hawa ni maadui wa maendeleo ya Mkoa wa Mtwara, watu
hawa ni hatari sana..ninaimani ndani ya miezi mitatu au mine ijayo kutakuwa
hakuna samaki Mtwara, hivi vitu ni hatari sana na vinaharibu mazalia ya samaki
na samaki wenyewe..Mtwara ni mkoa wa uwekezaji tunafahamu hayo nadhani watu ni
wengi wako hapa, watu hawa ni maadui zetu wote na tusiwaone mafahari, tuwaone
kuwa ni maadui..” alisema.
Alisema, ni
wajibu kwa wananchi wa Mtwara kushirikiana na jeshi la polisi kuweza kuutambua
mtandao huo na kuwakamata, na kwamba watuhumiwa hao wanahojiwa na baada ya muda
mfupi watafikishwa mahakamani.
“Naomba
tuendelee kuwahamasisha wananchi, hawa watu hawafai kabisa, kuna maali nimewahi
kukaa katika maisha yangu, maeneo ambayo wanatumia uvuvi wa namna hii hamna
samaki kabisa..kwahiyo tushirikiane, hii vita sio ya polisi pekee ni vya jamii
nzima..” aliongeza.
No comments:
Post a Comment