Thursday, November 12, 2015

Stakabadhi Ghalani bado kikwazo wilayani Tunduru


Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mfaume Juma, akizungumza na waandishi wa habari juzi mkoani Mtwara, juu ya mwenendo wa msimu wa ununuzi wa Korosho Ghafi kwa mwaka 2015/2016



Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mfaume Juma, akizungumza na waandishi wa habari juzi mkoani Mtwara, juu ya mwenendo wa msimu wa ununuzi wa Korosho Ghafi kwa mwaka 2015/2016


Na Juma Mohamed.

BODI ya Korosho Tanzania imesema haiko tayari kushirikiana kwa namna yoyote na uongozi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kutokana na wilaya hiyo kukataa kununua korosho kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao upo kisheria.
Kupitia mfumo huo, wakulima wanakusanya korosho zao kwenye vyama vya ushirika vya msingi na baadaye maghala makuu, ambapo kupitia vyama vikuu chini ya usimamizi wa Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na Sekretarieti ya mkoa husika, korosho huuzwa kwa ushindani kwenye minada inayofanyika mara moja kwa kila wiki.
Akizungumza juzi mkoani hapa katika kikao na waandishi wa habari juu ya mwenendo wa msimu wa ununuzi wa korosho ghafi kwa mwaka 2015/2016, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Mfaume Juma, alisema licha ya jitihada zilizofanywa na Bodi kurejesha mfumo huo, lakini uongozi wa wilaya hiyo umekataa kukubaliana nao.
Alisema, kitendo cha wilaya hiyo kuukataa mfumo huo ambao ulikumbwa na changamoto katika msimu wa mwaka 2011/2012 kutokana na soko la korosho kuyumba na kupelekea kutouzika, ni kinyume na sheria ya Tasnia ya korosho Na. 18 ya mwaka 2009 na kanuni zake za mwaka 2010 ambao umetoa vibali kwa wanunuzi kununua korosho moja kwa moja kutoka kwa wakulima.

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mfaume Juma.

“Kwakuwa nchi yetu inaoongozwa kwa kufuata misingi ya kisheria, Bodi ya Korosho haiko tayari kushirikiana na uongozi wa wilaya ya Tunduru kukiuka misingi hiyo. Hivyo kwa mnunuzi yeyote wa korosho ghafi atakayejihusisha na ununuzi wa korosho kinyume na utaratibu wa kisheria uliowekwa na Bodi ya Korosho, atakuwa ametenda kosa na Bodi haitasita kumchukulia hatua kwa mujibu wa sheria..” alisema.
Alisema, katika msimu wa 2011/2012 changamoto kama hiyo iliwahi kutokea katika mkoa wa Pwani lakini Bodi iliweza kukabiliana nayo na hatimaye kufanikisha kuurejesha mfumo huo ambao umeanza tena kutumika katika msimu huu katika mkoa huo.
Alisema, njia pekee ya wakulima wa Tunduru kuuza korosho kwa ushindani ni kupitia mfumo huo ambao unawawezesha wakulima kukusanya korosho zao katika ghala kuu na kuuza kwa mnada kwa kupitia vyama vyao vya msingi.

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Mfaume Juma.

“Kwa msimu huu suala la mfumo wa stakabadhi ghalani limewezekana sio tu kwa mikoa ya Mtwara na Lindi, bali pia kwa wenzetu wa mkoa wa Pwani ambao misimu mitatu iliyopita hawakuweza kufanya hivyo..kwa mara ya kwanza wakulima wa mkoa huo katika mnada wao wa kwanza uliofanyika Novemba 4 mwaka huu wameweza kuuza korosho kwa bei mzuri ya sh. 2,320 kwa kilo..” alisema.
Alielezea changamoto nyingine inayoikabili Bodi hiyo kuwa ni ununuzi holela wa zao hilo maarufu kama Kangomba/Choma choma, ambapo baadhi ya wadau wamekuwa na hisia tofauti kwa Bodi kwa kudhani kwamba inawaunga mkono wanaotekeleza hujuma hiyo inayofanyika nje ya mfumo wa stakabadhi ghalani.
“Ndugu wanahabari kuhusu changamoto hii, kwanza Bodi ya Korosho inapenda kukanusha kuwa haiko nyuma ya mtu yeyote anayejihusisha na ununuzi holela wa korosho..yeyote anayejihusisha na ununuzi holela anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwemo kutaifisha korosho alizonunua nje ya mfumo wa stakabadhi galani..” alisema.
Aliwataka wadau wa zao hilo hasa serikali za mitaa katika maeneo yanayozalisha, kushirikiana na Bodi katika kuhakikisha wanakomesha ununizi holela wa Korosho.
 Aidha, Bodi imekumbwa na changamoto nyingine ya usafirishaji wa zao hilo, ambapo ilipewa maagizo na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara kupitia kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kuwa korosho za mkoani hapa zisisafirishwe kwa njia ya Barabara kwenda katika bandari ya Dar es Esalaam na baadala yake itumike bandari ya Mtwara ili kuipa fursa bandari hiyo kutumika kikamilifu kwa kukuza uchumi wa Mtwara na wananchi wake.
Mfaume, alisema licha ya jitihada za Bodi za kufanya vikao kadhaa kwa kukutana na wadau husika wa pande zote ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Banfari Tawi la Mtwara na Wakala wa Meli za Kubeba Korosho Bandari ya Mtwara, utekelezaji wa agizo hilo umekuwa ni mgumu kutokana na changamoto iliyopo katika bandari ya Mtwara hasa uchache wa meli za mizigo zinazoingia na upungufu wa magati.
Aliyataja baadhi ya madhara ambayo yanaweza kujitokeza iwapo hali hiyo haitobadilishwa kuwa ni pamoja na maghala makuu kufurika pamoja na wakulima kukosa maghala ya kukusanyia korosho kwa ajili yam nada.
Madhara mengine ni Mikataba ya kimataifa ya wanunuzi kuvunjika kutokana na korosho kutosafirishwa kwa wakati ili ziwafikie wateja walioko nje, jambo ambalo linaweza kusababisha hasara kubwa kwa wanunuzi na wakulima kukosa soko nzuri.
Tayari minada minada miwili ya kuuza korosho imefanyika msimu huu katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambapo mnada wa kwanza ulifanyika Oktoba 2 mkoa wa Mtwara, huku mnada wa kwanza kwa mkoa wa Lindi ukifanyika Oktoba 17 katika kituo cha Lindi mjini.
“Mpaka sasa wiki tano zimepita tangu minada ya korosho ianze kufanyika msimu huu. Korosho zilizokusanywa maghala makuu na kuuzwa kati ya Oktoba 2 hadi Novemba 8 mwaka huu ni Tani 57,252.450..korosho hizo zimeuzwa kwa bei ya ushindani kati ya sh. 2,407 hadi sh. 2,620 kwa kilo.” Alisema.



No comments: